Makala/Tahariri

Mlango wa Tatu: Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Mmoja wa maofisa mcheshi wa polisi wa Kiingereza alipokuwa anaondoka Zanzibar nilikwenda kumuaga na nikamshika mkono na kumuambiya “Kwaheri Ukoloni!” Aliupokeya mkono wangu na kuniambiya “Kwaheri Uhuru”! —Marehemu Suleiman Behlani, alokuwa ofisa wa polisi (CID) Zanzibar

Waingereza na Siasa ya Kuikataliya Uhuru Zanzibar

Utawala wa Kikoloni wa Kiingereza ulikuwa na sera maalum juu ya Zanzibar ambayo waliita sera au mkakati wa kuikataliya Zanzibar (strategic denial) isije ikachukuliwa na nchi yenye uadui na Muingereza. Uingereza hakuitaka Zanzibar kwa kuwa ilikuwa muhimu kiuchumi au kibiashara. Kilichoaminiwa wakati ule ni kuwa Zanzibar ni mlango wa asili wa kuingiliya bara la Afrika na mwenye kuitawala basi amekuwa na uwezo wa kukitawala kinachoingiya na kutoka Afrika ya Mashariki na Kati.

Siasa ya Kiingereza juu ya Zanzibar ya karibuni ambayo ipo kutokeya mwezi wa Mei 1957 ni “haja ya kuvikataliya visiwa hivi visiingiye ndani ya mikono ya dola adui” na kwa mintarafu ya umuhimu wa kistratijia wa eneo lote la Afrika ya Mashariki.1 Ingelikuwa Zanzibar haikusimama kama ni Dola kwenye kizingiti cha Afrika Mashariki na Kati, Waingereza na wafuasi wake wasingejali kuhusu umuhimu wake. Visiwa vya Zanzibar vimetakiwa viwe kama visiwa vya Ukerewe na Nabuyondo ambavyo havina sifa ya kuwa ni dola.

Siasa ya Muingereza juu ya Zanzibar ilirithiwa na Tanganyika baada ya kupata uhuru wake mwaka 1961. William Edgett Smith ni mwanahabari na mwandishi wa jarida la Times la Kimarekani kwa muda wa miaka 35. Alizifuatiliya habari za hayati Mwalimu Nyerere kwa karibu na ameandika kuwa “marafiki wa Julius Nyerere wanakumbuka kuwa kwa muda mrefu alikuwa ana wasiwasi juu ya ukaribu wa Zanzibar na bara ya Tanganyika” na miaka michache kabla Nyerere alisema kuwa “Kama ningeliweza kukiburuta kisiwa kile nikakitupa katikakati ya Bahari ya Hindi, basi ningefanya hivyo.”2

Katika hafla ya chakula cha usiku iliyofanywa Dar es Salaam, mwaka mmoja au miwili kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere alisema kuwa anafikiriya kuwa tatizo kubwa litakaloikabili Tanganyika katika miaka ya baadaye itakuwa Zanzibar. “Hapana, sifanyi utani” alisema Mwalimu. “Ufalme wa kigeni, na watoto wenye kucheza na siasa. [Zanzibar] iko wazi kushawishika kutoka nje. Nakhofiya itakuja kutuumisha kichwa sana.”3 Kwa kurudia, mkutano wa tarehe 27 Februari 1963, ambao alihudhuria Makamo wa Rais Rashid Kawawa, chini ya mwaka mmoja kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwalimu Nyerere aliulizwa na Commonwealth Secretary Sir N. Pritchard kama Zanzibar itaachiwa kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki. Nyerere alijibu:

…ndiyo na itakuwa bora ikiwa Zanzibar itafungwa na mapema ndani ya Afrika Mashariki. Kinyume chake kuna hatari ya Zanzibar kugeuka Cuba na kuipa Afrika Mashariki tatizo lake la kwanza la kimataifa. Peke yao, Wazanzibari hawatojaribu kufanya kitu chochote dhidi ya Tanganyika lakini wanaweza wakawaleta marafiki zao ambao watawafanya wawe wakorofi. Zanzibar ilikuwa ni kituo cha kwanza cha ubeberu Afrika Mashariki. Uingereza iliuhifadhi utawala huu [wa Zanzibar] na ni jambo la kimantiki kuwa baada ya Uingereza kuondolewa Tanganyika Waafrika wa Zanzibar huenda wakaungowa Usultani.4

Kuitaja Cuba ilikuwa ni kumshituwa Sir N. Pritchard kwa kumtajiya Ukoministi lakini ni wazi alichokikusudiya Nyerere si Ukoministi bali ni uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu ambao akipenda sana kuwavunja maadui zake kwa kuwaita “Masultani” wakati “Sultan” ni neno la Kiarabu lenye maana ya nguvu au mamlaka.

Kutokeya tarehe 1 Disemba 1961, siku nane kabla ya Tanganyika kupata uhuru, tayari Balozi wa Kiingereza wa Zanzibar kwa niaba, alikwishapendekeza kwa The Secretary of State for the Colonies kuwa Zanzibar ni ndogo mno kuwa ni nchi ingawa aliupendekeza mfumo wa Shirikisho ambao ungelikubalika Zanzibar. Hapo tayari siasa ya kuinyima Zanzibar uhuru wake ili isianguke ndani ya mikono ya nchi adui bado inafanya kazi.

Anaandika Balozi:

[Zanzibar] ni ndogo sana na haina umuhimu (uhusiano wake na shirikisho utakuwa sawa na kitongoji kimoja cha Kiiengereza kwa Uingereza (England) nzima), haitowezekana sauti yake kusikika katika mabaraza ya Bunge la Shirikisho; na ikiwa shirikisho ni la kubana, na lenye nguvu kubwa ukilifananisha na nchi zilizoshirikiyana, hapana shaka [Zanzibar] itaonewa na washiriki wengine ndani ya shirikisho na itapoteza utambulisho wake. Wakati sehemu ya jamii ya kutoka “bara” iliyopo hapa hawatojali sana ikiwa hili litafanyika, hakuna shaka kuwa Wazanzibari wa kweli, ambao ndiwo walio wengi, wataupinga mfumo huo, hata kama utawaleteya faida za kiuchumi. Kuulinda utambulisho wa kitaifa na uhuru wa kitaifa ni mambo ambayo yanatizamwa kwa hamasa na si kwa mantiki, na wanayatabiri kuwa ni mambo yenye umuhimu sana kwao. Aina ya shirikisho lenye kutowa nafasi, lenye nguvu za Serikali ya Shirikisho zilizobanwa kwenye maeneo maalumu ya kiutendaji, na nguvu zilizobakiya zikabakishwa kwenye serikali za nchi [za shirikisho], ndilo aina ya shirikisho litakalowavutiwa walio wengi Zanzibar. Kunako shirikisho la aina hiyo kila eneo la nchi linaweza kujiwekeya serikali yake ya kitaifa, na huku likinufaika na faida za nguvu na ulinzi ambao unaweza kupatikana kwa kushirikiyana na mataifa makubwa, yenye utajiri na watu wengi zaidi.5

Hapana shaka yoyote shirikisho la aina hiyo lingelitegemeya kuwapo chini ya udhamini na ulinzi wa Muingereza au wa Tanganyika ili kulinda isitokee Zanzibar kuingiya ndani ya mikono na makucha ya nchi “adui” au ya “kibeberu.”

Hapana shaka pia Nyerere akifahamu vizuri kuwa Oman ndiyo iliyoung’owa ukoloni wa Kireno Afrika Mashariki baada ya kuushinda huko Oman na khasa ukatili waliouonyesha Wareno kwa wenyeji wa miji ya Qalhat na Quriyat na Hormuz. Anaandika Profesa E. Harper Johnson:

Wenyeji waliokandamizwa walihisi hawawezi kustahamili zaidi dhiki na udhalimu waliogubikwa nao na wakaamua kutafuta kujikomboa. Kulifikia lengo hili waliupeleka ujumbe wa siri Oman. Walipofika walitoa malalamiko yao kwa Imam juu ya unyama na udhalimu wa Kireno, na mabaya yote yaliyofanywa dhidi yao. Zaidi ya wananchi mia mbili walikatwa vichwa au kuuliwa kwa panga kwa jina la Mungu. Wareno waliwaingiliya kwenye nyumba zao, na kuwafukuza wenyewe na kuwanajisi wanawake wao. Wale waliokwenda kuomba msaada kabla walihukumiwa kifo.6

Oman ilikuwa ni dola ya kwanza ya Mashariki kuishinda dola kubwa ya kibeberu kutoka Magharibi. Ilifanikiwa kuwaondowa Wareno kutoka Mutrah baada ya Sultan bin Saif Al-Ya’rubi (1649–1668) kupewa taarifa muhimu na Muhindi aliyekuwa na Wareno lakini akiiunga mkono kadhia ya Waomani na “Baada ya Wareno kufukuzwa kutoka fukwe za Oman…walilipiza kisasi kwa kuwaadhibu Waswahili na Waarabu wa Kiomani wa Mombasa na sehemu nyengine za Afrika Mashariki kwa ukali mkubwa zaidi.”7

Dola ya Zanzibar ilikuwa imetanda Afrika Mashariki na Kati kabla ya kuingiya wakoloni wa Kizungu ambao walianza kunyanganyiana mpaka mwisho wake vikabakiya visiwa vya Unguja na Pemba. Pamoja na kuwa ilipofikiya Agosti 1961 iliamuliwa kuwa tarehe ya uhuru wa Zanzibar “isingeliwezekana kuwa kabla sana au baada sana ya [uhuru] wa Kenya na sababu kubwa ya hili ni mara Kenya itakapopata uhuru, uwezo wa ufalme wa Kiingereza wa kuilinda Zanzibar kwa nguvu za kijeshi utapunguwa kwa kiasi kikubwa sana.”8

Dhihaka ya kihistoria ni Zanzibar pamoja na historia ya Waarabu wa Kiomani waliyopigana na kuwashinda wakoloni wa Kireno kupotoshwa kutoka mtazamo wa kiukombozi na kuangaliwa kipropaganda kuwa ilikuwa ni kiti cha mwanzo cha ubeberu Afrika Mashariki. Nyerere alikuwa ameshatiya niya ya kuindowa Dola ya Zanzibar kwa kukitumiya kisingiziyo cha ubeberu na aliiyona fursa ya kuweza kufanya hivyo baada ya Tanganyika kupata uhuru na kwa kukosekana kwa uwezo wa Kiingereza wa kuilinda Zanzibar kwa nguvu za kijeshi kutoka Kenya. Na serikali ya ZNP-ZPPP ilimpa Nyerere fursa aliyokuwa akiisubiri ilipotaradadi baina ya kuipeleka Zanzibar kwenye njia ya siasa kali ya kizalendo ya Kiarabu ya Raisi Gamal Abdel Nasser, na kuwaomba Waingereza wabaki kuisaidiya Zanzibar kiulinzi baada ya uhuru wa Zanzibar wa tarehe 10 Disemba 1963. Matokeo yake ulinzi wa dola na uhuru wa Zanzibar ukapoteya.9

Tarehe 21 Novemba 1963, Balozi wa Kiingereza wa Zanzibar, Sir George Mooring alipeleka barua kwa Secretary of State for the Colonies yenye kusema:

Waziri Mkuu amenijiya na ombi la kutaka kutimiza Mkataba wa Kijeshi baina ya Zanzibar na Serikali ya Malkiya (H.M.G.). Serikali ya Zanzibar makhsusi inaomba kuwa Serikali ya Malkiya iombwe ikubali kutowa nguvu kwa ajili ya usalama wa ndani na wanataka kujuwa kama vikosi vya Kiingereza vitaweza kupatikana vyenye nguvu za kijeshi. Makadiriyo ya Serikali ya Zanzibar ni kuwa kutakuwa na tishio la usalama wakati na mara tu baada ya Siku ya Uhuru. Nitashukuru kama nitaelekezwa nitowe majibu gani, na kama Gavana wa Kenya ambaye namnukuu ujumbe huu atashauri kama Serikali ya Kenya itakuwa na upinzani wowote wa kuvitumiya vikosi vya Kiingereza viliyoko Kenya kwa ajili ya kuweka usalama Zanzibar ikiwa itahitajikana.10

Ujumbe wa hapo juu wa Sir George Mooring ulipelekwa kwa Secretary of State for the Colonies tarehe 21 Novemba 1963 saa kumi na mbili na nusu za magharibi. Siku hiyohiyo na wakati huohuo Sir George Mooring alimpelekeya Secretary of the Colonies ujumbe mwengine ambao uliongezewa hadhi ya kuwa ni siri na wa binafsi (secret and personal):

Suala hili [la mkataba wa ulinzi] limejadiliwa na Mawaziri pamoja na mimi mara nyingi hivi karibuni lakini kwa njia zisofahamika vizuri. Mpaka tarehe 20 Novemba sikuweza kupata makusudiyo au maelekezo ya niya kutoka kwao. Kwa hakika kama ripoti zinavyoeleza walikuwa wanalizungumza suala hili na Misri na nilifikiriya kuwa suala hili [la ulinzi] limeshamalizika. Upinzani kutoka A.S.P. kuwa na mahusiano na Misri pamoja na matatizo ya kujaribu kutafuta msaada kutoka kwengine kokote kule mbali na Uingereza ndiko kulikosababisha mabadiliko ya mtizamo wao wa hivi karibuni. Unafahamu kutokana na ripoti zetu za usalama za mwezi wa Oktoba kuwa ziko sababu za kufikiri kuwa kipindi cha mara tu baada ya uhuru kinaweza kikawa kigumu. Hali ya kijuujuu inaonekana kuwa imekuwa afadhali lakini chama cha U.M.M.A. bado ni tishio kubwa. Hili si tishio la kupuuzwa kwa sababu ingawa ni chama kidogo na hakina uwakilishi katika Baraza la Kitaifa, lakini kimekusanya takriban [wanasiasa] wote wenye misimamo mikali kutoka pande zote na kina uwezo wa kujenga mstari wa umoja wa wanafunzi, wafanyakazi na A.S.P. dhidi ya Serikali.11

Haistaajabishi kuwa majibu aliyoyapokea Balozi wa Kiingereza, Sir George Mooring, kutoka Secretary of State for the Colonies, tarehe 9 Disemba 1963 hayakuwa ya kuridhisha:

Kwa hisani yako muarifu Waziri Mkuu kuwa Serikali ya Kiingereza imeyapitiya kwa kina maombi yake ya kutaka mkataba wa kijeshi baina ya Uingereza na Zanzibar. Iwapo patatokeya hatari ya kuvamiwa Zanzibar kutoka nje, hapana shaka kutakuwa na mashauriyano ya hapo kwa hapo baina ya Serikali ya Uingereza na ya Zanzibar kama ni wanachama pamoja wa Commonwealth na msaada gani utahitajika kutolewa.12

Tangu hapo na kutokeya tarehe 2 Novemba 1963, Sayyid Jamshid bin Abdullah, Sultan wa Zanzibar alikuwa ameshamuandikiya barua fupi Sir George Mooring iliyoiyondoleya dhamana Serikali ya Kiingereza juu ya Zanzibar:

Mheshimiwa,

Nina hishma ya kuuhusisha Mkataba baina ya Sultan wa Zanzibar na Kanali Euan-Smith, Wakala wa Mtukufu Malkiya na Konseli-Mkuu, kuiweka Zanzibar chini ya himaya ya Kiingereza, ambao ulitiwa sahihi tarehe 14 Juni, 1890.

Ili Zanzibar iweze kuelekeya kunako uhuru tarehe 10 Disemba, 1963, hapana budi Mkataba ufutwe juu ya mamlaka yangu ambayo hayamo kwenye Mkataba nilioutiya sahihi tarehe 8 Oktoba, 1963, ambao unahusiyana na Himaya ya Kenya.

Kwa hiyo nina hishma ya kupendekeza kuwa mkataba wa 1890 uamuwe, kwa kuhusiyana na mamlaka yangu yasiyojumuuisha Himaya ya Kenya, kuanziya tarehe 10 Disemba, 1963.

Jamshid bin Abdullah bin Khalifa

Sultan wa Zanzibar13

Baada ya siku kumi, tarehe 12 Novemba 1963 yakaja majibu ya Balozi wa Kiingereza wa Zanzibar, Sir George Mooring:

Mtukufu,

Nina hishma ya kukuhusisha na barua yako Mtukufu ya tarehe 2 Novemba, 1963, kuhusu Mkataba wenye kuiweka Zanzibar chini ya himaya ya Kiingereza, ambao ulitiwa sahihi Zanzibar tarehe 14 Juni, 1890.

Nimeamrishwa na Mtukufu Malkiya kuwa makubaliyano Yake na Wewe Mtukufu kuhusu Mkataba utashika kuanziya tarehe 10 Disemba, 1963, wenye kuhusiyana na mamlaka Yako Mtukufu ambayo hayamo ndani ya Himaya ya Kenya.

A. G. R. Mooring

Balozi14

Kwa kifupi, siku Zanzibar ilipopata uhuru wake ilikuwa haina ulinzi wa aina yoyote na ilipovamiwa kutoka nje Waingereza walikataa kuipa msaada Dola ya Zanzibar na hawakutaka tena kujihusisha nayo na badala yake mkubwa wa usalama, Forsyth-Thompson akashauri imezwe na Tanganyika. Askari wa jeshi la polisi kutoka Bara na baadhi ya maofisa wa polisi wa Kiingereza walikuwa wameshatakiwa kuondoka nchini. Kulikuwa hakuna mkataba wa kijeshi na Uingereza wala Misri. Mshauri wa mambo ya Afrika wa Gamal Abdel Nasser, Mohammed Faiq alimwambia mwandishi wa kitabu hichi kuwa hapajakuwa na mkataba wowote wa kijeshi baina ya Zanzibar na Misri na suala hilo lisingeliwezekana.15

Kwa upande wa usalama, Mervyn Vice Smithyman, aliyekuwa Katibu Mkuu katika ofisi ya Waziri Mkuu wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Sheikh Mohammed Shamte, anakiri kuwa mbali ya serikali kuwa macho tangu ghasia za Zanzibar za Juni 1961, hakukuwa na “onyo la wazi la kabla [kuhusu mapinduzi], isipokuwa ripoti ya Abeid KARUME kwa Alan Bott wa kitengo cha Usalama” na kuwa kulikuwa na “operesheni kamili iliopangwa na iliowahusisha mamia ya watu pamoja na wale waliokuwa nje ya Zanzibar.”16

Kwa mujibu wa Smithyman, usalama wa Zanzibar wakati wa uhuru ulikuwa na miundo minne: Baraza la Usalama, Kamati ya Usalama ambayo ilikuwa chini ya uwenyekiti wa Smithyman, na Kamati ya Usalama kwa ajili ya visiwa vya Unguja na Pemba, na Kamati ya Uchunguzi ambayo Smithyman pia alikuwa ni memba. Muundo muhimu wa Usalama ulikuwa ni Baraza la Usalama ambalo memba wake walikuwa “Waziri Mkuu, Mawaziri wakubwa mmoja au wawili, Kamishna wa Polisi, Makatibu Wakuu wawili wenye kuhusika, na Tawi Maalum la Usalama (Special Branch).”17

Mfumo wa Usalama ambao sera zake zilikuwa zinashughulikiwa na Baraza la Usalama “ziliandikwa upya na Bwana Forsyth-Thompson. Bw. Forsyth-Thompson kwa miaka mingi sana alikuwa ni Mtumishi wa ngazi za juu wa Serikali ambaye alikuwa amehusika na masuala ya Amani na Usalama katika Ofisi ya Balozi wa Kiingereza. Siku kumi kabla ya Uhuru, Baraza la Mawaziri lilipanguliwa na mimi [Smithyman] nikampangia [Forsyth-Thompson] awekwe kwenye kazi maalum ya kuhakikisha kwamba kazi za Usalama zinawekwa katika hali ya juu ya kuweza kufanya kazi vizuri kabisa kabla ya kuondoka kwake katika mwezi wa Februari [1964].”18

Kwa mujibu wa Forsyth-Thompson “hakuna ushahidi wa kuwepo kwa mkono wa nje katika mapinduzi bali mapinduzi yalianzishwa na kikundi cha Afro-Shirazi Youth League chenye msimamo mkali. Si Umma Party wala si viongozi wa ASP wenye siasa wastani waliojuwa chochote kuhusu mapinduzi. Inawezekana Saleh Saadalla alikuwa anajuwa.” Ameelezea kabla kuwa Alkhamisi tarehe 9 Januari 1964, wanamapinduzi “walisikia ya kuwa Serikali inateremsha silaha kutoka Algeria…Hadithi ya silaha za Algeria zilivuma sana katika wiki baada ya Mapinduzi: kwa hakika ilikuwa ni upuuzi mtupu.”19

Bwana Forsyth-Thompson kwenye ile ripoti yake juu ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyoiandika Nairobi tarehe 10 Februari 1964 anatowa ushauri kuwa “Ufumbuzi bora wa Zanzibar wa mustakbali ni kumezwa (absorbed) na Tanganyika; ima kumezwa moja kwa moja, au bora, kuwekwa ndani ya mfumo wa Shirikisho wa karibu. Haiwezi [Zanzibar] kumiliki jeshi, wala shughuli za Mambo ya Nje, wala Serikali kamili yenye Mawaziri… kwa kuondolewa Mfalme na kuwekwa sawa kwa wenye kuutetea Uarabu, kikwazo kikubwa kimeondoka.”20

Kwa upande wa jeshi la Polisi, Kamishna wa Polisi wa Kiingereza, Bwana Sullivan hakukubaliyana na Waziri Mkuu Bwana Mohammed Shamte kuhusu kutolewa watu wa Bara kutoka jeshi la polisi la Zanzibar. Kwenye ripoti Kamishna Sullivan alimuandikiya Waziri Mkuu na kupeleka nakala kwa Balozi wa Kiingereza kwamba ikiwa polisi wa kutoka bara waliokuwa wanafanya kazi polisi Zanzibar watatolewa:

…uti wa mgongo mzima wa nguvu za polisi utapotea…idadi ya polisi 270 na katika hao, 90 ni Watanganyika, wengi waliobakia ni Wakenya, na kidogo kutoka Rhodesia, Zululand, Swaziland, Nyasaland na Uganda…Baadae nikamuonesha barua yangu John Harrison wa Usalama na alifadhaishwa vipi Serikali yoyote ile itaweza kufanya kitendo kama hicho. Alikwenda [Harrison] kumuona Waziri Mkuu.21

Kamishna Sullivan anamaliziya kwa kusema “Yote haya yalikuwa na athari mbaya juu ya jeshi la polisi, na ingawa hazikuonekana dalili za kukosa utiifu…haikufikiriwa kuwa hali ilioko haikuwapa askari moyo wa kupigana au kutoa taarifa za Usalama kwa Serikali, ambayo askari walihisi kuwa haiwaamini.”22

Kuna tafauti kubwa katika ripoti ya Kamishna Sullivan kuhusu upangaji na uendesheaji wa Mapinduzi ya Zanzibar na ripoti ya Bwana Forsyth-Thompson ambaye kama tulivyoona huko nyuma alihusika na kurekebisha mambo ya usalama kabla ya kuondoka kwake mwezi wa Februari 1964.

Ripoti ya Kamishna Sullivan ilianza na safari za vijana wa Kizanzibari waliopelekwa nchi za Kikoministi na inamalizikia kwa maneno yafuatayo:

Mpaka hapa inaonekana kwamba operesheni iliendeshwa kwa mujibu wa mipango mizuri na watu ambao walikuwa wameidhibiti hali na wenye ujuzi wa kutosha wa mikakati ya kivita ambayo ilikuja kufuatiliwa katika matukio ya baadae kwa karibu na kile nilichokisoma kuhusu mbinu za kuipindua serikali ndani ya kitabu cha Babu chenye kumbukumbu zake za mambo ya kila siku (diary).23

Makomred na Kivuli cha Mapinduzi

Ripoti za awali za Waingereza zilikuwa kimya kuhusu mkono wa Tanganyika ndani ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hata baada ya kutambuwa, Uingereza haikuweza kubadilisha mawazo yake juu ya Zanzibar na waliendeleya kutizama maslahi yao na kumuunga mkono Mwalimu Nyerere katika jitihada zake mpya za kuimeza Zanzibar. Kisingiziyo kipya kilikuwa ni Ukoministi hata kama alifahamu kuwa Makomred walikuwa ni “kikundi cha watu wachache [Waarabu?] na kibanzi cha wachache.”24

Kwenye mahojiano mbele ya televisheni aliyofanyiwa marehemu Mzee Karume, John Okello, na Abdulrahman Babu, na mwandishi wa habari wa Kiingereza, Babu alitamka wazi kuwa yeye na kikundi chake hawakusaidiwa na nchi za Kikoministi katika kufanikisha Mapinduzi na kuwa Balozi wa Cuba aliyekuwepo Dar es Salaam alikuwa hajui kitu kuhusu Mapinduzi kama alivyokuwa yeye hakujuwa chochote kuhusu mipango ya Mapinduzi ya Zanzibar. Okello alisema kuwa alisaidiwa na “Mungu wa Waafrika” kuyafanikisha Mapinduzi hayo Zanzibar na Babu aliyarudia kikasuku maneno ya Okello kwa kusema “tulisaidiwa na Mungu wa Waafrika.”

Mara tu baada ya kutokea Mapinduzi ya Zanzibar, “Jorge Serguera Balozi wa Cuba nchini Algeria aliruka kwa ndege kwenda Zanzibar kuitathmini hali ilivyokuwa. Baada ya siku chache aliruka akenda Moscow kuonana na Fidel Castro ambaye alikuwa anautembelea Muungano wa Kisovieti kuanzia Januari 13 mpaka 23. Castro alifadhaishwa kabisa na habari za Mapinduzi [ya Zanzibar]. ‘Fidel aliniuliza,’ anakumbuka Serguera, ‘Ni kweli [viongozi wa Mapinduzi Zanzibar] wanazungumza Kispaniola?’ Nikasema: ‘Ni kweli Fidel.’ Halafu akauliza: ‘Ni kweli wanasema “Patria o muerte. Venceremos!” ’ Nikasema: ‘ni kweli Fidel.’ Halafu akauliza: ‘Ni kweli tuliwapa mafunzo [ya kijeshi]?’ Nikasema: ‘Ni kweli, Fidel.’ Akasema: ‘Nilifikiri ni propaganda ya Kimarekani!’ ”25

Ingawa Babu na Makomred walikuwa na mipango yao ambayo ikiongozwa na fikra za kisoshalisti na zaidi za Mao Tse-Tung, isingeliwezekana kuungwa mkono na Cuba kwa wakati ule kufanya mapinduzi Zanzibar wakati Cuba ilikuwa na uhusiano mzuri na Urusi na ilikuwa haisikilizani na Uchina. Pia, ilikuwa ni kwa faida ya wahusika khasa wa Mapinduzi ya Zanzibar kuwatupiya mpira Makomred au Kamati ya Watu 14 kwa sababu kwa kufanya hivyo walikuwa wanajipa himaya ya bure.

Waliokuwa hawakijuwi kiini cha Mapinduzi wakipita wakitamba kuwa wao ndio wao wanamapinduzi wenyewe! Na ndio maana mpaka hii leo hakuna maelezo kutoka kwa Komred yoyote aliye hai au aliyekufa yenye kuthibitisha mchango wao kabla ya Jumapili tarehe 12 Januari 1964. Walikubali kuyatumiya na kutumiliwa na Mapinduzi kama walivyokubali wengineo katika chama cha Afro-Shirazi wakati Babu alitambuwa kuwa:

Waingereza waliiendeleza hii sera ya kuigawa Afrika Mashariki na Kati kutoka Afrika ya Kaskazini kwa nguvu ambazo hazijapata kuonekana. Walifikia kupandikiza chuki za migongano ya kikabila baina ya “Waarabu” na “Waafrika” Sudan na Zanzibar, na kwengineko Afrika Mashariki.26

Mtizamo wa kisoshalisti ulimpa Babu na wafuasi wake mgando wa ajabu wa kiitikadi na kuwafanya wadharau hisia za uzalendo za uzawa na ukabila wa mrengo wa Mwalimu Nyerere na wanamapinduzi wenzake.

Ali Sultan Issa kwenye kitabu cha kumbukumbu za maisha yake ameandika kuwa “Kulikuwa hakuna shaka kuwa Zanzibar ilielekea kunako njia ya mgongano na majirani zake, na sisi tulikuwa tuko tayari kuutumilia mgongano huo wakati utakapowadia.”27 Juu ya kutambuwa kwa Babu kuwa Waingereza walikuwa na sera ya wagawe uwatawale, Ali Sultan na Babu wakaona wataweza kuutumilia mgongano/mwanya huo na kuipenyeza itikadi yao ya kisoshalisti kutoka China.

Kigogo kimoja cha CCM, jina nalihifadhi, ameyaita Mapinduzi ya Zanzibar kuwa yalikuwa ni ya bahati “lucky affair.” Zanzibar iliupiganiya uhuru wake na ikaupata lakini haikujuwa namna ya kuulinda kwa sababu iliidharau sumu ya fitina za utumwa na stratijiya ya kutojiwachiya Zanzibar kuingiya ndani ya mikono na makucha ya “maadui” wawili, Muingereza na Mwalimu Nyerere.

Tagsslider
Share: