Makala/Tahariri

Nani wa kulaumiwa?

Nimekaa uwanja wa ndege wa ‘Kimataifa’ wa Karume, nikisubiri ndege kuondoka kuelekea ughaibuni  huku moyo wangu ukibubujikwa na machozi ya kuiaga nchi yangu na kuitathmini hali ya jengo la uwanja huu wa ‘kimataifa’ namna inavyoakisi kiwango cha uozo na  uharibifu wa makusudi wa watani wangu nabaki kujiuliza, Zanzibar masikini tumekukosea nini?

Kuna siku wakati nimepumzika hapo nyumbani, nilitumiwavideo ya wassap ya uwanja huu huu namna sehemu ya maegesho ya ndege ilivyojaa maji ya mvua huku abiria wa Oman Air wakipanda kuelekea ndani utadhani wapo bandarini, chini ya video hio huyo alieyeituma ameandika ‘Bandar Kisauni’,  yaani ‘Bandarini Kisauni’ na sio uwanja wa ndege, niseme tu nilikubaliana nae na uono wake na kucheka kicheko cha kujionea huruma, tusamehe Zanzibar!

Nifupishe kuelekea lengo hasa ya mada hii, ila ya hili jengo na barabara ya kuelekea liliko hili jengo yanaakisi ni namna gani tumefika hapa tulipofikishwa na ‘ wanasiasa wasomi’ wa nchi yetu adhimu, wasomi walioichanganya siasa katika kila kitu.

Wakati safari inaanza kuelekea kuruka nikaliangalia jengo lililo pembeni  ambalo hadi sasa sijui limechukua muda gani kukamilika, ni jengo tunaambiwa litakua terminal mpya ya kisasa ama tuiite ya ‘kisiasa’, terminal isiyokamilika na pengine isikamilike kamwe.

Wakati ndege inainuka katika ardhi ya Zanzibar suala linanijia na kujiuliza, hadi lini uteseke mama  Zanzibar? Jawabu nilioliwaza likazaa masuala zaidi ya majibu.

Naam, ya leo niliokusudia baada ya tathmini ya kukaa nyumbani ni namna gani sisi wenyewe kwa  mikono yetu tunavyoiua Zanzibar, baadhi kwa kutojua na wengine kwa makusudi,kasi hii ya uharibifu wa nchi yetu inafanywa huku hao wachache wenye kujua wakikaa kimya na wengine wakiipalilia kwa kuweka ukereketwa wa siasa mbele kuliko uzalendo.

Lakini kabla sijawahukumu wote, niwape hongera za dhati ndugu zetu wa uwanja wa wa ndege katika sehemu zote, ndugu zetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na ustahamilivu wa hali ya juu, wanaowaangusha kama ilivyo kawaida ni hawa wasomi wetu watengenezaji. Wapi  tuanze?

Kama nilivyolitolea mfano jengo, kasi hii ya uharibifu uliopachikwa jina la utengezaji  imo katika sehemu zote katika jamii yetu, ila leo nitajitahidi kuanza  katika maeneo tunayoteketea ya muhimu, na kama utakisia tayari, matatizo ya Zanzibar ni marefu mno kumalizia kwa mada moja, itanibidi kuanza na moja na kuendelea na sehemu nyengine siku nyengine. Tuanze na  la kwanza kwa umuhimu wake ambalo ni  afya.

Ndugu zangu wazee na ndugu zetu wanateketea kwa uharibifu uliopachikwa jina la uimarishaji wa afya za wananchi, kama umeshapata habari ama bado kuna ugonjwa ambao umeingia Zanzibar unaitwa Kigugunya, ama sijui huu ugonjwa jina lake asili yake ni wapi na nini, ila kwa kushindwa kulitamka  jina hilo wengine wanaita homa ya ‘muungano,’ sina uhakika ni huu muungano tulionao ila adha ya ugonjwa huu usiombe ukaipata , ni zaidi ya huo muungano.

Unapokupata ugonjwa huu kama hujakimbizwa haraka kupata dripu, maana kwa miguu yako hutoweza kuinuka unapokubana viungo vyote hupoteza netwaki na nguvu basi uko njiani kufa, ama zako ziwe bado zikalipo.

Kwa mawazo ya haraka haraka ungelifikiria kwamba wasomi wetu wamo katika hatua za dharura kutafuta chanzo na kinga za ugonjwa huu, la hasha! Bado umekosea maana hata sababu hasa haijajulikana ya chanzo cha ugonjwa huu, wengine wanasema ni mbu,tena mbu huyu hakutafuni usiku bali mchana kweupe! Hawakukosea waliouita ugonjwa huu  homa ya ‘muungano’.

Ukisalimika na huu ‘muungano,’ kuna ugonjwa wa ‘gesi’ ambao kila kukicha unathakilli afya za ndugu zetu, gesi imehamia katika matumbo ya wazee na ndugu zetu, chanzo ni nini? Aah, wengi wanasema ni ubora wa vyakula tunavyokula na maji tunayokunywa, ubora wa vyakula kwa maana ya vyakula tunavyouziwa  hasa  ‘wali’ ama mchele ni vibovu na havifai kwa matumizi ya mwanadamu, na maji kwa maana ya maji tunayokunywa ni machafu, upatikanaji wake ni mtihani, kila sehemu kuna matanki  ya maji, jaribu Michenzani, ya mji mkongwe kwa kuyajaribu hasa ni maji yaliyo na ladha ya chumvi.

Katika visiwa ambavyo idadi ya watu wake inajulikana udogo wake, ni kwa namna gani idadi ya matatizo ya kiafya kwa tathmini yangu yanazidi ya walio na afya imara hili linanipa tabu kutafuta jawabu kutoka kwa wasomi watengezaji, maana unayemuuliza katiaka ndugu na wazee wetu hapo nyumbani  atakueleza yake yeye na ya karibu yake yeye,  waliotangulia tayari katika wazee na ndugu zetu kwa sukari, presha, safari za India kwa wanaojiweza kidogo kutafuta afueni ni za kupishana.

Tatizo linajulikana wapi lipo, je tutibu chanzo ama matokeo?

Itaendelea.

 

 

 

 

 

Share: