Makala/Tahariri

Mtama alioumwaga Nape Mtama, na utabiri wa Nyerere

APR 13, 2017 AHMED RAJAB

JUMAMOSI iliyopita, Nape Nnauye, mbunge wa Mtama na waziri wa zamani wa habari, aliwahutubia wana CCM wa jimbo lake la Mtama, mkoani Lindi. Alisema maneno mazito bila ya kuyatafuna wala kuwa na kigugumizi.

Nape aliitoa hotuba yake kama wiki mbili baada ya Rais John Pombe Magufuli kumpokonya wizara aliyokuwa akiiongoza kwa zaidi ya mwaka mmoja. Siku moja kabla ya kufukuzwa uwaziri, Nape alikabidhiwa ripoti ya tume aliyoiunda kuhusu uvamizi wa ofisi na studio za kampuni ya utangazaji ya Clouds Media Group.

Kwa mujibu wa ushahidi wa picha za CCTV, uvamizi huo ulifanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akisaidiwa na watu waliokuwa na silaha. Baada ya kufukuzwa uwaziri, Nape akakumbwa na ile kadhia ya hoteli aliyokuwa amepanga azungumze na waandishi wa habari kuamrishwa kumkatalia. Alipojaribu kuzungumza na waandishi uwanjani karibu na hoteli walimiminwa vijana kujaribu kumzuia. Mmojawao alimtishia kwa kumtolea bastola katika jaribio hilo.

Nape aliuandaa mkutano wake wa Mtama akiwa na lengo la kueleza yote yaliyomfika siku hiyo.

Alipokuwa akitoa hotuba yake alionekana kuwa ni mtu mwenye kujiamini na mwenye kuyaamini aliyokuwa akiyasema. Ni dhahiri kwamba alikuwa akijijenga upya katika jamii. Akitaka ulimwengu umuone kuwa yeye ni mtu wa watu.

Na si mtu wao tu, lakini zaidi hivyo kuwa yeye pia ni mtu wa haki, mwenye kuitetea haki, asiye na mambo ya fitina na mwenye kusema kweli. Chambilecho mwenyewe: “Mimi ni mtoto wa Kimakonde na nimefundishwa kusema kweli.”

Kinachoshangaza — au pengine si cha kushangaza kwa kuzingatia siasa za chama chake — ni kwamba hakuwa akisema kweli kila alipostahiki kusema kweli. Hakika ya mambo ni kwamba Nape alistahiki kusema kweli sio leo, sio mwaka jana na hata sio mwaka juzi. Lakini angalau angelianzia huo mwaka juzi.

Heshima yake ingezidi kupanda na angezidi kuaminika lau angelianza kusema kweli baada ya kufanywa uharamia mkubwa wa kisiasa Oktoba 2015 wa kuipora demokrasia kwa kuufuta uchaguzi wa urais wa Zanzibar na wa Baraza la Wawakilishi. Uharamia huo ulikuwa pia kichekesho cha kisiasa kilichoiharibia Tanzania jina lake mbele ya macho ya ulimwengu.

Chama kinachotawala Tanzania pamoja na serikali zake zote mbili zilisema uongo mwingi kuuunga mkono uharamia huo na kwenda kinyume na haki. Wakati wote huo, Nape hakuonekana akisimama upande wa haki.

Hakuna anayekataa, na hata mwenyewe kama kweli ni mkweli hatokataa, kwamba katika safari yake ya kisiasa iliyomfikisha hapa alipo kuna nyakati ambapo hakusema kweli au aliibana kweli isitoke. Hayo ni miongoni mwa makosa yake ya kisiasa ambayo mahasimu zake hawakuyasahau na hawachoki kuyataja.

Muhimu ni kwamba tunapompima mtu, na hususan mwanasiasa, tuwe tunampima kwa kuyaangalia mazingira yanayomzunguka kwa sasa. Si kwamba tuyasahau makosa aliyokwishayafanya lakini tuyaenzi yale mema ambayo sasa ameamua kujitwika.

Jumamosi iliyopita, Nape alisimama upande wa haki kwa kuwatetea Watanzania waliotekwa na waliopotea. Alikuwa kiongozi wa mwanzo wa upande wa CCM aliyesimama kuwatetea. Kwa kufanya hivyo, aliwapiku marais wastaafu na hata maaskofu wakuu na mamufti waliokataa kufungua midomo yao kuulaani ubabe ulioingia mjini siku hizi pamoja na huo mtindo mbaya wa kuwateka na kuwapoteza wakosoaji wa serikali.

Miongoni mwa aliowataja Nape ni Ben Saanane, msaidizi wa mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya wa Hip Hop Roma Mkatoliki (jina halisi Ibrahim Mussa). Hatimaye Roma alipatikana siku hiyohiyo ya Jumamosi akiwa pamoja na wenzake watatu waliokuwa wamepotea tangu Jumatano iliyopita.

Inasemekana kwamba walipopatikana Roma na hao wenzake watatu wote walisema walikuwa na maumivu na walikuwa na alama za kupigwa.

Nayaandika makala haya kabla ya Jumatatu siku aliyoahidi Roma kuwa atayaeleza hadharani yaliyomkuta alipotekwa. Kabla ya kuibuka Roma na wenzake, Nape alimuomba Rais Magufuli aunde tume maalum ya kuchunguza visa hivyo vya kutekwa na kupotea kwa wanaoonekana kuwa ni wakosoaji wa serikali.

Pendekezo hilo la Nape ni muhimu kwa sababu tumeona jinsi visa kama hivyo vinavyoweza kuikumba nchi na kuifikisha pabaya. Nimezihesabu nchi zipatazo 30 duniani ambazo zimeshuhudia vitendo hivyo vya watu kutekwa na kupotea. Nne kati ya hizo ni za Kiafrika — Algeria, Equatorial Guinea, Morocco na Zanzibar wakati wa awamu ya mwanzo ya Serikali ya Mapinduzi.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu mtu husemekana kuwa amefanywa atoweke kwa nguvu pale anapotekwa nyara au anapofungwa kwa siri na dola au na chama cha siasa au na mtu wa tatu kwa amri au msaada wa dola au chama cha siasa.

Wanaomteka hukataa kusema mtu huyo yuko wapi au majaaliwa yake ni yepi. Lengo linakuwa kumfanya mtu huyo asiweze kupata hifadhi ya sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Waraka wa Sheria ya Kimataifa wa Roma uliounda Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, na ulioanza kutumika Julai 1, 2002, kitendo cha kumteka mtu na kumfanya atoweke ni kitendo cha uhalifu wa sheria. Ni kitendo cha jinai dhidi ya wanadamu.

Aghalabu mtu anapopotea asijulikane alipo huwa ameuliwa. Mtu huwa ametekwa, amewekwa kizuizini kinyume cha sheria na aghalabu huteswa, huuliwa, na maiti yake huzikwa au hutupwa pasipojulikana. Vitendo kama hivi vimefanyika kwa wingi hasa katika nchi kadhaa za Amerika ya Kusini katika miongo ya 1970 hadi 1990.

Nape alifanya vyema kushauri paundwe tume ya kuchunguza vitendo vya kupotea watu ambavyo yeye amesema vinafanywa nchini na vikundi vya kihuni. Alitoa ushauri huo akitambua kwamba kupotea kwa wakosoaji wa serikali, si mambo yaliyo mageni Tanzania, hasa Zanzibar.

Angeonesha uungwana wake angelivikemea pia vikundi ambavyo mara kwa mara tunasikia kuwa vinawashambulia wanaodhaniwa kuwa ni wapinzani huko Zanzibar. Vikundi hivyo vinajulikana. Vina majina ya kutishatisha kama “Mazombi”, “Janjaweed”, “Ubaya Ubaya”, “Mbwa wa Mwitu” na “Hali gani, vipi?”

Wenye kuviratibu na kuviongoza vikundi hivyo nao pia wanajulikana. Nape angezidi kuonekana kuwa ni mpigania haki angeshauri kuwa tume hiyo ya Rais pia ifanye uchunguzi kuhusu mashambulizi yaliyofanywa na vikundi hivyo tangu 2015.

Tena asingesita hapo lakini angeshauri paundwe tume nyingine maalum ya uchunguzi wa Wazanzibari waliopotea katika miaka ya 1960 na ambao hadi sasa hawajulikani wako wapi. Orodha yao ni refu na ina watu wa itikadi tofauti za kisiasa wakiwa pamoja na Abdalla Kassim Hanga, Abdulaziz Ali Twala, Saleh Saadalla, Othman Sharif, Amour Zahor, Said Dahoma “Kombanyongo”, Muhammed Salim “Jinja”, Mdungi Ussi na Juma Maringo (Jimmy Ringo).

Tumewataja wachache tu lakini wako wengi na familia zao mpaka leo hawajaambiwa na serikali nini kilichowafika watu wao. Hawajui kama wako hai au wamekufa na kama wamekufa walikufa vipi. Wala hawajui watu hao walipoteaje. Wanachojuwa ni kwamba walitiwa nguvuni na serikali.

Nape ni mtoto wa CCM. Ni kada wa muda mrefu aliyelelewa na akaleleka ndani ya chama hicho, chama ambacho marehemu mzee wake, Moses Nnauye, alikuwa mmoja wa vigogo wake. Anazijua mbinu na hila zote zinazotumiwa na chama chake. Na ameonya kwamba pasipochukuliwa hatua na matukio kama hayo ya watu kutekwa na kupotea yakiendelea basi CCM itajikuta pagumu ufikapo uchaguzi mkuu wa 2020.

Alisema amekaa miaka 16 ndani ya CCM na anajuwa kilichokuwa kinaendelea. Sisi nasi tusiokuwa ndani ya CCM hata nusu dakika nadhani pia tunafahamu alichokusudia kusema.

Nusura amwage mtama Jumamosi iliyopita na ayataje ya ndani ya CCM asiyostahili kuyataja hadharani lakini ghafla alijirudi.

Hata hivyo, aliyoyasema yanatosha kumfanya mdadisi aanze kuwaza mengi. Kwanza, alipiga vijembe na wakati huohuo akionya kuwa asiyeweza kuvumilia kupigwa vijembe “ende akalime nyanya.”

Pili, alimsuta na kumshambulia Mwenyekiti wa chama chake kwa kugusia kazi kubwa aliyomfanyia hata akachaguliwa Rais, akisahau kwamba hiyo ilikuwa ni kazi yake akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM. Tatu, amedokeza kwamba hatokiacha mkono chama chake lakini atayapigania ndani ya chama yale anayoyaamini.

Kinachodhihirika kwa yote hayo ni kuwa ndani ya CCM, hali ni hamkani si shuwari. Ni wazi kwamba kuna mpasuko ndani ya ngazi zake za juu. Kuna miongoni mwao wenye kuona kwamba mambo nchini, kwa jumla, na hata ndani ya CCM yenyewe, yanaendeshwa msegemnege na kwamba wakati umefika wa kugawana mbao.

Inawezekana kwamba Nape amepanga kuzicheza karata zake bila ya kujali kitamfika nini, potelea mbali afukuzwe chamani. Haiwezekani kuwa ana ujasiri huu alionao akiwa peke yake. Lazima ana wenzake. Nao ni pamoja na baadhi ya wale walioumizwa hivi karibuni na hatua ya mwenyekiti wao ya kukipanga upya chama chao.

Huenda Nape akawa anawatomeza kusudi wenye nguvu ndani ya chama ili wamfukuze. Likitokea hilo labda ataweza kuutimiza utabiri wa Nyerere wa kuzuka upinzani ndani ya CCM utaokigawa pande mbili chama kicho kikongwe kiasi cha kulifanya pande moja limeguke na kusababisha mabadiliko mengine katika mchakato mzima wa kuleta demokrasia halisi Tanzania.

Tusubiri tuone.

Share: