Makala/TahaririMaoni

Msimshike ‘sharubu’ Jecha rudini kwa Lukuvi Kanisani

Hii ndiyo sura inayojitokeza katika yanayodaiwa kuwa mazungumzo yanayoendelea Zanzibar na mjadala mzima wa mkwamo wa kisiasa katika visiwa hivyo. Katika pande mbili zinazokinzana, kila mmoja anasema lake linalompendeza bila kujali hoja za mwingine wala bila kuweka maswali ya msingi na kuyatizama pamoja. Ukisikiliza aliyosema Maalim Seif Shariff Hamad na yale ya Rais Dr. Shein juu ya msimamo wa CCM, mtu unajiuliza, kwa muda wote huo, tunaambiwa vikao sita, nini kilichokuwa kinazungumzwa, iwapo hakuna hata moja wanaloongea lugha moja?

Yawezekana wapo Wazanzibari ambao bado wana tamaa kuwa ipo siku Maalim Seif Shariff Hamad atatangazwa na kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Hao ndio wanaamini pia kwamba, Mheshimiwa Rais JPM ‘anashughulika’ na ipo siku ‘atatumbua’ jipu la Jecha kisha Maalim atangazwe!!! Lakini pia wanatamaa kubwa kwamba hata kama ‘jipu la Jecha’ litamshinda Mheshimiwa JPM, basi ipo jumuiya ya Kimataifa ambayo itaingilia na kumpa ‘haki yake Maalim’.

Binafsi sitaki kurejea katika msemo wa wenyewe Wazanzibari , “Yaguju!” Lakini nataka tutafakari kwa pamoja. Ukitaka kuyaelewa haya ya Jecha Salum Jecha na kauli ya Rais Shein katika sherehe za mapinduzi Jumanne, rudi katika mzizi wa jambo. Rudi katika yale yaliyotokea kupindua Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi, kama yalivyokusanywa na Waziri Mkuu na Jaji Mstaafu, Mzee Joseph Sinde Warioba. Wazanzibar/Wananchi walitaka Muungano wa Serikali Tatu na mpaka leo ndio kilio chao. Lakini Muswada ule ulitupiliwa kwa mbali, ukaja mjadala mpya kabisa kiasi cha kushutumiwa Tume ya Warioba na kuonekana kama ‘wasaliti’ fulani hivi.

Labda tujiulize, lile la Katiba lina tofauti gani na haya ya Jecha ya Uchaguzi Mkuu? Mapendekezo yaliyosomwa na Mzee Warioba Bungeni, ni ya Serikali kwa sababu Tume ilikuwa ya Rais na mapendekezo yao waliyakabidhi serikalini ndio yakapelekwa Bungeni.

Leo Rais Shein anatamba kuwa yeye ni Rais halali kwa mujibu wa Katiba. Na anaongeza kusema kuwa kufutwa uchaguzi ilikuwa kwa mujibu wa sheria na hivyo hata kurejewa uchaguzi ni kwa mujibu wa sheria. Watu wa CUF na wengine wenye kufuatilia mambo haya kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Zanzibar, wanasema hapana. Hapa utaona kuwa ni yale yale ya wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba walivyokuwa wakitetea na kusema kuwa walikuwa wamewasilisha maoni ya wananchi, kujali masilahi ya nchi na mustakbali mwema wa muungano. Waliokuja kuyapindua nao walidai kuwa wanatetea maoni, matakwa na masilahi ya wananchi.

Mtu pekee aliyekuja kuwa mkweli na kufumbua fumbo la Katiba ya UKAWA na Mapinduzi ya CCM, ni Mheshimiwa William Lukuvi. Pengine kwa kuona kuwa Maaskofu, Mapadiri na waumini wenzake hawatalielewa fumbo lile na hivyo kudandia Bogi la kutaka serikali tatu, ilibidi awe muwazi.

Alisema hofu ni Uislamu. Muungano wa Serikali Tatu, utaifanya Zanzibar kuwa huru zaidi na hivyo ni hatari kwa ‘Waislamu’ kuchukua nchi na kuleta hatari ya ugaidi mpaka Bara. Hilo akalirudia aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta alipokuwa akiongea na Watanzania wanaoishi Uingereza alipotakiwa kueleza kwa nini walipindua ‘Katiba ya Wananchi’. Pamoja na maelezo yake mengi ya kuzunguka, lakini mwisho akawataka Watanzania wale wajiulize, je, wangetaka kuona Zanzibar inayotawaliwa na Sheikh mwenye madevu na kilemba? Hawaoni hatari yake?
Huu ndio msingi wa ‘mapinduzi’ ya Jecha katika uchaguzi, akaufutilia kwa mbali. Mengine ni porojo, ndio maana yanachukua sura ya mdahalo wa viziwi.

Labda kama alivyofanya Mheshimiwa Lukuvi, tulifafanue hili. CUF ni UKAWA. UKAWA ndio wanataka Muungano wa Serikali Tatu, kuwapa nchi, ni kutafuta ‘Shari’ na ‘hatari’ aliyoizungumzia Mheshimiwa William Lukuvi. Kwa hiyo, hoja inayosimama hapa ni ya Dr. Shein. Kwamba lazima uchaguzi urudiwe na kuhakikisha kuwa CCM inatapa ushindi wa kishindo. Mantiki yake ni kuwa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa Tanzania inaondokana na hofu aliyozungumzia Lukuvi Kanisani.

Nimesikia kauli ya CCM wakiomba radhi juu ya lile bango la kibaguzi lililoingia uwanjani siku ile mbele ya Rais Magufuli, Rais Shein na Marais wastaafu. Lakini nini kosa la watu wale? Kile kilichoandikwa katika bango lile, kinatofauti gani na aliyosema Samwel Sitta? Hivi maneno ya bango lile, tuseme ndiyo mazito kuliko yale aliyosema Mheshimiwa William Lukuvi Kanisani na kisha akayakariri ndani ya Bunge, tena kwa kujiamini!

Rais Shein na Jecha, wana mamlaka na nguvu gani ya kuja na jambo kubwa kama la kufuta uchaguzi na kung’ang’ania urudiwe kama hakuna maelekezo kutoka CCM Dodoma (Dar es Salaam) na Serikali ya Muungano! Tukijiuliza swali hilo, sasa tutizame vile vikao vya Maalim Seif na JK na kisha Mheshimiwa JPM, tulitarajia vije na ufumbuzi gani?

Leo mjadala ni ‘Maalim kupewa haki yake’, atapewa vipi iwapo yale ya Waheshimiwa sana William na Samwel hatuyaoni na kuyasemea kama Wazanzibari? Mbona Bara hatusikii wakisema kuwa ikishika CHADEMA atarudi Mjerumani na siasa zake za ‘ki-Hitler’ au kusimika sera za akina Angela Dorothea Merkel za Christian Democratic Union (CDU)? Kwa nini hofu iwe ni kurudi Mwarabu/Hizbu, ‘Sheikh’ mwenye midevu na kilemba?

Kama hayo hatuyaoni, basi tusubiri Jumuiya ya Kimataifa na wenye MCC wampiganie Maalim haki yake ya kutangazwa! Pengine ifike mahali tutumie akili japo kidogo tu tujiulize, watu walioipiga Afghanistan, wakaivamia na kuiharibu Iraq, kisha wakaisambaratisha Libya na sasa wapo Syria, watasilikiza kilio cha wanaotaka ‘Maalim’ atangazwe au watajali zaidi yale ya William Lukuvi aliyetoa kauli ya kulihami Kanisa na hatari ya ‘Katiba ya CUF/UKAWA’ inayotaka Muungano wa Serikali Tatu?

Hao wenye MCC wana mengi wanayataka katika madini yetu, mafuta na gesi, watahangaika na ya ‘kumpa haki yake Maalim’ waache mikakati yao na walio madarakani kupata mradi wao?

Suala hapa, sio Dr. Shein kuwepo Ikulu au kumpisha Maalim. Tatizo la Zanzibar ni kubwa zaidi ya hapo. Na maadhali hawataki kuliona, litaendelea kuwatafuna kama nchi na kama jamii.

Jiulize tu, hii hali iliyopo Zanzibar hivi sasa kiuchumi, kijamii na kila hali, na mustakbali wake utakavyokuwa kama siasa zikiendelea katika mkondo wake huu huu, wale waliokuwa wamebeba bango la sera za akina Samwel Sitta za “Sheikh mwenye madevu” pale uwanja wa Amani katika sherehe za Mapinduzi, wananufaika vipi?

Share: