Makala/Tahariri

Roho zao zitazidi kudamirika

Na Jabir Idrissa,

INGAWA sijaipata nakala ya ripoti ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar ambayo tayari ilikabidhiwa kwa Dk. Ali Mohamed Shein, Februari 9, mwaka huu, nimebaini aibu ndani yake.

Ni aibu kwa sababu ubunifu uleule wa uongo umeruhusiwa kuwa sehemu ya maelezo kwenye ripoti hii ambayo penye uongozi unaojiheshimu, ingetarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kusaka maendeleo ya kweli ya kidemokrasia.

Ubunifu wenyewe ni mambo ya kutunga. Yaleyale ambayo kwa zaidi ya mwaka tangu uchaguzi mkuu ulipofanyika 25 Oktoba 2015 na kuhujumiwa kwa kufutwa kibabe siku tatu baadaye, yameshindikana kuelezwa kwa bayana au sema hayajaelezwa kiadilifu, yamekutwa kwenye ripoti.

Kwa mfano, eti Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha anasema kulikuwa na tatizo la ucheleweshaji wa “makusudi uliopangwa” wa kuwasilisha matokeo ya kura za urais.

Inaelezwa kwamba ucheleweshaji huo ulifanywa kwa ushirikiano na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya kisiwani Pemba. Hivi ucheleweshaji huu uliripotiwa wapi? Mbona hakukusikilikana chama chochote kulalamikia ucheleweshaji huu?

Hizi taarifa katika ripoti kwamba kuna fomu za matokeo zilizoonekana kurejeshwa namba nyingine juu yake na baadhi yake kufutwa matokeo yake kwa wino maalum na kuandikwa kwa mkono, zilitokea wapi? Ni chama gani kililalamika?

Inapoelezwa kwamba kulikuwa na upigaji wa muhuri wa kituo cha kupigia kura katika fomu za matokeo ya vituo vingine kinyume na maelekezo ya Tume, hii taarifa ndio inakaaje hasa?

Jecha ameeleza wakati wa kusoma taarifa yake mbele ya Dk. Shein kwamba katika baadhi ya vituo vya kupigia kura vilikuta matokeo ya vituo yakiwa yamebandikwa lakini fomu za majumuisho zilikuwa na marekebisho mengi yaliyofanywa juu ya wino mweupe kuficha udanganyifu na katika fomu nyingine wagombea walipunguziwa kura.

Kwamba wasimamizi waliopewa jukumu la kuratibu shughuli zote za ujazaji wa matokeo ya kura kwenye fomu halali za Tume ya Uchaguzi Zanzibar walikuwa wamelala usingizi wa pono au walilishwa nusu kaputi ili wasione hao waliohujumu?

Na kinachosikitisha ni kwamba taarifa hizi zinarudiwa kwenye ripoti ya uchaguzi wakati hakuna hata mtu mmoja kufikia sasa aliyehojiwa na vyombo vya usimamiaji wa sheria, na hivyo kuwa na maana kuwa hakuna kesi yoyote mahakamani.

Hivi ni kweli Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inazingatia taarifa kama hizi kuwemo kwenye ripoti ya uchaguzi? Kwa sababu kama taarifa hizi ndio zinapigiwa chapuo zikielezwa kuwa ndicho ambacho Tume ilikiona, itakuwa na maana kuwa viongozi waliopo wamejitukanisha.

Kwamba mpaka leo hii, wameshindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wasimamizi waliohujumu uchaguzi na hivyo kusababisha hasara kwa serikali inayotumia fedha za wananchi.

Hiki ni kitu kisichoingia akilini labda tu kama wananchi na dunia wanatakiwa kuamini kuwa hizi taarifa za kuharibiwa taratibu za ujazaji wa kura kwenye fomu za Tume zilikuwa na manufaa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndio, kuna manufaa ya CCM, kwa sababu mara zote, na uzoefu wa matukio unaonesha haya, kuwa uharibifu wa uchaguzi unaonufaisha maslahi ya CCM hauna tatizo na huvumiliwa na mfumo wa usimamizi wa uchaguzi. Hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa kushughulikia wahusika.

Haiingii akilini kwamba matatizo ya uchaguzi yanayotajwa kama sababu ya kufuta uchaguzi mzima wa Zanzibar, yanayooneshwa ni yale yaliyotokea katika baadhi ya majimbo ya kisiwani Pemba, lakini uchaguzi ukafutwa majimbo yote 54.

Huu ndio ubunifu wa hali ya juu wa Jecha na makada wenzake wa CCM ambao waliamua kufisidi akili zao na kudharau maslahi ya nchi na watu wake mbele ya maslahi binafsi ya chama wanachokiabudu.

Kwa hakika haya yanayoelezwa kwenye ripoti ambayo Dk. Shein anatamba kuwa ndio halisi, ya kweli na hakutakuwa na ripoti nyingine yoyote, ni mambo ya kutunga yanayostahili kupuuzwa na watu wenye mapenzi mema na Zanzibar.

Hakuna uchaguzi uliovurugika si kwa majimbo ya Pemba wala ya kisiwani Unguja. Pangekuwa na hali hiyo, viongozi wa Tume wasingekuwa na nafasi ya kuficha maana kila mtu aliyekuwa maeneo husika, wakiwemo watazamaji wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi, wangelikuwa wameona.

Ninasikitika kwamba watu wazima wanaojinasibu kuwa wanaongoza kwa haki na kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na ilivyoelekeza Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, wanashikilia taarifa za kutunga na kuendelea kuzieneza hadi kwenye ripoti ya uchaguzi iliyotumika fedha nyingi za wananchi kuiandaa.

Kadiri uongozi wa Dk. Shein chini ya nguvu ya CCM na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo maamuru ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unavyojichimbia mamlakani kupitia mapinduzi ya maamuzi ya wananchi, ndivyo wanavyodhalilika na kujionesha kuwa hawaongozi kwa maslahi ya umma isipokuwa maslahi binafsi ya kifisadi na kidhalimu.

Kilichofanyika Zanzibar kuhusu uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 ni dhulma isiyomithilika. Wakubwa wa CCM wamedhulumu na kupitia njia hiyo wanakalia viti visivyowastahikia.

Bali dhulma haidumu na inapodumu matokeo yake huwa ni kuangamiza. Roho za wenye kudhulumu haziwezi kusafika hata iweje badala yake zitazidi kudamirika na kujinyonga kwa kuwa zinahofia adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Tagsslider
Share: