Makala/Tahariri

Nani Mkosa katika Vita na Michafuko ya Congo ?

Makala na Othman Miraji (25032017)

Umoja wa Mataifa na idara yake inyosimamia operesheni za wanajeshi wake wa kulinda amani ziko katika mzozo mkubwa. Hilo limedhihirika wazi j wiki hii wakati wa majadiliano ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York kuhusu hali ilivyo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kibali cha kuweko majeshi ya Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati (Monusco) -operesheni ilio ghali na kubwa kabisa- kinabidi ifikapo Machi 31 kirefushwe kwa mwaka mmoja. Lakini ripoti iliyowasilishwa mbele ya Baraza hilo ni ya kuhuzunisha sana. Pia majadiliano ndani ya baraza hilo yaligeuka kuwa ya kutupiana lawama juu ya nani aliye mkosa wa hali ilivyo sasa huko Congo.

“Hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inatia wasiwasi.” Hivyo ndivyo alivyoanza kusema mjumbe wa Baraza la Usalama katika Congo ambaye ni mkuu wa Monusco, Maman Sidikou, katika ripoti yake. Alitoa sura vipi matumizi ya nguvu yanayosababishwa na mivutano ya kikabila yanavyozidi kuenea. Alisema karibuni vitendo vya matumizi ya nguvu vimesambaa hadi katika maeneo ambayo katika miaka ilopita hali ilikuwa tulivu.

Mkuu huyo wa Monusco aliwalaumu watu wa tabaka la juu katika mji mkuu wa Kinshasa ambao wanaitumia hali ya mambo isiokuwa na muelekeo na wanawatumia kwa maslaha yao wanamgambo walioko katika maeneo ya michafuko. Alisema hatari ya kutokea mapigano ya kisiasa ni kubwa katika miji, huku akilitilia nguvu jambo hilo kwa kutoa tahadhari.

Maman Sidikou alisema vitendo vya kuendewa kinyume haki za binadamu vimeongezeka kwa asilimia 30 mnamo mwaka 2016 ukilinganisha na mwaka wa kabla. Asilimia 64 ya uhalifu wa kukiuka haki za binadamu ulifanywa na vyombo vya usalama vya dola, na asilimia 36 tu vilitekelezwa na waasi na pia wanamgambo. Hali hiyo inafanya kuwa ngumu kazi ya Monusco katika kuendesha operesheni zake ambapo inatakiwa pia ishirikiane kwa karibu na jeshi la serikali..

Kutokana na hali ilivyo, Monusco imegeukia kuwekea uzito kusaidia kuwaandikisha katika daftari wananchi wanaotaka kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao. Pia inaisaidia serikali na Upinzani kuutekeleza mwafaka uliokubaliwa na pande mbili hizo Desemba 31 mwaka jana. Kwa ufupi: Umoja wa Mataifa unasaidia, kupitia uchaguzi mkuu ujao, kuuwekea kikomo, kwa upesi kama iwezekanavyo, urais wa Joseph Kabila.

Matamshi ya mkuu wa Monusco Maman Sidikou, japokuwa yalitolewa kwa lugha ya kidiplomasia, lakini ukiyapima yanatoa ujumbe kwamba Monusco, ikibidi, itakuwa tayari kulumbana na utawala wa Kabila. Na itafanya hivyo, licha ya kutambua kwamba Kabila aling’ang’ania kubakia zaidi madarakani wakati kipindi chake cha pili kilipomalizika Desemba mwaka jana. Haishangazi kuona kwamba msimamo wa serikali ya Congo katika majadiliano ya mjini New York ulikuwa mkali na wa uchokozi.

Ni jambo “lisilokubalika” kwamba Monusco haina uwezo wa kuukomesha mzozo wa Congo, alifoka Leonard She Okitundu, makamo wa waziri mkuu wa Congo na ambaye wakati huohuo ni waziri wa mambo ya kigeni. Alisema serikali haitozuwia juhudi za kutaka kufanyike uchaguzi katika mazingira ya amani na uwazi. Lakini wakati huohuo alidai kwamba Monusco inachelewesha kutuma vifaa vya kuendeshea uchaguzi.

Okitundu alisisitiza kwamba jeshi la Congo limebeba shughuli za kijeshi za vikosi vya Umoja wa Mataifa katika kuendesha vita dhidi ya waasi na wanamgambo. Alidai kwamba wanajeshi wengi wa Umoja wa Mataifa wanakataa kugawana habari na wanajeshi wa serikali, kwa hivyo ushirikiano baina ya pande mbili hizo umekuwa mgumu. Mwisho makamo huyo wa waziri mkuu wa Congo alilitaka Baraza la Usalama liondoe kutoka Congo sehemu ya jeshi lake na pia litayarishe mpango wa kukomesha operesheni za Monusco katika nchi hiyo..

Maman Sidikou hataki kabisa kusikia maneno yanayozungumzia kupunguzwa sasa idadi ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walioko Congo. Yeye anataka idadi ya watumishi wa Umoja wa Mataifa katika Congo iongezwe kwa kupelekwa nchini humo polisi 320 zaidi na pia magari 36 ya kijeshi yalio na silaha. Takwa hilo linaonesha kwamba hapo kabla Monusco yenyewe ilizubaa. Jambo moja ni wazi: Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani katika Congo unahitaji polisi zaidi kuliko wanajeshi. Hivyo, lazima kuna mkakati mpya unapikwa.

Maman Sidikou alilikwepa suala la wapi walipo mabingwa wawili wa Umoja wa Mataifa waliotekwa nyara huko Congo. Hajazungumzia hata kidogo juu ya mustakbali wao. Kwa zaidi ya siku kumi sasa wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa hawajulikani waliko. Wao walipewa jukumu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wachunguze juu ya mauaji yaliotokea katika Mkoa wa Kasai baada ya jeshi la serikali ya Congo kupambana na wanamgambo. Makaburi manane yaliyokuwa na maiti nyingi yaligunduliwa.

Kwa upande wake Okitundu alihakikisha kwamba jeshi la serikali linajaribu kuwatafuta mabingwa hao wawili waliopotea. Meneno hayo yanaonekana kuwa ni ya kipuuzi kwa vile jeshi la serikali hivi sasa linawazuwia wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kuzidisha shughuli za kuwatafuta watu hao.

Wachunguzi Michael Sharp wa kutoka Marekani na Zaida Catalan wa Sweden zaidi ya wiki mbili zilizopita waliripotiwa wamepotea pamoja na mkalimani wao wa Kicongo. Hapo kabla Kamishna wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu, Ra’ad al-Hussein, alitangaza kumegunduliwa huko Kasai makaburi ya halaiki ya watu.

Video za simu za mkononi ziliwaongoza wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa kwenye maeneo yalikokuweko makaburi hayo. Picha za Video hizo zilionesha ukatili mkubwa uliofanywa, namna wanajeshi wa serikali ya Congo walivyowauwa vijana barabarani, wengi wao wakiwa bado ni watoto. Vijana hao walikuwa tu wamekamata magongo walipokuwa wanaandamana, huku wakiwalalamikia wanajeshi kwa maneno makali. Vijana hao walinyamazishwa kwa kufyetuliwa risasi za bunduki. Kamera ya simu ya mkononi, inashukiwa ya mmoja wa wanajeshi, ilirikodi kwa dakika saba tukeo lililoonesha maiti kadhaa pamoja na watu waliojeruhiwa vibaya. Watu wengine waliokuwa bado hawajafa walifyetuliwa risasi zaidi. Wakati mauaji yakifanyika kulisikika nyuma sauti za watu wakisheherekea.

Hao waliouawa ni wanamgambo wa aliyekuwa chifu wa kijadi wa eneo hilo, Kamuina Nsapu, ambaye alimpinga Joseph Kabila. Mkoa wa Kasai ni ngome ya Upinzani. Nsapu aliuliwa na polisi Agosti mwaka jana, na tangu wakati huo kumekuweko mapambano baina ya jeshi na wafuasi wa Nsapu. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa ni kwamba katika mapambano yake na wanamgambo jeshi la serikali limewauwa si chini ya watu 400. Zaidi na zaidi wanamgambo wanaingia katika miji mikubwa. Vyombo vya habari viliwahi kuripoti kwamba kulitokea mapigano katika mji wa Kananga ulio na wakaazi milioni moja na ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Kasai ya Katikati.

Wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa waliondoka Kananga kabla ya kuelekea kwenye barabara nje ya mji. Habari zinapingana. Kuna ile inayosema na kuenezwa na jeshi la serikali kwamba wachunguzi hao wametekwa nyara na wanamgambo wa Nsapu. Pia kuna habari nyingine inayodhania kwamba watu hao wawili walitekwa nyara na wanajeshi wa serikali ili kuzuwia uchunguzi wa mauaji yaliofanywa.

Charles-Antoine Bambara, msemaji wa Umoja wa Mataifa katika Congo ( Monusco) amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa utafanya kila kinachowezekana ili kuwapata mabingwa hao.

Kisa hiki kimetokea wakati muhimu. Mwisho wa mwezi huu wa Machi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litabidi lirefushe muda wa kuweko jeshi la Usalama la Umoja huo katika Congo. Kwa miaka sasa Rais Joseph Kabila ametaka majeshi hayo yaondolewe. Pia Umoja wa Mataifa unataka wanajeshi hao waondoke, lakini si sasa, bali hadi pale kile walichokiendea kimetekelezwa: kutoweka wanamgambo wote. Kwa sasa Umoja wa Mataifa utataka idadi ya wanajeshi wake huko Congo iongezwe. Hasa kwa vile katika siku za karibuni imedhihirika kwamba wanajeshi na polisi wa nchi hiyo ndio wanaotenda ukatili mkubwa .

Share: