Makala/Tahariri

Miaka 51 ya shuruti la muungano wa Tanganyika dhidi Zanzibar

Awadh Ali Said

Fakhari iliyozoeleka katika maadhimisho ya kila mwaka ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964 kwa kusainiwa Hati za Makubaliano ya Muungano kulikofanywa na Marais wa Mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar ni kuhisabu umri wa Muungano wenyewe na kujipa maliwazo kuwa Muungano umeendelea kudumu. Hatuna mazowea ya kutathmini afya na uimara wa kweli wa Muungano wenyewe.

Pengine kufanya hivyo kunaweza kuhesabiwa kuwa ni sawa na kuunyanyapaa Muungano. Lakini ukweli mchungu ni kuwa Muungano huu umedumishwa kwa gharama kubwa katika muktadha wa maendeleo ya kisiasa katika Tanzania na khususan kwa upande wa Zanzibar. Tokea kuasisiwa kwake hadi leo , ikiwa sasa ni zaidi ya nusu karne, Muungano na khasakhasa muundo wake, umebaki kuwa ndio ajenda kuu ya kitaifa katika siasa za Zanzibar. Muungano unaendelea kudumu ukiwa unalindwa kwa nguvu kubwa za kisiasa na kidola pengine kuliko jambo lolote katika uwanja wa kisiasa hapa Tanzania.

Katika umri wake, Muungano huu umepitia misukosuko mingi. Mwaka 1984 katika kuunusuru Muungano ilibidi Serikali nzima ya Zanzibar iondolewe madarakani. Aliondolewa Rais Aboud Jumbe Mwinyi, Waziri Kiongozi wake Ramadhan Haji Faki na Baraza lake lote la Mawaziri. Mwanasheria Mkuu wa Serikali hiyo aliyekuwa Raia wa Ghana,Bashir Swanzy alitimuliwa nchini na kurejeshwa kwao. Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi , Marehemu Wolfgang Dourado alikamatwa Zanzibar na kupelekwa magereza ya Tanzania Bara kwa kile kilichodaiwa ukosoaji wake wa Muungano. Orodha ya waliopata majeraha katika harakati za kuudumisha Muungano ni refu.

Hivi karibuni tumeshuhudia kufutwa kazi kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na kufukuzwa uanachama kwa aliyekuwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mansour Yussuf Himid na hivyo kupoteza nafasi zake zote za kisiasa kutokana na misimamo yao ya kutokukubaliana na mambo mbalimbali katika Muungano wakati wa Mchakato wa Katiba Mpya. Viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Uamsho takriban 20 ambao wamekamatwa Zanzibar na kushtakiwa katika Mahkama za Tanzania Bara na kuzuiliwa katika magereza ya Tanzania Bara kwa makosa ya ugaidi , nao kabla ya kukamatwa kwao waliendesha harakati kubwa ambazo ziliungwa mkono na wafuasi wengi zilizolenga kuukosoa Muungano. Hata yale maeneo ambayo tunajivunia kuwa ni mafanikio ya Muungano , kama kukua kwa biashara baina ya pande mbili hizi, nako kila uchao tunasoma ripoti za vikwazo katika uendeshaji wake; mathalan vilio vya kila leo vya utozwaji kodi mara mbili kwa bidhaa zinazotokea Zanzibar na kuingia katika soko la Tanzania Bara. Biashara inaendelea kwa mtindo wa “kila kilema kina mwendo wake”

Yote hayo ni matokeo ya Muundo wa Muungano ambao kwa maumbile yake muundo huo milele hauwezi kujenga Muungano unaotoa haki, hadhi na fursa sawa baina ya washirika wa Muungano. Huu ni muundo wa Muungano wa Nchi mbili unaoendeshwa na Serikali mbili. Serikali moja, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebeba na kuyachanganya kwa pamoja mambo ya Tanzania Bara na yale mambo ya Muungano ambayo kimsingi ni mambo ya ushirika wa pamoja baina ya pande mbili za Muungano; na Serikali ya pili , Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imebakishiwa yale mambo ambayo si ya Muungano.

Muundo huu uliobuniwa kama muundo maalum wa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kutokea 1964 hadi 1965 kama ilivyoelezwa kwa ufasaha ndani ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ukafanywa kuwa Muundo wa Kudumu. Kila muda unavyokwenda, Muungano ulikuwa UNADUMISHWA kwa kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano , ilianza yakiwa mambo 11 na sasa yako 22 ;na hii maana yake ni kuyamega mamlaka ya Zanzibar katika eneo fulani, mathalan suala la fedha na sarafu (1965) na mafuta na gesi (1969) na kuyaingiza katika himaya ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo kimsingi ni Serikali ya Tanganyika iliyobaki na mambo yake yote na ikaongezewa mamlaka juu ya baadhi ya mambo ya Zanzibar na baada ya ongezeko hilo ikabadilishwa jina na kuitwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kiuhalisia Tanganyika ilijibakisha kama ilivyo na ikajiongezea mambo ya Zanzibar, haikumega chochote kutoka kwenye mamlaka yake na kuyapeleka kwengine. Aliyeuita muundo huu kuwa ni kiinimacho alikuwa amefikiri vyema. Muundo huu utadumisha misukosuko daima. Mfano chukua eneo la mapato na matumizi ndani ya muundo huu wa Serikali mbili. Baada ya miaka 50 ya Muungano huu eneo hili linafukuta mgogoro. Na utata uko wazi.

Na msingi wa utata huu ni muundo wenyewe wa Muungano. Jiulize uko wapi mfuko wa mapato na matumizi kwa ajili ya mambo ya Tanzania Bara yasiyohusu Muungano (ambayo hayo Zanzibar haihusiki asilani), na uko wapi mfuko wa mapato na matumizi wa mambo ya muungano (ambao katika mfuko huo Zanzibar inahusika kikamilifu na ingestahiki kuchangia na kupata gawio kama kuna bakaa).

Lakini ni wazi kwa muundo huu kamwe huwezi kutofautisha kuwa mapato haya yametokana na vyanzo vya Tanzania Bara au yametokana na vyanzo vya Muungano. Yote yamo mfuko mmoja tu. Pia huwezi kutofautisha kuwa matumizi haya ni kwa ajili ya shughuli za Tanzania Bara au kwa ajili ya shughuli za Muungano tu . Yote yanatumiwa kwa pamoja tu. Katika hali hii huwezi kutegemea utulivu kwa sababu uwazi na utambuzi wa maeneo na mipaka katika mapato na matumizi ni jambo nyeti katika ushirikiano wowote.

Tuchukue mfano mwengine, uchumi si jambo la Muungano, Zanzibar ina uchumi wake na Tanzania Bara ina uchumi wake na kiukweli hizi ni chumi mbili tofauti , mmoja ni uchumi mkubwa na mwengine ni uchumi mdogo LAKINI ni chumi shindani ( “competing economies” – na ushahidi wa hilo ni utozaji kodi mara mbili kwa bidhaa za Zanzibar) hasa katika maeneo ya biashara ya bidhaa, uwekezaji na utalii . Kwa upande wa Zanzibar uchumi huu ambao ndio unaopaswa kuiendeleza na kuihudumia Zanzibar NYENZO KUU za uchumi ,ambazo ni SERA ZA FEDHA (monetary policies) na SERA ZA KODI (fiscal policies) zimeondoshwa na kufanywa ni mambo ya muungano na hivyo Zanzibar haiwezi kusarifu uchumi wake bila misukosuko. Wakuu wa Benki Kuu na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Taasisi ambazo kimsingi zinasimamia uchumi wa Tanzania Bara hawawezi kuandaa sera zitazoendesha chumi mbili zenye mgongano wa kimaslahi na kwa vile huwezi kuokoa chungu cha mwenzako wakati chako kinawaka pia, Taasisi hizi zinatumika kuimarisha uchumi wa Tanzania Bara.

Katika jambo pekee lililo kwenye orodha ya mambo ya Muungano na Zanzibar ikaliwekea Wizara na Waziri basi ni suala la fedha lakini ni wazi Waziri huyu hana uwezo wowote katika maamuzi ya sera za fedha na kodi. Athari za kiuchumi zinazotokana na muundo huu zipo za kila aina. Hivi karibuni kuliibuka kashfa ya ESCROW ambayo kimsingi imetokana na mambo yasio na uhusiano wowote na mambo ya Muungano , ni mambo ya Tanzania Bara. Kufuatia mzozo huo wafadhili wakazuia misaada ya fedha na hii ikapelekea kuadimika kwa fedha za kigeni katika soko la ndani. Kwa vile mahitaji ya fedha za kigeni yalibaki palepale au yaliongezeka thamani ya fedha za kigeni ikapanda. Wakati wafadhili wanazuia misaada tunaambiwa thamani ya dola moja ilikuwa ni tshs 1635 hivi sasa thamani ya dola ni tshs 1900 ikiwa ni ongezeko la thamani kwa asilimia zaidi ya 15. Hii maana yake ni kuwa thamani ya sarafu ya Tanzania ambayo ni jambo la Muungano imeporomoka kwa asilimiaa 15 kutokana na matendo ya upande mmoja wa Muungano na kupelekea kuyumba kwa uchumi sio tu wa upande huo bali na wa upande wa Zanzibar kwa kosa lisiloihusu. Na katika mtanziko kama huu wa kiuchumi haijawahi Taasisi za kifedha na kiuchumi za Tanzania kuinusuru (bail out) Zanzibar.

Kwa hali ya mwenendo wa Muungano wetu ni sahihi alivyowahi kusema Prof Yash Ghai, mwanasheria mashuhuri wa mambo ya Katiba aliyeongoza Mchakato wa Katiba Mpya ya Kenya aliposema kuwa ” haishangazi kuwa Muungano huu unakumbwa na matatizo, bali kinachoshangaza ni kuwa umeweza kudumu”

(… the surprise is not that the Union has run into difficulties, but that it has survived at all )
(Issa G. Shivji,Tanzania The Legal Foundations of the Union, Second Expanded Edition, 2009, pg xviii, Foreword by Yash Ghai)

Tagsslider
Share: