Makala/Tahariri

Muungano una kasoro za kimfumo na kimsingi kabisa, sio changamoto!

Ningesema kama niko kwenye somo la physics basi neno momentum lingekuwa sahihi kabisa kuchapua mjadala unaondelea masiku ya hivi karibuni huko Dodoma dhidi ya kile kiitwacho hujuma za kiuchumi dhidi ya Zanzibar ukoloni mweusi wa Tanganyika.

Lakini kwa bahati mbaya hatuko skuli, niseme tuu natoa wito kwa wawakilishi walioko barazani kuendeleza mjadala huu wa muungano.Hii sukari nadhani ni kitumbuizo tuu.Naamini muungano huu una kasoro za kimsingi kabisa.

Ninachoweza kusema mifano ya aina ya hii kama sukari ni mingi, tujikumbushe na tujiridhishe kuwa wenzetu wana lengo na mawazo ya kikoloni dhidi yetu.Ni tofauti na ile dhana ya udugu ambayo huekwa mezani.Majibu anayotoa waziri mkuu ni ya ubabaishaji tena wa hali ya juu wa kuzima mjadala.Ukimsikiliza vizuri Mh.Majaliwa anasema ametoa vibali vya sukari vya mwaka huu na kuiweka Zanzibar katika mizani ya akili yake sio sehemu kabisa ya udugu hata ule wa mtoto wa kambu.

Kumekuwepo na masuala mingi ya mtindo wa kikoloni na kuiminya Zanzibar, mfano wale waendao Berlin Ujerumani kujitangaza utalii ni takriban kila mwaka suala hili la Zanzibar kujitangaza kiutalii basi Tanganyika huingilia na kuanza pirika za kikoloni.

Niendelee hapo hapo kulikuwa na suala la Drop, Zantel, leseni za mameli, kodi mara mbili bandarini n.k. Ifike wakati wawakilishi nao wajitutumue kwa kuwarudishia wananchi wenyewe aidha wanaridhishwa na mwenendo wa kubakia ndani ya muungano au la.

Tushukuru mabadiliko ya kumi ya katiba yanatupa uwezo wa kuitisha kura ya maoni.Hivyo ni sahihi kisheria wawakilishi kuwapatia nyenzo wananchi nao kutoa maoni yao.Tusipoteze muda kurekebisha kasoro za muungano, tokea awali haukuwa na malengo ya kiuchumi bali kinyume chake yaani kudhoofisha uchumi wetu.

Kumalizia niseme tuu muungano huu una kila aina ya viashiria vya kuifanya Zanzibar kuwa koloni.Sidhani kama kasoro zake zinastahiki kuitwa changamoto kama PM Majaliwa atakavyo tuamini. Hizi ni kasoro zenye mizizi ambayo yanakwenda hadi kwenye malengo ya muungano wenyewe.

Changamoto sio neno sahihi kuwakilisha matatizo ya muungano.Kuna matatizo ya kimfumo, ushahidi wa hili utagundua kila tume ya watalaam inatoa ushauri wa kubadili mfumo.Kitu chenye kasoro za kimfumo hakiwezi pewa neno changamoto au kero!

Share: