Makala/Tahariri

Profesa Sharif: Karume alidhani amesaini Shirikisho la Afrika Mashariki, si Muungano wa nchi mbili

WAKATI Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ukitimiza miaka 48 mwaka huu, kumekuwa na harakati nyingi visiwani Zanzibar za kutaka uhuru mpya wa visiwa hivyo na kuupinga Muungano wazi wazi.

Watu wamekuwa wakijadiliana kupitia kwenye makongamano, mabarazani na hata kwenda mahakamani kutafuta uhalali wa Muungano. Kupitia njia hizo Wazanzibari wametoa sababu mbalimbali za kupinga Muungano.

Katika kongamano la uundwaji wa Katiba mpya ya Tanzania na suala la muungano kwa Zanzibar, hali ya kutokubalika kwa Muungano ilijionyesha waziwazi.

Akitoa mada katika kongamano hilo, Profesa Abdul Sharif anasema kuwa ikiangalia historia ya Muungano imejaa kasoro zinazoondoa kabisa uhalali wake.

Anasema suala la Muungano lilikuwapo barani Afrika kabla hata ya nchi zake kupata uhuru ambapo zilitaka Muungano wa Shirikisho.

“Nchi za Afrika Mashariki zilikubaliana kwamba, zikipata uhuru zitaanzisha Muungano wa Shirikisho (East African Federation). Hata Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba, yuko tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika mpaka nchi zote za Afrika Mashariki zitakapopata uhuru kwa pamoja ili kuunda ‘federation’, ” anasema Profesa Sharif na kuongeza;

“Miezi mnne kabla ya uhuru wa Zanzibar, Waziri wa Kenya, Tom Mboya alipelekwa na nchi hizi, Kenya Uganda na Tanganyika kuwauliza watu wa Zanzibar kama wako tayari kujiunga na Shirikisho; Zanzibar ikajibu kwamba iko tayari. Hata Afro Shirazi Party hawakuwahi kusema kuwa wanataka kuungana na Tanganyika peke yao, haikuwa sera yao. Hata Karume alidhani amesaini shirikisho.”

Anaendelea kusema kuwa kabla ya kutokea shirikisho hilo, kukatokea Mapinduzi Zanzibar yaliyofuatiwa Muungano ambao hawakuutarajia;

“Lakini baada ya siku 100 tu baada ya Mapinduzi ghafla tunasikia kuwa Zanzibar na Tanganyika zinaungana katika mfumo mpya kabisa. Sasa tujiulize, kwa kiasi gani watu wa Zanzibar waliulizwa kama wanautaka muungano huu?”
Jambo la pili kwa mujibu wa Profesa Sharif linalotilia shaka uhalali wa Muungano ni wakati wa makubaliano ya Muungano kati ya Mwalimu Nyerere na Abeid Karume.

“Tunajua kuwa marehemu Karume alipokwenda Dar es Salaam kuzungumzia Muungano hakuruhusiwa kuchukua mshauri wake wa sheria (Attorney General) au mtu mwingine.

“Mfumo mzima wa Muungano uliundwa na washauri wa Mwalimu Nyerere waliokuwa wazungu. Wao walitumia Katiba ya Ireland Kaskazini wakati ilikuwa ni koloni ya Uingereza. Wamebadilisha hapa na pale ndiyo wakafanya Hati ya Muungano tuliyopewa.” Anaeleza Profesa Sharif.

Anataja kasoro ya tatu ya Muungano kuwa ni kubadilishwa kwa Hati za Muungano bila mashauriano. Anasema pamoja na kuwa mkataba ule ulikuwa ni wa kimataifa, ulikuwa pia ni wa kisheria.

Profesa Sharif anasema kuwa mkataba ule haukuridhiwa na upande wa Zanzibar kama ulivyoridhiwa na Bunge la Tanganyika.

“Kama Hati ya Muungano ni mkataba wa kimataifa, kweli wale marais wanaweza kusaini lakini inatakiwa uridhiwe na mabunge ya pande mbili. Tunajua kule Bara, Bunge lilikutana na lilaridhia, lakini huku Zanzibar hakuna dalili yoyote kwamba mkataba ule uliridhiwa na Baraza la Mapinduzi, ambalo ndilo lilikuwa Baraza la Kutunga Sheria.”

Muungano si halali?
“Kwa hesabu yetu sisi Katiba inakuwa halali pale wananchi wanaposhirikishwa na wanapotoa ridhaa yao, uhalali unatokana na watu. Mimi naweza kusema kwamba Muungano wa 1964, yalikuwa ni mapinduzi ya kikatiba, (constitution coup d’ etat),” anasema Profesa Sharif.

Huku akitumia mizani kuonyesha kutokuwapo kwa uwiano katika Muungano wa sasa, Profesa Sharif anasema Muungano wa sasa umepora madaraka ya Zanzibar.

“Tofauti na Muungano wa Shirikisho tulioutarajia ambapo tungekuwa tunachangia sehemu moja, Muungano uliokuja ukawa unahamisha madaraka ya Zanzibar na kuyapeleka kwenye Muungano,” anasema na kuongeza,
“Mambo 11 ya Zanzibar yakatolewa kutoka Zanzibar yakatiwa Tanzania. Mizani haiko sawa.

Ingeishia hapo watu wangekaa kimya. Lakini katika miaka ya baadaye, miaka miwili au mitatu, mambo yakaendelea kutolewa na kuwekwa Tanzania, kuanzia sarafu mwaka 1965, mafuta na gesi mwaka 1968, Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973. Mpaka leo mambo 11 mengine yametolewa huku na yametiwa huku. Sasa hii ya kutoa madaraka huku na kupeleka huku ilikuwa halali?”

Huku akimnukuu Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Profesa Issa Shivji, Profesa Sharif anasema, “Huu ni unyang’anyi katika Muungano. Mambo yote yaliyohamishwa yalikuwa si halali ni batili”.

Anaongeza kuwa licha ya ushauri wa Profesa Shivji alioutoa mwaka 1993, bado Serikali ilimpuuza ambapo mwaka 1995 wakamwondoa Rais wa Zanzibar asiwe tena Makamu wa Rais wakamleta Mgombea Mwenza ambaye ndiye anayekuwa Makamu wa Rais.

“Rais wa Zanzibar anachaguliwa na watu wa Zanzibar na anakuwa kiunganishi kati ya serikali ya Zanzibar na Muungano, kumwondoa yeye imekuwa tena Muungano umekatwa kimakusudi, hauko tena moja kwa moja”.

“Makamu wa Rais amechaguliwa na Watanzania wote anawasema wote. Rais ndiyo alikuwa mwakilishi, alikuwa akitusemea, mwenza hawezi kutusemea hata kama amezaliwa Zanzibar. Mpaka imefika wakati, hata Jaji Mkuu na Waziri Mkuu wanasema Zanzibar siyo nchi.”

Katiba ya Muungano 1977 ina uhalali kiasi gani?
Kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Profesa Sharif anasema haikuwa na uhalali kwa sababu pia haikushirikisha wananchi kikamilifu.
Anaongeza kuwa Katiba hiyo ilitokana na Muungano wa vyama vya ASP na TANU vilivyounda CCM.
“Baada ya kuungana kila upande wa Muungano ulitoa watu 10 kwa ajili ya kuandika katiba ya chama.

Mwalimu Nyerere kama Mwenyekiti wa CCM akateua watu 20 kuandika katiba ya Tanzania iliyokamilika ndani ya wiki moja.

Baada ya hapo ikapelekwa kwenye chama maana wakati huo ndiyo chama kimeshika hatamu. Wakaipitia kwa wiki mbili kisha ikapelekwa kwenye Bunge.

“Wabunge watatu tu wakaruhusiwa kusema, baada ya hapo Waziri Mkuu wakati ule Edward Sokoine akasema, jamani nchi hii inatawaliwa na chama kimoja na chama kimekamata hatamu, maadamu chama kimeshaipitisha Katiba basi Bunge halina haja tena ya kujadili. Watu wakapiga makofi. Mchango wa wananchi ukawa ni makofi,” anasema.

Jambo jingine linalotatiza Muungano katika Katiba kwa mujibu wa Profesa Sharif ni ibara ya 64 inayohusu kazi za Bunge na sheria zinazopaswa kutumika Bara na Visiwani.

“Wamepenyeza kwa mlango wa nyuma kwa kuzidisha madaraka ya Tanzania Bara na kupunguza madaraka ya Zanzibar katika ibara ya 64. Sasa kama tayari mko kwenye Muungano, kwanini tena mseme sheria hii itumike huku na nyingine itumike huku?” Anahoji Profesa Sharif.

Anataja baadhi ya sheria zinazoinyima Zanzibar madaraka kuwa ni pamoja na Sheria ya vyama vya siasa ya 1992 ambapo hapo awali haikuwa ya Muungano.

Sheria nyingine ni ya Bahari na Uvuvi ambayo awali haikuwa ya Muungano, lakini mwaka 1989 ilifanywa kuwa ya Muungano baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Bahari na Maeneo ya Uchumi wa Bahari (Territorial Sea and Exclusive Economic Zone).

“Mwaka 1993 wakapitisha tena sheria ya Bahari Kuu na hivi karibuni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka ametumwa kwenda Umoja wa Mataifa kupeleka ombi kuzidisha eneo la bahari ya Tanzania bila kushirikiana na Zanzibar . Ikiendelea namna hii mwisho wake hapa Zanzibar tutabakia na nini?” Anahoji Profesa Sharif.

Kwa kuwa Muungano ni suala la kisheria, Profesa Sharif anashauri kuwa kabla ya kubadilisha jambo lolote, ipigwe kura ya maoni ili kupata theluthi mbili ya Watanzania kukubali jambo hilo.

“Unapopunguza madaraka ya Serikali ya Zanzibar peke yake linakua suala la Kikatiba, sheria zote hizo zimepitishwa Bungeni na zinaongewa kule bila hata kupata theluthi mbili ya Wazanzibari wala Watanganyika. Tungehitaji kupata theluthi mbili ya maoni ya watu kuhusu mabadiliko hayo. Vinginevyo ndivyo tumekuwa tukiporwa madaraka yetu tangu 1977,” anasema.

Nini kifanyike?
Anamalizia kwa kusema kuwa Muungano huu hauna uwiano kwani Tanzania Bara ni kubwa kieneo na kwa idadi ya watu huku Zanzibar ikiwa ndogo, hivyo anashauri kubadilishwa kwa mfumo wa Muungano.

“Twende wapi? matatizo ya Muungano, siyo kwamba wanaroho mbaya, muundo wa Muungano una kasoro, haukuthamini uhuru wa Zanzibar kikamilifu. Tubadili mfumo huu. Hakuna uwiano kati ya Tanganyika yenye watu zaidi ya 40 milioni na Zanzibar yenye watu milioni moja. Huwezi kumweka Simba kubweka na kondoo pamoja,” anasema Profesa Sharif.

Mwananchi

Tagsslider
Share: