historiaMakala/Tahariri

Nani alimuuwa Mzee Karume??

Nani alimuua Mzee Karume?

Na: Yericko Nyerere

John Gideon Okello alizaliwa 1937, katika Wilaya ya Lango nchini, Uganda na alifariki mwaka 1971 kijijini kwao Lango Uganda alikokwenda kutupwa na Julius Nyerere na Karume. Kifo chake kimeacha majonzi kwa wanamapinduzi, kwani licha yakuwa rais wa kwanza wa Zanzabar na Baba halisi wa Taifa la Zanzibar kwa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar lakini Waafro + Shiraz hawa wamemezeshwa uongo kuwa Karume ndie baba yao.

Okello kafa masikini hata msiba wake umehudhuriwa na ndugu tu bila heshima yoyote ya kiukombozi.

Capt Yusuf Hamud ndie aliyetekeleza mauaji hayo, lakini bado hoja inasimama kuwa,
Nani alimuua Karume?

Hapa kuna dhana nne.,

Wapo wanaosema ni chuki za askari mamluki wa Okello, hawa wanaungwa mkono na Julius Nyerere,

Na wapo wanaosema ni Julius Nyerere na Muungano wake, hawa wanaungwa mkono na mzee Aboud Jumbe Mwinyi aliyefungwa kizuizini pale Mjimwema Kigamboni.

Pia wapo wanaosema ni visasa vya ndugu aliowau Karume kipindi cha mpito tangu anyang’anye madaraka kwa Okello.
Hapo bado jibu la kitendawili hiki ni gumu, hasa ukitazama hoja za kila upande ni nzito na zinatetea kwa nguvu!

Na wapo wanaosema yalikuwa mapinduzi ya jeshi.

Hoja za Shivji ni nzito sana, hoja za Prof Othuman ni nzito pia, Hoja za Lissu ni nzito pia na hoja za Joseph Mihangwa ni nzito.

Joseph Mihangwa anasema wazi.

Kwa mujibu wa taarifa za Usalama wa Taifa Zanzibar, mipango ya “kupindua” Serikali ya Karume ilianza kusukwa tangu 1967 – 1972 ndani ya Zanzibar na Tanzania Bara, ambako nyumba ya Abdulrahman Babu ilikuwa kituo cha mikutano ya Wazanzibari ya kupanga Mapinduzi hayo.

Kama hivi ndivyo, Karume alikuwa na sababu tosha kumtaka Nyerere kumrejesha Babu Zanzibar “kuhojiwa”, Februari 1972.

Mkutano wa mwisho ulifanyika Aprili 2, 1972, ambapo ilikubaliwa Mapinduzi yatekelezwe Aprili 7, 1972, yakihusisha makundi mawili: kundi la Wazanzibari kutoka Bara, wengi wao wakiwa wanajeshi, na kundi la Wazanzibari ndani ya Zanzibar, likihusisha raia na wanajeshi wachache.

Pamoja na uamuzi huo, kikao kilitoa majukumu mazito kwa baadhi ya washiriki, ikiwa ni pamoja na Hamoud na Ahmada kupewa jukumu la kuiba silaha kutoka kambi ya kijeshi, Bavuai.

Ilikubaliwa kuwa, Babu na wafuasi wake kutoka Bara wasafiri kwa mtumbwi kwenda Zanzibar Aprili 6 kuamkia alfajiri ya Aprili 7, na kufikia eneo lililopo kati ya mitambo mikuu ya mawasiliano [Cable and Wireless] na Klabu Starehe.- Baada ya hapo, Babu abakie amejificha kwenye nyumba ya Hamoud Hamoud, iliyotizamana na Klabu Starehe eneo la Shangani, kusubiri saa ya mapambano kuwadia.

Kwa mujibu wa taarifa, Babu aliondoka Dar es Salaam kwa mtumbwi uliofungwa redio mbili za mawasiliano, jioni ya Aprili 6, safari iliyoelezwa kuwa ya “kuvua samaki”; wakati madhumuni halisi yalikuwa ni kuwafikisha Babu na wafuasi wake Visiwani usiku wa Aprili 6, kwa maandalizi kamili ya kupindua Serikali

Jioni hiyo, Aprili 6, Uongozi wa Jeshi uligundua upotevu wa silaha nyingi Kambini Bavuai.- Na ingawa uongozi ulikuwa bado haujamhusisha mtu yeyote, lakini Hamoud, Hamada na askari wengine walianza kufuatiliwa kwa siri.

Yaelekea kufikia hapo, Babu alijulishwa na kuonywa kwa njia ya redio akiwa baharini, juu ya kugunduliwa kwa mpango mzima wa Mapinduzi; akakatiza safari na kurejea haraka Dar es Salaam hima.- Haijulikani kama wafuasi wake walikuwa wamekwishafika Zanzibar au la; au kama nao walijulishwa na kurejea Dar es Salaam.

Lakini kuwapo Visiwani wanajeshi kama Kanali Mahfoudh- (Mkurugenzi wa Operesheni JWTZ, Dar es Salaam) na Luteni Hashil Seif (Kikosi cha Wanamaji, Ukonga, Dar es Salaam) saa ya kuuawa Karume, kunaonyesha baadhi yao tayari walikuwa Zanzibar kusubiri wenzao.

Saa 12.00 asubuhi, Aprili 7; Ali Khatibu Chwaya (raia) alikwenda kwa Ali Mshangama Issa (afisa wa tatu, meli M.V. Afrika, mkazi wa Zizi la Ng’ombe, Zanzibar), kumweleza juu ya kutowasili kwa kundi la Dar es Salaam.

Baadaye asubuhi hiyo, Ali Mshangama, Chwaya, Miraji Mpatani -(karani wa shirika moja, Zanzibar), Mohammed Abdullah Baramia (Mtunza Bohari, Idara ya Elimu), Ahmada na Hamoud, walikutana nyumbani kwa Hamoud na kuonyesha kukerwa na kusikitishwa kwa kutowasili kwa wapanga mapinduzi kutoka Dar es Salaam, hasa wakijua pia kwamba, silaha zilizoibwa bado zilikuwa nyumbani kwa Hamoud, na hatari ya kuwezakugunduliwa.

Ilipofika saa 6.00 adhuhuri siku hiyo, Mshangama, Hashil Seif, Amar Saad Salim, maarufu kama Kuku (afisa usafirishaji, Idara ya Siha, Zanzibar) na Chwaya, walikutana nyumbani kwa Amar Saad ambako Mshangama, Hashil Seif na Baramia walipendekeza mpango wa kupindua Serikali uahirishwe hadi watakapopata taarifa tofauti kutoka Dar es Salaam.

Kwa hiyo, saa 9.00 mchana siku hiyo, saa mbili tu kabla ya kuuawa kwa Karume, Baramia alikwenda nyumbani kwa Hamoud eneo la Shangani kuwasilisha pendekezo hilo.- Alimkuta Miraji Mpatani nje ya nyumba na kumweleza Baramia kwamba, pamoja na kundi la Dar es Salaam kutowasili, Ahmada na Hamoud walishikilia Mapinduzi yafanyike tu siku hiyo, kwa sababu Ahmada alikuwa anatafutwa na maafisa wa Jeshi.

Je, ni kwa sababu hii Luteni Hamoud, Kapteni Ahmada na Chwaya waliamua kufanya Mapinduzi, licha ya wenzaokutaka yaahirishwe?.

Kwa mujibu wa mkakati wa Mapinduzi uliofikiwa Aprili 2, 1972, Suleiman Mohamed Abdullah Sisi (mwanajeshi wa JWTZ, mkazi wa Ilala Flats, Dar es Salaam) alipangwa kuongoza utekaji wa kambi ya Jeshi, Mtoni, ambapo Kapteni Ahmada, alitakiwa kuteka kambi ya Jeshi, Bavuai, Makao Makuu ya Jeshi na Chuo cha Jeshi cha mafunzo ya Redio, vyote hivi viko eneo la Migombani.

Kituo cha Polisi cha Malindi kingeshambuliwa na kutekwa na kikundi chenye silaha kikiongozwa na Luteni Hamoud ambacho kingeweza kuteka magari yenye Redio za mawasiliano.

Askari Yusufu Ramadhan angeongoza kikundi cha maafisa wa Polisi walioingizwa kwenye mpango huo na kuteka Kituo cha Polisi cha Ziwani.

Amour Dughesh (mwanajeshi; Zanzibar), yeye angeteka Ikulu na kumkamata Karume, kisha kumpeleka Kituo cha Redio kumlazimisha atangaze kupinduliwa kwa Serikali yake.- Baada ya hapo, Kituo hicho kingeachwa chini ya udhibiti wa Badawi, Mpatani na Mohamed Said Mtendeni (mwandishi wa habari, gazeti la China, mkazi wa Vuga, Unguja).

Uwanja wa Ndege ungetekwa na kikosi cha wanajeshi na baada ya hapo kingeachwa chini ya udhibiti wa Ali Sultan Issa (meneja wa Shirika la Mafuta, Zanzibar).

Mpango huo ulilenga pia kuteka Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa ASP, ambayo yalikuwa pia Makao Makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar, ikiongozwa na Kanali Seif Bakari na kuwekwa chini ya udhibiti wa Mohamed Abdullah Baramia, Kapteni Khamis Abdullah Ameir, wa Makao Makuu ya Jeshi, Zanzibar; yeye alipangwa kuzuia mashambulizi kutoka nje kama Mapinduzi yangefanikiwa.

Mapinduzi au mauaji ya Kisiasa?

Mapinduzi ni kitendo cha kutaka kubadili sawia hali, serikali au mfumo fulani wa kijamii kwa matumizi ya nguvu, ikiwa ni pamoja na kuondoa mhimili wa mfumo huo.

Mapinduzi yanaweza kuwa kwa njia ya jeshi kama jeshi limetumika au ya kiraia kama raia walitumika, kama yalivyokuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Mauaji ya Karume hayawezi kuitwa mapinduzi ya kijeshi wala ya kiraia kwa sababu kifo chake hakikubadili mfumo wala muundo wa serikali.- Haya yanaweza kuitwa mauaji ya kisiasa yenye lengo la kuondoa chanzo au mhimili wa kero katika jamii bila kubadili serikali.

Mwanazuoni mahiri Barani Afrika, Profesa Ali Mazrui, anatafsiri mauaji ya kisiasa (political assassination) kuwa ni kitendo cha siri cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri kisiasa, kinachofanywa na wakala asiye wa serikali; kwa sababu za kisiasa au zisizofahamika.

Naye Profesa William Gutteridge wa Chuo Kikuu cha Aston, anasema mauaji ya kisiasa kuwa ni kitendo cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri katika jamii kwa sababu za kisiasa na kinajumuisha pia jaribio la mapinduzi lililoshindwa na watu wengi kuuawa katika kutekeleza kilichokusudiwa.

Kwa mantiki hii, mauaji ya Karume, kama yalivyokuwa mauaji ya Rais Anwar Sadat wa Misri, kwa kupigwa risasi wakati akiangalia gwaride la jeshi lake, yalikuwa na lengo la kuiondolea jamii kero bila umuhimu wa kubadili serikali.- Katika mauaji kama hayo, mlengwa huwa mmoja tu kama chanzo au mhimili wa kero.

Karume aliuawa kwa sababu ya utawala wa kimabavu, ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu kama tulivyoona hapo juu; wakati Sadat aliuawa kwa kuisaliti jamii ya Kimisri, kwa kusaini Mkataba wa suluhu kati ya Misri na Israeli uliojulikana kama Camp David ili kusitisha harakati za Waarabu dhidi ya Uzayuni wa Kiyahudi.

Sababu nyingine ilikuwa ni kukumbatia sera za kiuchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hatua iliyoathiri maisha ya Wamisri kiuchumi na matarajio ya kijamii ya Waislamu nchini humo na Jumuiya pana ya Kiarabu kwa ujumla.

Malengo ya mauaji ya Karume yanajidhihirisha kwa vielelezo kwa yale yaliyofuatia chini ya utawala wa mrithi wake, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, aliyechukua uongozi Aprili 11, 1972.

Baraza la Mapinduzi lililoketi Aprili 10 -11, 1972, pamoja na kumthibitisha Jumbe kuanzia Aprili 7, 1972 kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza hilo, pia lilipitisha azimio la kudumisha, kulinda, kutetea na kuendeleza fikra, malengo ya kimapinduzi na sera alizoacha Karume.

Hata hivyo, Wazanzibari wengi walitaka Kanali Seif Bakari amrithi Karume kwa kuwa alikuwa mtu wa karibu zaidi kwa Karume kuliko Jumbe, kwamba ndiye pekee miongoni mwa Wazanzibari ambaye angeweza kuendeleza fikra za mwasisi huyo wa Taifa la Zanzibar.

Nyerere aliingilia kati akiwa na hoja kwamba, kwa kuwa Rais Karume aliuawa na mwanajeshi, kumteua Bakari ambaye alikuwa mwanajeshi kumrithi kiongozi wa kiraia, kungetafsiriwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyoweka mwanajeshi madarakani.- Hoja ya Nyerere ikashinda.

Kwa kuanzia, Jumbe alifuta Amri ya Karume ya kutoagiza chakula na bidhaa nyingine kutoka nje; akaruhusu akiba ya fedha za kigeni kutumika kuagiza chakula kumaliza tatizo la njaa na upungufu wa vitu, jambo lililokuwa mwiko wakati wa Karume.

Vivyo hivyo, kwa mara ya kwanza, Serikali ya Zanzibar iliruhusu wanafunzi 17 kutoka Zanzibar, kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi kupeleka wengi zaidi.

Desemba 1972, ASP kilifanya Mkutano Mkuu wake wa kwanza tangu 1962 uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 900 kutoka Visiwani, Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wa TANU, pamoja na wageni wengine kutoka nchi 12 za Kiafrika, wakiwamo wawakilishi wa chama cha MPLA cha Angola.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jumbe alilaani tawala za kimabavu na ubabe, ukandamizaji na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya raia, alisema:- Viongozi lazima wawatumikie watu, na si watu wawatumikie viongozi.

Kwa maneno hayo, alikuwa amefungua milango ya demokrasia Visiwani, utawala bora, uwajibikaji na kuongoza kwa mifano, tofauti na enzi za Karume.

Februari 5, 1977, Nyerere na Jumbewaliunganisha vyama vyao, TANU na ASP, kuunda Chama cha Mapinduzi CCM, jambo ambalo lisingewezekana wakati wa Karume ambaye hata Muungano wenyewe aliweza kuusigina kwa kisigino cha nguvu.- Vivyo hivyo, mwaka 1979, Zanzibar ilijipatia Katiba yake ya kwanza baada ya Katiba ya Uhuru ya 1963, chini ya Serikali ya Mseto wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP).

Ni wakati wa utawala wa Jumbe, Zanzibar ilipata Bunge (Baraza la Uwakilishi) lake la kwanza kwa njia ya uchaguzi, wakati kabla ya hapo, Karume aliapa pasingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50, kuanzia 1964 hadi 2014.

Chini ya Jumbe, kwa mara ya kwanza tangu 1964, wanasheria waliruhusiwa kufanya kazi Zanzibar; watuhawakugongewa tena milango usiku na kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Na tazama, yote yalifanywa kuwa mapya, ambapo isingewezekana chini ya utawala wa Rais Karume.

Nani alimuua Karume?

Share: