Makala/Tahariri

Siku ya kumtoa mhanga Theresa May yakaribia

Na Ahmed Rajab,

WIKI iliyopita katika sahafu hii niliandika kuhusu wingu linalozidi kutanda katika siasa za Uingereza. Sitozitendea haki siasa hizo ikiwa sitoendelea kuizungumza mada hiyo.

Sababu ni kwamba lile wingu nililolizungumzia wiki iiyopita limekuwa likitanda zaidi na limegeuka umbo. Limekuwa nene, limeteremka na sasa limemgubika kabisa Theresa May, waziri mkuu wa Uingereza. Hajijui, hajifai. Mambo yamemsakama na amewatumbukia nyongo Waingereza.

Yanayomkuta May yanaweza kuwa funzo kwa wanasiasa wengine, hata wale wa kwetu na hasa wale wa chama chenye viongozi wenye kibri kama walivyo wengi wa viongozi wa chama cha Conservative cha May. Kibri na kutowajali wananchi wa kawaida ni miongoni mwa mambo yaliyokiponza chama anachokiongoza May.

Jambo moja lililodhihirika tangu May awe waziri mkuu, Julai mwaka jana, ni kwamba yeye hana msimamo. Huwezi kumlinganisha na Margaret Thatcher, mwanamke wa mwanzo kuwa waziri mkuu wa Uingereza na aliyekuwa pia kiongozi wa chama cha Conservative. Thatcher alikuwa na sera zilizoichafua jamii na kuwaumiza wengi, hasa wa tabaka la chini. Lakini alikuwa na msimamo. Akijua akitaka nini na akishikilia kukipigania mpaka akipate.

May ni tofauti naye. Hajui anataka nini na wala hana msimamo. Nitatoa mifano miwili tu. Kabla ya kura ya maoni iliyofanywa Juni 23, mwaka jana ya kuamua iwapo Uingereza ibakie au itoke kutoka Muungano wa Ulaya (European Union), May alikuwa mtetezi mkubwa wa Uingereza isalie katika Muungano huo. Baada ya kura ya maoni iliyoamua kuwa Uingereza ijitoe kutoka EU, May akabadili msimamo.

Alipochaguliwa na wabunge wenzake awe kiongozi wa chama chao na kupata uwaziri mkuu, baada ya waziri mkuu David Cameroon kujiuzulu kufuatia hiyo kura ya maamuzi, May alisema kwamba hakuna haja ya kufanywa uchaguzi mkuu. Aliashiria kwamba ataendelea kuwa waziri mkuu hadi 2020. Mara ghafla, Aprili 18 mwaka huu alibadili msimamo akasema patafanywa uchaguzi mkuu Juni 8.

May akiamini kwamba chama chake kitakishinda kwa kishindo chama cha Leba kinachoongozwa na Jeremy Corbyn. Haikuwa hivyo. Aliumizwa vibaya baada ya chama chake kushindwa kujinyakulia viti vingi vya bunge katika uchaguzi huo. Badala ya kubwagwa Corbyn aliwashangaza wengi kwa chama chake kunyakua viti vingi kuliko ilivyotarajiwa.

Uchaguzi wa Juni 8 ni uchaguzi ambao May hakulazimika kuufanya lakini aliamua ufanywe kwa kuamini angepata kwa wingi mkuu viti katika bunge kumwezesha awe na nguvu wakati wa mashauriano na Muungano wa Ulaya (EU) ya mchakato wa Uingereza kujitoa kutoka Muungano huo. Mchakato huo una jina maarufu la mkato, “Brexit”.

Matokeo ya uchaguzi mkuu yalimuweka pabaya Theresa May, hasa ndani ya chama chake. Matokeo hayo yalimshtusha kiasi cha kumfanya aonekane kama hajui anafanya nini au afanye nini. Alikuwa kama mtu aliyepigwa na dhoruba.

Hata hivyo, aliweza kujizoazoa baada ya kuwahutubia wabunge wa chama chake Juni 12, na kuwataka radhi kwa matokeo mabaya ya uchaguzi. Kidogo alipata afueni. Lakini siku tatu baadaye, mambo yalimgeukia tena alipopata dhoruba nyingine baada ya kutokea maafa ya moto ulioliteketeza jumba la Grenfell Tower la ghorofa 24 lililo magharibi mwa London ambamo watu chungu nzima walifariki dunia.

May alilaumiwa kwa kutowajali ipasavyo waathiriwa wa moto huo.

Juu ya hayo, bado May aliendelea kujikokota. Na bado akiendelea kukabiliwa na hatari. Viongozi kadhaa wenzake wa chama chake wamemkalia chonjo. Kuna wenye visu wanaomvizia wamkate miguu; kuna washikao panga walio tayari hata kukifanya kichwa chake kiwe halali yao.

Wote wanakubaliana kwamba May hafai tena kuwaongoza. Serikali yake ni dhaifu na haiwezi kusimama bila ya msaada wa wabunge 10 wa chama kidogo cha Ireland ya Kaskazini cha Democratic Unionist Party (DUP). Mpaka hivi ninavyoandika, May bado hakupatana sawasawa na chama cha DUP.

Watu hawana imani naye sasa. Anayumbayumba na kama si leo basi kesho, na kama si wiki hii, basi wiki ijayo kuna siku lazima ataanguka. Pengine mwishoni mwa mwaka huu au hata mwakani, lakini kuna siku atapomoroka.

Siku hizi wamejitokeza wengi ndani ya chama chake wasemao kuwa Theresa May hafai kuwa waziri mkuu. Chama hicho kimegawika. Wabunge wake wanazozana na kulaumiana.

Baada ya kura ya maoni ya mwaka jana, uchaguzi mkuu wa mwaka huu, sidhani kama wapiga kura wa Uingereza wana hamu ya kwenda tena kupiga kura kwa hivi karibuni. Lakini patakuja siku lazima uchaguzi mkuu ufanywe na utapofanywa nina hakika ya mia kwa mia kwamba chama cha Conservative hakitoweza kufua dafu endapo Theresa May ataendelea kuwa kiongozi wake. Kwa sasa chama chake kimepwaya. Hakitoweza tena kusimama bila ya kuwa na kiongozi mpya.

Ikiwa hali ya mambo inayomkabili May itaendelea kuwa hivi ilivyo, basi nionavyo ni kwamba chama kitaamua kuwa na kiongozi mwengine kabla ya mkutano wake mkuu, ambao mwaka huu unatazamiwa kufanywa Oktoba Mosi hadi Nne, jijini Manchester.

Siku hizi May hapendezi Uingereza na hapendezi mbele ya macho ya viongozi wa nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya (EU).

Inasemekana kwamba baadhi ya mawaziri wana wasiwasi mkubwa kwamba May hawezi kufikiri sawasawa. Wanasema hajiwezi, anaonekana kuchoka na kwamba baada ya kuzuka ule moto wa Grenfell Tower aliangua kilio. Hiyo ilikuwa mara yake ya tatu kutokwa na machozi katika kipindi cha wiki, kuanzia pale yalipotolewa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Juni 8.

Baadhi ya wabunge wa chama chake wana wasiwasi na msimamo wake kuhusu ule mchakato wa “Brexit”. Miongoni mwa wabunge hao inasemekana kwamba kuna walio tayari kumbwaga May. Kwa hakika, kuna shinikizo kubwa kwa mawaziri na wabunge kuwataka wamuangushe May.

Wabunge wasiopungua darzeni moja wako tayari kuandika barua zisemazo kwamba hawana imani na waziri mkuu. Barua hizo hupelekwa kwenye kamati ya wabunge ijulikayo kama “kamati ya 1922”. Idadi hiyo ikifika 48 basi hapatakuwa na budi ila pafanywe uchaguzi wa ndani ya chama wa kumtafuta kiongozi mwengine.

Hata hivyo, sidhani kama May atakuwa tayari kujiingiza katika mchuano huo. Nasikia kwamba wiki iliyopita, barua ya kutokuwa na imani na May iliachwa bungeni bila ya kutiwa saini; hiyo ikiwa ishara ya azma ya baadhi ya wabunge wa chama cha Conservative wanaompinga May.

Wafuasi wa May, kwa upande wao, wanataka kumnusuru asipinduke kwa kuanzisha mkakati wa kutumia vitisho. Kitisho kikubwa ni cha kuwatisha wabunge wao kwamba wasipomuunga mkono May na pakalazimika kufanywa uchaguzi mkuu mwingine, chama cha Leba kikiongozwa na Jeremy Corbyn kitashinda na kitaunda serikali yenye sera za Kimarx. Hicho ndicho kitisho cha mnadhimu mkuu wa Chama cha Conservative katika bunge.

Hadi sasa tunasikia kwamba kuna wabunge wasiopungua watano ambao wamekuwa wakimsihi waziri wa mambo ya nje, Boris Johnson, ajitokeze wazi kumpinga May na awanie uongozi wa chama chao.

Wabunge wa Conservative wamempa May muda usiozidi wiki mbili aache kujionea huruma, ajikaze na aoneshe kwa vitendo kwamba anaweza kuwa kiongozi madhubuti.

May ana changamoto nyingi na kubwa zinazomkabili. Kwanza, kabisa ni haja ya kupunguza makali ya zile sera zake za kubana matumizi. Tumeona kuwa athari moja ya sera hizo ni lile jumba la Grenfell Tower lililoteketea moto wiki iliyopita. Limeteketea kwa haraka kwa sababu wanaohusika walibana matumizi ya fedha zilizotumiwa kulikarabati jengo hilo. Vifaa vilivyotumiwa vilikuwa duni.

Changamoto nyingine kubwa aliyonayo May na iliyoanza tangu Jumatatu ya wiki hii ni yale mashauriano ya “Brexit. Mchakato huo unaweza pia ukammaliza May, kwani ni mchakato wenye mazongezonge mengi, utadhani ni laana. Ulimuangamiza Cameroon, sasa unamtishia May na huenda baadaye ukakiangamiza chama kizima cha Conservative.

Ukweli ni kwamba kwa sasa serikali ya May inaonesha kwamba haijui inataka iwe na mahusiano ya aina gani na Muungano wa Ulaya. May mwenyewe hajui, mawaziri wake hawajui. Kuna mgawanyiko ndani ya serikali yake, na pia ndani ya nchi nzima, kuhusu mchakato huo.

Share: