Makala/Tahariri

Sitta na Nambari

Na Salim Said Salim

Lugha ya Kiswahili (ninaamini hata ya Kinyamwezi) inayo misemo, mafumbo na methali inayotoa mafunzo mengi, mbali ya yale anyopata mtu shule, juu ya dunia yetu hii iliojaa ujanja na hadaa. Kwa mfano ipo misemo yenye maneno haya …Siku za mwizi 40, Ukiujua huu nami naujua huu na Ukweli ukidhihiri uwongo hujitenga.

Lakini kwa mwanasheria, mwana siasa na mpenda michezo mwenye kujilabu kuwa mtu wa viwango, Samwel Sitta inaonekana amejitia kwenye kikaango na kujikaanga kama pweza kwa mafuta yake.

Hii inatokana na kushindwa kujifunza maana ya misemo kama hii licha ya kuishi ukanda wa pwani kwa muda mrefu na kuwa karibu na Waswahili wa klabu ya Simba (tokea ikiitwa Sunderland). Badala ya kuthibitika kuwa mtu wa viwango umma sasa unamuona ni kiumbe sio tu asiyekuwa na viwango bali kama aliyepika chakula katika kikaango kilichokuwa na ufa.

Sasa hicho chakula kimemwagika na hakuna anayetaka kukila na badala yake anakaangwa kwa kutumia vibaya mahesabu yaliomalizia nambari sita badala ya tisa. Sitta aljifanya mjuzi wa kucheza na nambari, lakini kilichojitokeza ni kuadhirika juu ya mahesabu ya kura kwa rasimu ya katiba ya Andrew Chenge iliyopiga chenga mapendekezo ya Tume ya Jaji Joseph Warioba iliyotokana na maoni ya wananchi.

Masikini Sitta alifikiria nambari zinamalizikia sita na kufumbia macho kwamba watu wanajuwa kuwa zipo nambari 7,8 na 9. Kama niivyosema zile methali za siku za mwizi 40, ukiujua huu nami naujua huu na ukweli ukidhihiri uwongo hujitenga hali inayoonekana baada ya hicho kilichoitwa kuridhiwa kwa rasimu ya Chenge imedhihirisha uhakika wa mafunzo ya misemo hii.

Lakini kabla sijafafanua zaidi naona labda nieleze juu ya umuhimu wa Sitta na wenzake kuwaelza Watanzania nini kiliwasibu hata wakafikiria wao ndio wajanja na watu wengine ni mbumbumbu?

Au ni jeuri ya chama chao kushika hatamu ndio iliyowapa kibri cha kutaka kuburuza hata waliokufa kwa kutonyesha maajabu ya Bibi …..,mama yake Zitto Kabwe kuwa naye alipiga kura akiwa akaburini.

Ni kweli katika baadhi ya nchi na si ajabu hata Tanzania wapo wanaotumia majina ya watu waliokufa kupiga kura ili kusaidia mgombea au chama chao kupata ushindi. Au tunataka kuambiwa huyu marehemu naye pia alitumika mtandao kupiga kura kwa simu ya mkononi kutoka kaburini.

Taireni Sitta na Samiha Suluhu kwa kuona suluhu ya kupata ridhaa ya kutengeneza katiba mpya ni kumpaChenge uongozi wa kazi ya kuipiga chenga rasimu ya Jaji Warioba. Hapa Sita, Samiha na Chenge aliyejifanya ndio mtemi wa lile Bunge la Katiba wanapaswa kutueleza kama mama yake Zitto alituma ujumbe (SMS) kutoka kaburini, au mwanawe ndiye aliyempiigia kura au nani alipewa jukumu la kumpigia kura huyu marehemu.

Lakini yote sita, sasa nizungumzie la saba na baadaye la nane na la tisa. Hili la saba ni kuonekana kuwa Sitta labda haelewi kuwa baada ya 6 zipo nambari nyengine ambazo ni kubwa zaidi ziliolizidi jina lake na kwahivyo wapo atambue kuwa wapo pia waliomzidi kwa maarifa na ujanja wa mahesabu.

Laiti kama angelikuwa mwerevu basi angelitilia maanani tahadhari aliopea mapema juu ya hatari ya kucheza nambari kwani wengi wanaofanya hivyo hujikuta katika hali ya hatari au heshima yao kupata athari.

Sasa Sitta baada ya kupuuza ule ushauri wa kutochezea tunaona kuwa siku za mwiizi baadhi ya wakati hazitimii hata 40 kama habri za hivi karibuni zinayoonyesha. Hapo awali Sitta na Chenge waliona walifanikiwa kupiga chenga kinachotakiwa na umma kwa kucheza na nambari, lakini sasa nambari zinawapiga wao chenga.

Miaka iliopita wakati wa ile iliojulikana kama sakata ya kuchafuka hali ya hewa ya kisiasa iliopelekea kutimuliwa Rais wa pili wa Zanziar, Sheikh Aboud Jumbe tulisikia mchezo wa nambari. Wapo aliosema moja na moja mili na wengine wakasema moja na moja ni tatu. Lakii Sitta na wenzake katika Bunge la Katiba wamekuja na hesabu mpya. Nayoni moja na zero( mtu aliyekuwakaburini( ni mbili. Makubwa haya.

Nambari nane ni hili la Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Ali Haji Ambar ( sio nambari). Huyu bwana ameeleza kwamba hajapiga kura na kwamba tokea tarehe 5 Agosti hadi siku ya kupiga kura hakuwemo kwenye kikao cha Bunge la Katiba.

Lakini katika huo mchezo wa nambari tumeambiwa jina lake katika orodha ya wapiga kura ni nambari 209 na katika orodha ya wapiga kura ni nambari 39. Jee naye huyu kura yake ilipigwa kwa njia gani? Au yupo mtu aliota kwa niaba yake kuwa angelisema “Ndiyo”? Hili naloni suala zito ambalo umma unapaswa kuelezwa ilikuaje.

Sasa nije katika hiyo nambari 9 ambayo Sitta aliisahau kwa kudhani mwisho wa hesabu ni 6. Hili ni la wale waliokwenda kufanya ibada ya Hijja. Taarifa zinaeleza kuwa baadhi yao walikuwa waliamua kuacha mambo ya duni – mapenzi, siasa,micezhezona mengine- pembenei na kujihusisha na kumuabudu Mola wao na kwahivyo hawakuwa na habai kabisa na suala la kupiga kura.

Jee hizi kura zao zilipigwa vipi au yupo mtu ambaye wakati akisali, msikitini au kanisani, alipata maagizo kichwani kutoka Mecca kwamba na watu hawa walikuwa wanapiga kura ya Ndiyo na kumuomba Mola ajaaliye rasimu ya Katiba ya Sitta, Samiha na Chenge ipite?

Masuala haya niliyoyaleza hayatoi ishara yoyote ile isipokuwa ulipita mchezo mchafu wakuvunja sheria katika kutengeneza sheria mama ya nchi. Hii ni hatari ka sababu kama sheria mama inatengenezwa kwa kuvunja sheria nini utarajie katika kuisimamia na kuitekeleza hio sheria mama

Tuache kujidanganya kwamba rasimu iliyopendekezwa na Bunge la Sitta sio tu imekosa rodhaa ya wananchi, bali pia haikupata ridhaa ya hao waliokuwa ndani ya Bunge hilo. Badala yake ridhaa imetokana na kuchezea nambari.

Kama hili sio kwlei basi hizi dosari zilizojitokeza za kura kupigwa kutoka kaburini, kuhesabiwa kura ya mtu ambaye amethibitisha hakupiga kura na kizaazaa cha kuwapigisha kura waliokuwa katika ibada ya Hijja wakati hawakufanya hivyo kutolewe maelezo.

Kwa Sitta na kundi lake kutoa taarifa tu haitoshi, bali waruhusu vyombo vya habari kama jicho la umma kuwahoji ili kupata ufafanuzi na sio kutoa taarifa na wasitoe nafasi ya kuulizwa masuali. Ni vyema kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein wakaitafakari hali hii na kukataa kudanganywa na maelezo ya nambari ili kujiimarishia heshima na imani ambayo Watanzania waliokuwa nayo kwao katika suala la utawala wa kidemokrasia, haki na sheria.

Kwa kuhitimisha kwa kutumia hio sufuri iliojumuishwa na moja Dodoma hivi karini kusomeka kama ni mbili mimi ninaziunganisha 1 na 0 kusomeka kama 10 kwa kuwaomba wanachama wa CCM kuwa na hadharina Sitta ambaye anasemekana kuinyatia tiketi ya chama chao kuwa mgomea Urais katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Mtu ambaye anajaribu kuchezea nambari tena bila ya kuwa na ujuzi nazo kama atapewa hatammu ya kuiongoza nchi anaweza kuendelezamchezo huowa nambari ambao matokeo yake huwa sio mazuri kwa taifa.

Lakini ni vizuri kwa wanachama wa vyama vyote vya siasa kwa ujumla kuwa macho kuhakikisha na wao hawasimamishi katika uchaguzi mkuu ujao wagombea ambao nao wanaweza kuchezea nambari kwani mchezo wa nambari ni wa hatari.

Share: