Makala/Tahariri

SIMULIZI FUPI YA MAISHA YA MZEE ALI HAJI PANDU

SIMULIZI FUPI YA MAISHA YA MZEE ALI HAJI PANDU NA NAMNA MAALIM SEIF ALIVYOKUA AKIFANYA HARAKATI JELA KAMA VILE YUPO NJE.

Na Bi Zainab.

Mke wa Mzee Ali Haji Pandu (Bi Zainab) leo amewasimulia Vijana wa Vyuo Vikuu walio chini ya JUVICUF maisha ya Mume wake tangia kipindi cha mwanzo wa harakati za kujinasua katika Makucha ya Tanganyika hadi kufikia sasa ambapo Mume wake bado anaendelea kukiunga mkono Chama cha Wananchi CUF ambacho ameanza nacho katika harakati hizo.

Katika simulizi hiyo Bi Zainab amesema kua mwanzo Mume wake huyo alikua Jaji Mkuu wa Zanzibar ambaye alipewa wadhifa huo na Mzee Karume lakini baadae aliamua kuacha kazi hiyo na kuamua kujiunga na harakati. “Nakumbuka siku moja nilimuona mume wangu anakuja nyumbani kwa baiskeli mbovu akitokea kazini jambo ambalo halikua kawaida kwasababu kila siku akirudi kazini alikua analetwa kwa gari. Nilipomuuliza ndipo akaniambia kua ameacha kazi”.

Akisimulia maisha yao Bi Zainab alisema kua Mzee Ali Haji Pandu alikua msiri sana na hakua akimwambia mambo yake anayoyafanya lakini Bi Zainab alikua anajua yote anayoyafanya na kila siku akiingia ndani tu anamwambia kila alilolifanya hadi Mzee Ali Haji Pandu akaona bora tu amwambie maana kila analolifanya kwa siri mke wake huyo analijua. Sababu ya Mzee Ali Haji Pandu kumficha Mke wake ilitokana na hofu kwamba Wanawake hawaaminiki lakini baadae aliamua kumuamini.

Baada ya kujua kua Mume wake aliacha kazi Bi Zainab amesema kua mwanzo alimlilia sana Mume wake aachane na mambo hayo (harakati) lakini baadae aliamua kumuunga mkono. “Siku moja nilimfata Mzee Idrisa Abdul Wakil kipindi hicho Mzee Idrisa ni Speaker wa Baraza la Wawakilishi kumuomba amwambie mume wangu aachane na mambo hayo “. Pia alisema kua “Dr. Salmin Amour aliniambia kua nimwambie mume wangu asijitokeze sana katika siasa na alimtuma kaka yangu ambaye walisoma pamoja nje amwambie baba ili aniambie mimi nimwambie Mume wangu aachane na siasa lakini baba akasema yeye hawezi kumkataza maana yule ni Mume wangu na hata akimkataza Mzee Ali Haji Pandu hawezi kujiunga na CCM”.

Akizungumzia swala la Maalim Seif ndani ya harakati hizo, Bi Zainab alisema kua kulikua na orodha ya Viongozi walioziongoza harakati hizo waliojulikana kwa jina la Front Liners ambao walikua ni Mzee Ali Haji Pandu, Soud Yussuf Mgeni, Mzee Machano, Hamad Rashid, Mzee Shaaban Mloo na Nasor Seif. Orodha hii iliongozwa na Maalim Seif ambaye alikua Jela kipindi hicho lakini alifanya kazi kama vile yupo nje. “Maalim Seif kipindi hicho alikua Jela lakini alikua akifanya kazi as if yupo nje”.

Akifafanua hilo Bi Zainab alisema kua wakati Maalim Seif yupo Jela Mzee Ali Haji Pandu alikua akimwandikia ripoti za sehemu na matukio mbali mbali na kumpelekea Jela kupitia Vijana ambao walikua wanaenda kuzichukua kwa Bi Zainab na kumpa kijana mmoja wa Jela ambaye hakupenda kumtaja jina na yeye huyo kijana alimfikishia Maalim Seif.

Baada ya Maalim Seif kuzipokea, Bi Zainab amesema kua Maalim Seif yeye alikua haandiki ripoti anaandika kitabu kizima kwa kile alichodai kua ripoti za Maalim Seif zilikua ndefu na zenye page nyingi. “Maalim Seif yeye alikua haandiki ripoti anaandika kitabu maana karatasi za ripoti zake zilikua ni nyingi sana”.

Akiendelea kusimulia hali hiyo Bi Zainab alisema Vijana hao aliowaita GO BETWEEN walifanya kazi hiyo mda mrefu huku Mzee Ali Haji Pandu anaendelea na harakati nje na kila anapoenda hata pale anapokwenda London basi akirudi anamuandika ripoti Maalim Seif na yeye Bi Zainab ndie aliekua Organizer wa Vijana hao.”Nakumbuka siku moja Mimi nasafiri kwenda Masomoni na Mzee Ali Haji Pandu nae anasafiri Vijana walikuja kwangu kuchukua mzigo, walipokuja nikawambia kua mimi nasafiri wakashtuka sana na kusema kua sasa tumeshakwama. Tutafanyaje kazi kama wewe hupo?” Bi Zainab amesema kua aliwambia Vijana hao kwamba bado hawajakwama na kusema kwamba kwasababu yeye peke yake ndie aliekua akiwasiliana na yule kijana wa Jela ndio maana Vijana hao walishtushwa na kuondoka kwake lakini alitumia njia nyengine na kazi ikaendelea kama kawaida.

Akisimulia swala la Mashirikiano yake na Wake wa Viongozi wengine Bi Zainab alisema kwamba yeye alikua anaishi na mke mwenzake ambaye walikua wanakaa nyumba moja lakini Mke huyo alikua hajui chochote kinachoendelea kwasababu alikua ni CCM kwa hiyo yeye alikua akifanya kazi kwa karibu sana na Mke wa Maalim Seif Bi Awena na kusema kwamba wakati Maalim Seif anamuacha Mke wake wa mwanzo harakati hizo zilikua bado hazijaanza hivyo Bi Awena ndie aliyeshuhudia mikiki mikiki yote hiyo mwanzo mwisho. Pia Bi Zainab alisema kua alishirikiana pia na Wake wengine kama vile mke wa Mzee Shaaban Mloo, mke wa mzee Machano n.k.

Akisimulia zaidi jambo hilo amesema kwamba wakati wote huo walishirikiana vizuri na Wake wa Viongozi hao lakini mwaka 1989 ndipo waliposhirikiana zaidi baada ya Viongozi wapatao 18 kuekwa ndani wakidaiwa kua ni wakorofi. Hapo ndipo Bi Zainab alipo-arrange mpango wa Wake wote wa Viongozi hao 18 kutoka Pemba na Unguja kwenda Ikulu Dare-es-salaam kuonana na raisi Ali Hassan Mwinyi na kumtaka awaeleze kosa la Waume zao.

Bi Zainab amesema kua baada ya ku-arrange mpango huo, wakati yupo Bagamoyo kimasomo alipewa taarifa iliyomtaka aende Dare-es-salaam ambako wenzake walishafika tangia asubuhi ndipo na yeye akachukua usafiri na kuelekea Dare-es-salaam.

Kabla ya yeye kufika wenzake walipofika Ikulu Dare-es-salaam walikutana na Maafisa wa Usalama (Security Offers)na kuomba wakutanishwe na raisi Ali Hassan Mwinyi lakini bahati mbaya aliekua Mwandishi wa raisi Ali Hassan Mwinyi Mahmoud Ameir Jabir aliwaagiza Maafisa hao wa Usalama kua wawambie Wake hao kwamba kesi ya Waume zao iko Zanzibar na inashughlikiwa Zanzibar kwa hiyo waende kwa raisi wa Zanzibar ambaye alikua ni Idrissa Abdoul Wakili kwa kipindi hicho. Kwa mujibu wa maelezo ya Bi Zainab, huu ulikua ni mpango maalum wa kuwaondosha Wake hao pasi na mafanikio wa yale waliyoyaendea.

Bi Zainab amesema kua baada ya hapo yeye alifunga safari hadi Dare-es-salaam na alipofika akakutana na wenzake na kuwauliza walipofikia. Wao wakamjibu kama walivyoambiwa kuwa kesi itashughulikiwa Zanzibar na kwamba wao wameambiwa warudi Zanzibar. Bi Zainab akawauliza kua “Ina maana kote huko tulikotoka wengine Pemba wengine Unguja halafu tufike hapa tuambiwe hivo tu? Nyinyi ndo mumesharidhika?” Wakajibu kua hawana jengine la kufanya.

Bi Zainab akawambia hapana ni lazima tumuone raisi. “Mimi nikitaka langu siwezi kurudi nyuma na hakuna wa kunirudisha nyuma nikitaka langu, nikawambia ni lazima tumuone raisi kwa nini tusimuone? kwani si ni raisi wetu? kwani si tumempigia kura Wazanzibari?”

Baada ya hapo anasema kila mtu akashindwa kujiamini wengine wakaanza kusema wanaumwa na vichwa wengine presha na wengine wakahoji ni nani atakaezungumza? Bi Zainab akawambia yeye atazungumza wao wanyamaze kimya ndipo hapo wakapandisha kwa raisi.

Wakati wakielekea huko walikutana tena na wale Maafisa wa Usalama na kuwauliza wanaenda wapi? Bi Zainab akawajibu tunataka kumuona raisi, wale Maafisa wa Usalama wakawambia nyinyi si mumeambiwa kua kesi ya Waume zenu ipo Zanzibar muende Zanzibar? Bi Zainab akawajibu sisi shida yetu ni kumuona raisi na hatutoondoka kama hatujamuona raisi na kama munaweza tuuweni sote. Ikabidi wale Maafisa wa Usalama wapige simu na baadae wakaruhusiwa kuonana na raisi.

Siku ya pili yake wakati anaelekea zake Masomoni Bagamoyo Bi Zainab alipokea taarifa kua mume wake ameshaachiwa huru na kwamba tayari ameshafika Zanzibar. Aliposikia hivyo Bi Zainab ikabidi aghairishe kwenda Bagamoyo na badala yake akarudi Zanzibar kwenda kumuona mume wake.

Mwisho Bi Zainabu alimalizia kusimulia simulizi hiyo fupi ya maisha yao hayo na harakati za Ukombozi kwa kusema kwamba anamshkuru Mungu kua hadi leo Maalim Seif hajamuacha mkono Mzee Ali Haji Pandu na hua anaenda mara kwa mara kumjulia hali na anamsaidia kadiri ya uwezo wake na kwa upande wake yeye na Bi Awena bado ni Maswahibu wa karibu sana na kusema kua zamani Maalim Seif alikua akimwita kwa jina lake (Bi Zainab) lakini baada ya kuongoza mapambano hayo Maalim Seif hadi leo akikutana nae anamwita Jeshi. “Mwanzo Maalim Seif alikua akinita kwa jina langu lakini baadae alinibadilisha jina na mpaka sasa akija nyumbani hunita Jeshi na mukienda kuonana nae mwambieni tu Jeshi anakusalimia atakua ameshaelewa”.

FB

Share: