Makala/Tahariri

MWIZI WA ZANTEL, UKIMYA WA SERIKALI NA DHARAU ZA TCCRA

Na: Mwandishi Maalum

Kama kuna mtu duniani, ukitoa Mzanzibari, asiyejua maisha waishiyo wanyama msituni, basi amuombe Mungu amgeuze kuwa mnyama japo siku moja. Ataona. Na tena hivyo akiomba, aombe awe mnyama mfano wa Swala, Paa, punda milia na wanyama wengine walio wengi lakini dhaifu zaidi msituni.

Akishakuwa mnyama, mtu huyo, basi aende zake akaishi kwenye mbuga kubwa ya wanyama. Akishaishi huko awekewe walinzi wakali watakaoweza kumlinda asiliwe na wanyama wengine kama simba, chui na duma, ili akishajifunza haya maisha, arejeshwe kuwa mwanadamu, aje tena asimulie wengine.

Mzanzibari, ni mtu pekee ambaye ana uzoefu wa maisha yote mawili kwa wakati mmoja; maisha ya kuishi kama mtu na kuishi akiwa mnyama dhaifu ambaye wanyama wenye nguvu humuonea na kumuumiza kila uchao bila kupata shufaa ya msaada wowote. Si kwa wanyama wenziwe wadogo na dhaifu wala si kwa wanyama wakubwa wenye nguvu.
Mzanzibari mnyonge hana kauli wala hana haki. Ikitokezea akidhulumiwa, hana pa kulalamika wala hana wa kumsikiliza wala wa kumwambia lolote la msaada au ushauri. Si dola, si kiongozi wake wa jimbo wala sio nchi yake. Hapana aliye tayari kumsaidia wala kumtetea kwa lolote.

Mzanzibari wa leo licha ya kufanywa aamini kuwa yeye maisha yake yote atabaki mnyonge asiye kitu wala sauti, amini kwamba hana haki ya kupata huduma bora za afya, za elimu wala za msaada wa kisheria pale inapohitajika.

Kwa mfano, sote tunajua huduma zetu za afya ni za kuzimu kwa uoza na upofu. Lakini ukifika huko Hospitali kutaka huduma hizo hizo mbovu, muuguzi au daktari ana haki ya kukutukana matusi ya nguoni. Hakuna wa kumrudi. Muuguzi au daktari anaweza hata kukuua kwa makusudi akiamini hakuna pahala pa kumshitaki wala wa kumfanya lolote.
Mahakamani halikadhalika. Tumeona mara ngapi watoto wa viongozi na wengine hata wa masheha tu, wakipita na vyombo vya moto na kumgonga mpita njia mnyonge na kumuondosha duniani au kumuachia ulemavu wa kudumu. Mwisho wa siku, hakuna liwalo. Mtoto huyo wa mkubwa au wa sheha, hafikishwi mbele ya sheria na wala hakuna chochote kinachofanyika.
Wacha nisipoteze muda mwingi kwa kurudia rudia kukupa matukio ambayo si mageni tena masikioni mwako. Haya yote niyasemayo, tunayapata kila uchao. Na ndio kwa maana hii naandika makala hii kusema kuwa, nchi yetu haina tafauti na mbuga za wanyama au maisha ya msituni. Mkubwa humla mdogo na mdogo maisha huliwa tu na hana msaada wa kisheria wala wa kihaki za kimaumbile za kuishi.
Thamani ya mwananchi wa kawaida katika nchi hii ni ndogo kuliko ile ya kuku boi au mbuzi wa kafara. Kiongozi aliyechaguliwa na wananchi hao dhaifu, ili aje awatetee, ndiye huyo huyo ambaye hugeuka na kuwafanyia uharamia wale wale waliompa yeye ukubwa na utukufu. Kiongozi huyo mchaguliwa, badala ya kuwalipa waliomchagua hisani, huishia kuwalipa nuksani.
Tumeyaona ya Mv. Spice Islander, Skargit na mengineyo mengi. Kwetu sisi kufa mtu wa kawaida, raia, mchochole ni sawa na kufa kuku au bata mavi tu. Si chochote kwa viongozi wetu. Na vivyo hivyo ndivyo ilivyo inapokuja kwenye huduma kwa wananchi na huduma kwa wateja wa kawaida.

Tumelalamikia sana kuhusu suala la mchele mbovu wa ‘Mapembe’. Hakuna lililofanyika zaidi ya kuubadilisha jina na kuiita: ‘Super mapembe!’ Kusema uhakika mchele wa mapembe ni mchele mbovu na usiofaa kuliwa na mwanadamu. Lakini nani anajali?

Kuubadilisha jina mchele mbovu wa mapembe na kuuita ‘Super’ hakuufanyi uwe mzima na unaofaa kuliwa. Kufanya hivyo ni matokeo ya kejeli tu ya kuwabeza wananchi walio wengi wasiodiriki kula mchele mzima unaofaa. Na hili Serikali wala mamlaka ya viwango, wamelinyamazia kimya kwa sababu hawajali mustakabali wa maisha ya anayekula mapembe!.
Sasa nije kwenye mada. Shirika la ZANTEL ni moja kati ya mashirika makubwa ya simu hapa Zanzibar. Shirika hilo, lilipoanza kuja hapa visiwani ilijipatia umaarufu mkubwa kwa wananchi. Umaarufu ambao ulichanganyika na uzalendo wa hali ya juu. Kila Mzanzibari, alijivunia kutumia simu ya Zantel.
Hadi kufikia mwaka 2014, Zantel lilikuwa ndio shirika pekee lenye wateja wengi zaidi wa simu visiwani Zanzibar. Ongezeka hilo la wateja, lilikuja sio kwa ubora wa huduma watoazo Zantel, bali ni kwa sababu ya uzalendo tu. Uzalendo wa Wazanzibari wenye uchu wa kutaka utambulisho wao.
Pamoja na hayo ya uzalendo na ubovu wa huduma zao, awali huduma za Zantel hazikuwa mbaya sana ki hivyo. Lakini katika siku za hivi karibuni, maji yamezidi unga. Wizi wa mchana na huduma mbovu kupitiliza za mtandao na mafikio mabovu ya network ni mgogoro mtupu.

Hivi sasa Zantel limekuwa shirika linaloongoza kwa kuwaibia wateja wake kuliko shirika lolote la simu nchini. Tena linawaibia kwa mbinu ya wizi wa kimacho macho: Wizi wa mchana, kweupeee! Hawaoni haya wala kimeme. Ni wizi kwenda mbele tu.

Wakati malalamiko ya wateja yakizidi kupamba moto, Zantel ndio kwanza, imejitia pambani za masikio, Haisikii wala haijali kuwa wanaolalamika kuibiwa ni wateja wanyonge wasio na uwezo wowote zaidi ya kutumia kidogo walicho nacho kuwasiliana na wengine duniani kujipatia riziki. Zantel hilo hailijali. Imeshikilia wizi, wizi, wizi usiku na mchana.
Hivi sasa ukiweka shilingi mia kwenye simu yako ya Zantel, ukipitisha dakika moja au mbili utakutia haipo. Imeliwa. Usiku ukitia elfu mbili ukiamka haimo wala huoni huduma uliyopata.
Ukiwauliza Zantel huduma kwa wateja, hawana majibu zaidi ya maneno mengi yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Mwizi hana haya wala hakosi la kujitetea. Na hivyo ndivyo Zantel walivyo.
Licha ya wateja kulalamika, Zantel hawaonyeshi kama wanajali kwa sababu kadhaa. Moja ni kuwa wanaamini, na kwa hakika ndivyo ilivyo, kuwa hakuna mtu wala mamlaka ya kuwawajibisha: si Serikali wala sio TCCRA. Wote hao la moja: kusimamia maslahi yao binafsi na sio wananchi wanaotakiwa kuwasimamia.
Pili, Zantel ina uhakika kuwa Wazanzibari ni watu wapole mno. Au kwa lugha ya wenzetu wa kuumeni; Wazanzibari ni ‘Mdebwedo!’ au ‘Mayakhe’. Hawana ubavu wa kudai haki yao kwa nguvu kama vile kuandamana na hata kutishia kuihama Zantel moja kwa moja.

Kwa ukubwa wa dhuluma wanazofanyiwa wananchi wa Zanzibar na Zantel pekee, ingekuwa ni nchi ambazo haziongozwi kwa sheria za msituni, basi Zantel wangefilisiwa kwa kuwalipa fidia wananchi iliowaibia na kuwapa usumbufu kwa muda wote huu. Lakini wapi, Serikali haijali wala TCCRA haina habari. Wananchi wamebaki hawana la kufanya!
Sasa ikiwa Watumiaji wa Zantel wanaitegemea Serikali na TCCRA iwasaidie kwa kuingilia kati tatizo la wizi na huduma mbovu za Zantel, basi wanajidanganya. Hakuna litakalokuwa. Kikubwa kilichobaki kwa sasa, wananchi inabidi waamue moja kati ya mawili: kusuka au kunyoa.
Iwapo Wazanzibari wataamua kusuka, basi itawalazimu wazichukue simu zao zote wazitoe laini za Zantel wazitupe mashimoni au kwenye majalala ya taka. Ndani ya masaa ishirini na nne yajayo, katika visiwa vya Zanzibar hakutakuwa na mtu yeyote anayetumia simu ya Zantel. Ikiwa hakuna anayetumia simu hizo, Zantel watamuibia nani?
Ama Wazanzibari wakiamua kunyoa, basi sharti waandamane na kufika ofisi kuu za Zantel Amani na kule Msasani bara kudai haki yao. Wakifika huko wapige kambi kutwa kucha wakidai haki yao mpaka moja liwe. Wapate au wakose.

Rai hii ya kunyoa, kwa hakika si nzuri sana hata hivyo, kwani katika nchi ambayo mwananchi wa kawaida ni sawa na swala au punda milia wa dola, wananchi wataishia kuzingirwa na polisi na kuuwawa bure! Na rai hii inapofanya kasoro, namaanisha kuwa baina ya kusuka na kunyoa, kusuka huwa bora zaidi kuliko kunyoa.
Kwa hali ilipofikia sasa, kuna haja kwa watumiaji wa Zantel kuihama kampuni hii kwa mara moja na kuiacha ikihaha kutafuta wateja sehemu nyengine iwaibie. Wateja wenyewe labda nao watoke katika sayari za Mars na Venus na sio tena hapa duniani kama wataweza.
Tutakapofanya hivyo, tutakuwa tumeitia adabu Zantel na pia Serikali na TCCRA ambazo kwa pamoja zinashirikiana kutufanyia hujuma na dhuluma ili tuzidi kuwa mafukara na wahanga wa kafara za ulafi wao.

Ni ukweli usio na chenga chenga kuwa Zantel imeshindwa kutoa huduma bora nchini. Serikali nayo imeshindwa kututetea kwa hili. Na TCCRA pia imeshindwa kutekeleza wajibu wake dhidi ya Zantel hata baada ya kupokea malalamiko ya wateja. Wakadharau. Mwisho wa siku ni sisi tunaopata shida. Tufike mahala tuseme, ‘BASI, INATOSHA, TUMECHOSHWA NA ZANTEL!’

Tagsslider
Share: