Makala/Tahariri

Mkono wenye baraka

Ilikuwa ni baada ya sala ya Ijumaa katika msikiti wa Mazrui ndipo nilipobahatika siku hiyo kuugusa ‘mkono uliobarikiwa.’ Wakati tukitoka msikitini macho yangu yakabahatika kutua kwa mtu ambae tokea nifike Zanzibar nilikua na hamu nimuone na kumsabahi, japokua yeye hanijui, mtu huyo ni aliyekua mwanasheria wa Zanzibar, si mwengine ni Almuadham Othman Masoud.”

“Mbona una haraka ghafla mjomba, nisubiri..” kwani hata nilikua namsikia tena rafiki yangu tulioenda msikitini pamoja. “tutaonana pale mbele naenda kusalimia kwanza,” nikamwambia huku nikijisogeza karibu haraka haraka nimfikie Bwana Othman.

“Salaam alaykum habari za Ijumaa” Nikapeleka mkono. “Aah, waalaykum salam, vipi hali?” Haki ya Allah ni kama vile ananijua na kwa uso ulio na furaha akanirejeshea salamu, ndani ya nafsi yangu mawazo ya kila aina yanayomhusu mtu huyu niliempa mkono yalisongamana nikajikaza kurudisha bashasha, “Alhamdulillah hali salama tu. “Haya ishallah siku njema.” akatabasamu na tukaagana kwa Ahsante.

Baada ya hapo nikamtafuta swahiba wangu tulioenda msikitini hapo pamoja na aliponiona tu namna hatua zangu zinavyonepa na uso ulivyobadilika kwa furaha akaniuliza kwa utani, vipi mzee salama? Kumbe alikua akiniona pale tulipokua nikisabihiana na Othman. “Ah mambo leo ya Ijumaa ni mazuri, nimeugusa mkono wa mtetezi wangu, unajua ule ni mkono wa Baraka?” Rafiki yangu aliniangalia akajua leo itakua hadithi ni ya Mheshimiwa Othman tu hadi tufike nyumbani.

Na kweli, maana alichokua hakukiona na hata yeye Bwana Othman nilipogeuka tu na nikahisi hakuna mtu ananiangalia niliubusu mkono wangu wa kulia nikiashiria ndani ya moyo wangu kwamba nimeubusu mkono ule nilioukamata.Japokua kufanya jambo hilo si ajabu kwa mtu unaemuheshimu mbele yake, kiutamaduni wa Kizanzibari ukimfanyia mtu mbele yake utamtia haya kwani si jambo lililozoeleka. Waarabu wana utamaduni huo.

Wapi nianzie umuhimu wa kitendo alichokifanya shujaa huyu wa Zanzibar ambae alikua ndio sura ya SMZ kisheria kwenda bungeni na kuwakatalia SMT hadharani katiba yao pendekezwa yenye malengo ya kuimaliza Zanzibar kwa kuwapatia kura yake ya HAPANA. Looh! mbona walichanganyikiwa na kujua hakika kitumbua kimeingia mchanga, hakiliki tena!

Kauli ya Mheshimiwa huyu uzito wake katika historia ya kizazi kiliopo na kijacho ni pigo kwa wanaotaka kuifuta Zanzibar, hata katiba ya CCM ipite basi historia imeshaandikwa kwa wino mzito usiofutika kwamba mwanasheria mkuu wa Zanzibar alikataa.

Mtu huyu bila kujali maslahi yake binafsi wala usalama wake aliamua kusema yale ambayo watani wake umemtuma kusema bila ya woga wala kujali kama atakosa madaraka na maslahi mapana ya fedha ambayo wale wauza nchi hupata, tena sio pesa ya kununua njugu ni “fedha chafu” wanavyosema wenyewe, alichotakiwa yeye ni kuwa miongoni mwa wamwaga wino wa uchuuzi wa Zanzibar achukue donge lake, yeye akawaambia mkono huu utamwaga wino wa utetezi wa Wazanzibari tu.

“Yule sio mtu wa kawaida unajua” Niliendelea kwa furaha kuzungumza na swahiba wangu, “watu wa aina hii hapa kwetu ni wachache na hutumwa na Allah kwa kazi maalum.” “Ni kweli.” Alikubaliana nami swahiba wangu akijua kwamba hadithi leo haitoisha.

Na kweli maana tulipofika tu nyumbani nilisogeza laptop yangu kujikumbusha Zaidi mtu huyu, moja kwa moja nilienda hapa:

Hapo nilimuona zaidi mtu huyu ni nani na anaongozwa na misingi gani. Wakati nikiendelea kuzungumza na moyo wangu kitendo kile cha kujipenyeza penyeza hadi kumfikia niukamate mkono wa mtu huyu alieiokoa Zanzibar na aibu ya kuambiwa hata mwanasheria wake kakubali kuuza nchi, fikra zikanijia, “pengine na yeye alijiuliza suala huyu jamaa ni nani?” Basi kama anasoma mzalendo.net pengine huenda akakumbuka siku hiyo kwa furaha niliokuwa nayo lengo langu lilikuwa ni hilo, kuushika mkono wenye Baraka na kukuombea dua katika serikali yetu ijayo urudishwe na wadhifa ulio bora zaidi kuitumikia nchi yetu. Allah akubariki waliokuleta duniani kwani inasemwa “ Kwa matunda yake mutawaelewa wao.” By their fruits ye shall know them.
Ahsante Muheshimiwa Othaman,Zanzibar inakupenda.

Tagsslider
Share: