Makala/Tahariri

Must read : Viongozi na dhamana walizopewa – kisa cha Sayyidna Omar Bin Khattab

Na Salma Alghaithiy, Zanzibar

Kabla ya yote ningependa nitoe kisa kimoja ambacho ni kizuri maudhui yake yanafanana na makala hii ambayo nataka kuielezea baadae, kuhusiana na kadhia ya viongozi wanavyotekeleza majukumu na kujisahau kwamba wao wana jukumu kubwa na dhima mbele ya Allah lakini pia mbele ya wanaowaongoza.

Kisa hicho ni kati ya kiongozi na wanaoongozwa ambacho kilitokea miaka kadhaa nyakati za masahaba ambapo wakati wa enzi za Masahaba wa Bwana Mtume Muhammad (Radhi za Allah ziwe juu yake) wakati wa utawala Sayyidna Omar Bin Khattab (Radhi za Allah ziwe juu yake) ambaye alikuwa ni kiongozi wa umma wa wakati ule mwenyewe alikuwa na kawaida ya kutembea katika Mji wake nyakati za usiku na kujua hali za raia wake.

Katika kutembea kwake ndipo akakutana na kisa hiki ambacho ningependa ukisome vizuri wewe msomaji wa gazeti hili ili ukifahamu na kisha utapima namna gani viongozi wetu tulionao hivi sasa.

Sayyidna Omar alisikia sauti ya Mwanamke akisoma mashairi ya kusikitika kuwa yupo peke yake katika kitanda hana mtu wa kumliwaza na kumtimizia haki yake ya matamanio ambapo alisema lau kama hamwogopi Mwenyeenzi Mungu basi angetafuta Mwanamme amkidhie haja yake hiyo kwa usiku ule.

Sayyid na Omar aliposikia maneno hayo mazito kwa raia wake akashtushwa sana na kuamrisha siku ya pili apelekwe kwake kwa huyo Mwanamke ili kujua khasa ni kwa nini akawa anasoma mashairi yale.

Alipokuja na kuulizwa sababu ya mashairi yake yule Mwanamke akasema mumewe amekwenda katika vita vya jihadi muda mrefu na yeye ni binaadamu ana hisia kama mtu mwengine, na ndipo hapo Sayyid na Omar akajiona ana makosa makubwa na dhima kama kiongozi wa umma na akajiuliza kwa nini hajafikiria jambo hilo mapema.

Baadae Sayyid na Omar akatafakari akaona ili pate uhakika wa jambo hilo akamfuata mwanawe Sayyidat Hafsa Bint Omar ambaye alikuwa ni Mke wa Bwana Mtume Muhammada (Radhi za Allah ziwe juu yake) na kumuuliza ni jee Mwanamke anaweza kustahamili muda gani pindi akiwa mumewe hayupo?

Kwa hakika Bibi Hafsa (Radhi za Allah ziwe juu yake) akajibu kwamba Mwanamke anaweza kuvumilia na kustahamili hisia na matamanio yake miezi minne tu na zaidi ya hapo hawezi tena na inakuwa ni mtihani mzito kwake.

Kwa hikima na busara zake Sayyidna Omar akatoa amri kwa wanajeshi wote ambao wamekwenda vitani na wameacha wake zao huku majumbani ambao wamekaa zaidi ya miezi minne basi warudi na wabadilishwe wengine yaani waende vitani kwa zamu kila ikifika miezi minne waende wengine wale warudi majumbani mwao.

Lengo ilikuwa ni kuwarejesha wale wanajeshi waweze kukaa na wake zao majumbani na kuondosha ile dhima ya wanawake kulalamika kama ambavyo yule mwanamke alivokuwa akilalamikia hali yake upweke aliyokuwa nayo wakati mume wake akiwa vitani.

Ndio hapo tena Sayyidna Omar Bi Khattab akaanzisha utaratibu wa kuwekwa Daftari maalumu la kusajili kila aliyetimiza miezi 4 arudishwe nyumbani kutoka vitani na kubadilishwa waende wengine kutokana na hali ya kuwafikiria wanawake katika kuwatimizia haja zao za kimaumbile.

Hivyo ndivyo ilivyotokea wakati wa utawala wa kiongozi Sayyidna Omar Bin Khattab ambaye katika utawala wake alikuwa anahakikisha watu wake hawapati tabu na akijitahidi kuonesha uongozi wake wenye uadilifu kwa anaowaongoza bila ya kumuonea mtu bila ya kumdhulumu na kumhatarishia maisha yake kiafya na kisaikolojia.

Huo ni mfano mdogo wa Sayyidna Omar katika uongozi wake kwa umma aliokuwa akiuongoza, kwa hakika hilo ni dogo sana miongoni mwa aliokuwa akiyafanya kwa raia wake ikilinganishwa na yale mengine ambayo alikuwa akiyatenda na kuyatekeleza na kuyatafutia ufumbuzi kwa lengo la kuonesha kwamba yeye ni kiongozi mwema kwa raia zake na kiongozi muadilifu lakini kubwa alikuwa akiogopa dhima mbele ya Allah kwani uongozi ni utumishi na ni dhamana kubwa.

Kisa hiki kinaweza kutupa funzo kubwa hasa kwa viongozi wetu ambao amejisahau katika kutekeleza majukumu yao na kujua dhima ambayo wanayo mbele ya Allah na mbele ya familia za watu ambao wamesekwa ndani kwa takriban mwaka wa tatu sasa.

Tayari watu kadhaa wapo rumande wakiendelea kusota na kudhalilishwa wakiwa kwenye Magereza amma ya hapa Zanzibar na yale ya Segerea Dar es Salaam ambao baadhi yao wala hawana kesi za kujibu lakini ni uonevu tu na kurimbikiziwa kesi ambazo hazina kichwa wala miguu.

Ingawa mifano ipo mingi ya watawala kutumia nafasi zao na vyeo vyao kuwasweka ndani amma viongozi wa dini au viongozi wa kisiasa au watu wa kawaida huku kesi zao zikiwa zinapigwa tarehe tu bila ya kuhukumiwa.

Kwa mfano viongozi wa Taasisi za Kiislamu na wale wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Viongozi wake wamechukuliwa na kuwekwa ndani miaka kadhaa sasa bila ya kushughulikiwa kesi yao ikamalizika huku familia zao zikiachwa kwenye unyonge mkubwa.

Familia hizo bado zipo katika hali ngumu ya kimaisha hali mbaya ya kisaikolojia lakini katika hali ya kibinaadamu wapo njia panda kutokana na hali halisi ya kimaumbile jee ni nani ambaye anaweza kuvumilia katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kuwa mbali na mwenza wake ambaye ni halali yake katika ndoa? Sayyidna Omar Bin Khattab aliyaona hayo na kwa kuogopa jukumu akachukua haraka khatua za kuwarejesha watu ambao walikwenda katika kupigania dini ya Allah jee hawa ambao ni kesi za kubambikiziwa tu wenye mamlaka hawalioni hili?.

Ni kitu cha kuzingatia kama ambavyo Sayyidna Omar alivyoona na akafikiria vipi mtu atenganishwe na mke wake au familia yake katika muda wote huo tujiulize kwa mfano hao wenye kuwaweka wenziwao ndani wangejaribu kukaa kando na wake ao kwa muda wa mwaka mmoja atajisikiaje jee wataweza na kama hawawezi ni kwa nini waendelee kuwaweka wenziwao ndani kiasi hicho na miaka yote hiyo?

Bila ya shaka yoyote unapomchukua Mwanamme maana yake unajua hakika kwamba umeisambaratisha familia kwa kuwa tegemea la Mwanamke au familia ni Baba na Baba anapokosekana katika familia unaleta maumivu kwa Mke na watoto.

Lakini pia kuna baadhi yao wana watoto wa kuwalea ambao ni mayatima kuna wazee wao ambao huwa wanawatizama kwa hali na mali lakini hilo halijazingatiwa kama wana familia na watu wanaowategemea nyuma yao.

Ni nani ambaye anapenda kuona katika nyakati za sherehe na furaha baba yake hayupo au mume wake hayupo na wanabaki wakiwa na mawazo mengi na hisia mbaya nyoyoni mwao na kuwaumiza kisaikolojia zaidi.

Maumivu ya kukosekana Baba ndani ya nyumba ni makubwa na yasio kifani na mwenye kuumia sio mke peke yake lakini watoto wanapata maumivu makali wanapowaona watoto wenzao wakifurahi na familia zao nyakati za skukuu na siku za furaha lakini pia wanaumia wanapoambiwa mashuleni njoo na baba yako, fikiria mtoto anapata maumivu gani anaposikia sauti hiyo kutoka kwa mwalimu, na akizingatia Baba yake hajamuona zaidi ya miaka mitatu? Unamkumbusha nini mtoto bila ya shaka unamuumiza na kumtonesha kidonda ndani ya moyo wake.

Lakini pia fikiria pale anaposimama mwanamme kwenye kiriri cha mahakama na akaelezea kuwa yeye kafanyiwa vitendo vya kudhalilishwa kwa kuingiliwa kinyume cha maumbile, wewe kama mke ni maumivu ya kiasi gani unayoyapata kumsikia mume wako, au unamiaje unapomsikia mwanao anasema hivyo na jee mtoto anapata hisia gani anapomsikia baba yake akizungumza neno hilo? Hayo yote wenye mamlaka wanaona ni jambo dogo na halina ukweli, na ndio mana wakalipuuza na kutolipa uzito wowote.

Ni jambo kubwa ambalo linatakiwa kutafakariwa na kila mtu kwani hili sio la mtu mmoja ni jambo ambalo linaumiza kiafya na kisaikilojia.

Kila mmoja ni mchunga na ataulizwa juu ya alivyovichunga hilo ni la kulizingatia hasa kwa hawa viongozi wetu wa sasa ambao sio tu wanashindwa kuonesha kwamba dhamana walizopewa na umma ni dhamana kubwa ambazo ndani yake kuna hekima kubwa lakini hayo ni kwa wale wenye mazingatio.

Naam nimetoa kisa hicho ili tuweze kuona namna gani viongozi wetu wa sasa hivi wanavyoshindwa kuchukua mifano mizuri yenye hekima busara na uadilifu kama ambavyo viongozi wa umma wa kiislamu walivyokuwa wakitekeleza.

Licha ya kuwa na viongozi wengi wa kiislamu lakini matendo yao wanayoyafanya dhidi ya waislamu wenzao ni mabaya na bila ya shaka haya sio tu hayatoi taswira nzuri kwa uislamu wao lakini pia yanatahiri imani zao na za waumini wenziwao.

Vitendo hivyo havileti sura nzuri ya uongozi kwani kumdhulumu mtu hali ya kuwa unajua kama unamdhulumu ni jambo kubwa ambalo malipo yake ni mabaya mbele ya Allah.

Kesi hiyo wanatuhumiwa kwa ugaidi jambo ambalo viongozi wenyewe wanasema Tanzania hakuna ugaidi kama hivi juzi kiongozi mmoja alivyosikika na kuandikwa kwenye magazeti akisema kwamba ugaidi haujafika Tanzania, sasa suali la kujiuliza wale waliokamatwa kwa ugaidi wanawekewa nini magerezani?.

Watu wanawekwa ndani na kudhalilishwa huku viongozi wa serikali wakiwa kimya, mahakimu na waendesha mashtaka wakizidi kuminya haki za watu hao umma nao ukiwa umenyemazishwa, wanaharakati nao wamenyamaza kama kwamba hakuna kinachoendelea ndani ya magereza hayo.

Ni jambo la kusikitisha na kuumiza sana unapoona mtu anafanya vitendo vya kudhalilisha wengine na kisha mamlaka zote zikiwa zimefumba mdomo huku wengine wakibeza na kudharau matendo ambayo walitendewa mahabusu hao.

Wito wangu kwa waislamu wote nchini kumuogopa Mwenyeenzi Mungu na kuondosha khofu ndani ya mioyo yao na waelekeze macho kwa familia zaidi ya 50 ambazo zinapata tabu huku majumbani kutokana na waume zao kuzuwiwa kwenye magereza ya Segerea huko Dae es Salaam huku kesi yao ikiwa inapingiwa siku bila ya kumalizika.

Familia hizo zaidi ya 50 za Masheikh zinapata tabu zinapaswa kusaidiwa zinapaswa kutizamwa zinapaswa kuhurumiwa kwani hazina makosa yoyote waliyoyafanya lakini zinaumizwa kwa makusudi kwa kuwa waume zao wapo ndani kwa kesi ambayo ushahidi wake zaidi ya miaka mitatu haujapatikana.

Hakuna sababu tena ya kuendelea kukaa bila ya kuwaangalia wake na watoto ambao wanazidi kuumizwa kisaikolojia hali ya kuwa wapo watu wenye uwezo wa kuwasiadia kifedha nao wakaishi maisha ya kutimiziwa mahitaji yao.

Kwani kutoa fedha na kuwatimizia mahitaji yao wake hao na watoto sio kwamba utakuwa umeponesha majeraha walionayo lakini angalau umewasaidia kwa kiasi kidogo kwa wale ambao wanahangaika nayo wameyapata na yale ya kimwili na kisaikolojia tukubali kwamba ndio wameshaumizwa na jeraha hilo haliwezi tena kupona wala kuondoka.

Enyi viongozi wenye mamlaka, Muogopeni Mwenyeenzi Mungu na mkae mkukikumbuka kwamba dhamana mlizopewa ni za kupita na ipo siku mtaulizwa juu ya yale yote mliokuwa mkiyatenda dhidi ya binaadamu wenzenu wakati mna uwezo wa kuondosha dhulma lakini mkaziwacha zifanyike.

chanzo:zanzibaryetu

Tagsslider
Share: