Makala/Tahariri

Rasimu ya II ya Katiba: ni mtego uliomnasa na kumuangusha Jumbe 1984 ?

 • Rasimu ya pili ya katiba: je,mtego uliomnasa na kumuangusha Jumbe,1984 utamnasa rais Shein 2014 ?

 • Na Laila Abdullah

  Rasimu ya pili ya Tume ya Jaji Warioba katika mojawapo ya vifungu vyake inasema,

  “Jamhuri ya muungano wa Tanzania ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na muungano wa nchi mbili za jamhuri ya Tanganyika na jamhuri ya watu wa Zanzibar……”

  Ikiwa ni “Shirikisho lenye Mamlaka Kamili”, basi Jaji Warioba na Tume yake, wanawatia Wazanzibari katika MTEGO ule ule alioutumia Mwalimu Nyerere, alipopendekeza kwa Rais Aboud Jumbe kuunganisha Afro-Shirazi Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) na kuunda CCM.

  Na mara tu baada ya Rais Jumbe, kutekeleza hilo,akamzunguka na kabadilisha Katiba na kukifanya Chama cha Mapinduzi (CCM) -SUPREME- chenye “Mamlaka Kamili” au KAUL YA MWISHO mjini DODOMA .Yeye mwenyewe akiwa Mwenyekiti.Wengi waliamini eti alistaafu kama Rais wa Tanzania,kumbe amehamishia tu madaraka chamani alikokaliah kiti.

  Rais Jumbe, alipotanabahi nchi na chama chake imeingizwa mtegoni,ikawa KISHADA kimesha kwenda arijijo.Juhudi za Rais Jumbe na wanasheria wake akina SWANZY na Dourado, kujinasua na kuinusuru Zanzibar,ziligonga mwamba huko Dodoma, 1984.Ikawa kama wasemavyo waswahili:”Majuto ni mjukuu.” Kuanzia hapo hatima ya Zanzibar, ASP na ya viongozi wake, imekuwa ikiamuliwa na chama huko Dodoma na sio KUSIWANDUI-makao Makuu ya ASP.

  Laiti Jumbe hangeunganisha ASP na TANU,Mwalimu asingeweza kumshinikiza ajiuzulu kule Dodoma.Angemwambia sikiliza: ” Wewe ni Rais wa TANU na Mimi ni Mwenyekiti wa Afro-Shirazi Party,Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar.Ni vyombo hivyo tu huko visiwani,ndivyo vyenye mamlaka ya kuniuzulu.”Pale Rais Jumbe alipoihitajia sana TURUFU hakuwanayo tena kuicheza mezani kule Dodoma, Mwalimu alimcheza na kumnasa kwa “mtego wake wa panya”.

  Sasa Jaji Warioba na mwenzake Dr.Salim Ahmed Salim,katika Tume ya Katiba , sio tu waliwahi kuwa Mawaziri-wakuu chini ya Mwalimu Nyerere vipindi tofauti, bali ni wajumbe pia wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere”-NYERERE FOUNDATION”.Taasisi hii ina jumuku la kuenzi na kutukuza itikadi na maadili ya marehemu Mwalimu.Vigogo hivi viwili, vimeongoza Tume ya Katiba hii mpya ambayo Rasimu yake ya Pili, amekabidhiwa Rais Jakaya Kikwete na wadau wengine hapo Desemba 30, 2013 mjini Dar-es-Salaam.

  RASIMU HII YA PILIi imekuja na MTEGO mwengine wa panya. Mara hii sio kuipokonya CCM-Zanzibar mamlaka ambayo hainayo tena (Kesi ya Dr.Amani na Dr.Gharibu) yatukumbusha hayo,bali ikiwa Dr. Mohamed Sheni, Rais wa Zanzibar na Wazanzibari kwa jumla, HAWATACHUNGA, basi hatima ya Zanzibar kama ” NCHI” yenye Mamlaka yalioanishwa na Rasimu ya Katiba kuwa”si ya Shirikisho”, itaangukia nayo kuamuliwa Dodoma na sio Zanzibar. Kero za Muungano zitaselelea badala ya kuzikomesha.Na ndoto ya waziri-mkuu Mizingo Pinda kuwa “Zanzibar si Nchi” itatimilia.

  Sidhani kuwa Jaji Warioba na mwenzake Dr.Salim ,hawaelewi nini maana ya “Tanzania ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili” au nini tafsiri (defination ) ya Shirikisho?

  Tafsiri ya “Shirikisho” ni kuwa na “CENTER”-yaani shina-DODOMA na Tawi-Zanzibar na sasa Tanganyika.Na mamlaka ya kila upande (Constituency) yanafafanuliwa wazi- tena dhahiri-shahiri ili kila Upande usiingilie mambo ya mwenziwe au constituency ya mweziwe.

  Sasa unaposema “JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NI NCHI NA SHIRIKISHO LENYE MAMLAKA KAMILI“, huo ni mtego mwengine wa kupora mamlaka ya Zanzibar na ya nchi mpya iliofufuka ya Tanganyika; na kulifanya Shirikisho-SUPREME”-lenye mamlaka kamili hata katika maswsali yasio ya Shirikisho.NI MARUDIO ya mtego wa Mwalimu uliomnasa Jumbe 1984 mjini Dodoma.

  Kudai “Tanzania ni nchi na Shirikisho” ina maana tutakuwa chini ya Katiba mpya na nchi 3 badala ya mbili, kama vile Ujerumani Magharibi na Mashariki zilipounda 1990, Shirikisho moja linalojulikana leo “THE FEDERAL REPUBLIC OF GERMANY”. Kinyume na Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Ujerumani ilikuwa nchi moja -Unitary State-kabla ya vita vya pili vya dunia na ilirejea kuwa hivyo ingawa chini ya mfumo wa shirikisho hapo Oktoba 3, 1990 baada ya kuporomoka ukuta wa Berlin.

  1984 ilikuwa ni hatima ya JUMBE na Afro-Shirazi Party ilioamuliwa kule Dodoma , mara hii NI HATIMA YA WAZANZIBARI NA YA VIZAZI VIJAVYO kwa jumla,ilio mashakani. Dr.Shein,CCM-Zanzibar na Wazanzibari -bila ya kujali vyama na Jumuiya zetu,tunapaswa mara hii, KUCHUNGA ili “Mtego wa Panya” usitunase tena !

  Rais Mohamed Shein, kama Rais wa Zanzibar, ULIEKULA KIAPO KUITETEA na KUILINDA ,na kama unavyodai wewe PEKEE NDIE WA KUISEMEA,JUKUMU liko mabegani mwako -kuikoa Zanzibar au kufuata sera za chama!a

  Tagsslider
  Share: