Makala/Tahariri

SMZ – HAYA HAYATUFAI, TUYAWACHE!

Kwa binaadamu mwenye akili timamu na fikra za kimaendeleo hafanyi jambo lolote bila ya kulifanyia tathmini na kujua kuwa jambo hilo lina manufaa au halina. Na kwa yoyote anayefanya bila kuangalia haya, ama hupata hasara kubwa au huwasababishia wengine hasara kubwa kwa kufanya kwake hivyo.

Kwa muda mrefu sasa, Serikali imejenga mtiririko wa mambo ambayo yameshakuwa ni sehemu ya itifaki na utamaduni wa Taifa ijapokuwa mambo hayo hayana faida tena yoyote kwa wanaofanyiwa, wananchi, na taifa kwa ujumla, badala ya hasara. Mambo kama hayo kwa lugha ya kiungwana tunaomba na kuishauri Serikali ifikie dakika, saa, na siku iyawache na iunde mengine yenye tija nasi. Hebu tuanze kuchambua moja moja.

Kitendo cha Viongozi wanapotembelea miji na wilaya za Zanzibar kufanya mikutano ya hadhara kwa kujumuisha hadhira ya wanafunzi wa Shule za Umma yaani za Serikali hakifai. Na kitendo hiki kwa Wenzetu wa Bara kilipigiwa kelele sana wakati wa Mwalimu Nyerere, ambapo Waziri wa Elimu wakati huo, 1978 kwenda mbele, Bi Tabitha Siwale alikataza sana jambo hili. Likapunguwa kule bara lakini Zanzibar awali leo! Mkoko ndio kwanza unaalika mauwa!

Hapa kwetu, wiki ya masomo ina siku Tano kwa nne, maana ijumaa ni nusu siku. Isitoshe, ikitokea Waziri au kiongozi wa nchi kutembelea eneo hilo wanafunzi hutolewa na kupangwa njiani tangu asubuhi mpaka jioni wakipiga kofi. Hakuna kusoma wala nini hapo, kisha tukifeli tunalaumu NECTA, kelele haziishi lakini, kikulacho kinguoni mwako.

Imeshakuwa utamaduni kwa watoto wetu wa kinyonge kila siku kutolewa madarsani kupokea Viongozi na kuishia patupu bila kusoma. Utamaduni huu ni wa kionevu dhidi ya wanafunzi wa Kinyonge wasiodiriki kusoma shule za kulipia kama wasomeshwazo watoto wa viongozi ambao huwatoa watoto wetu kuwapigia kofi huku watoto wao wakisoma nje ya nchi au shule binafsi nchini. Hii si haki.

Baya zaidi, mbio za Mwenge ambazo mimi binafsi sioni umuhimu wake, wala sioni nchi yoyote iliyoendelea ikitumia mwaka nzima kukimbiza moto kwa gharama za mabilioni ya walipa kodi. Watoto wetu na wafanya kazi wa wizara mbali mbali, hutolewa makazini na kuanikwa barabarani kuusubiri mwenge huku shuhuli muhimu za masomo na kazi za maendeleo zikisimama kwa masaa na masiku mwaka nzima.

Mbio za mwenge hazina faida yoyote kwa taifa hili. Na kama serikali yaona zina faida, basi nawakimbize mwenge wenyewe wakipokezana mpaka wamalize mikoa yote 26 ya nchi bila kushirikisha wanafunzi wetu wa kinyonge hasa hapa Zanzibar. Kwa jinsi Serikali yetu inavyotukuza shuhuli zisizo faida na taifa kama huu Mwenge, kuna watu muhimu katika utumishi wa Umma hapa Zanzibar wametolewa kazini kwa kukosa kutii amri kama hizi.

Bwana Salim Suleiman, ana Masters ya sayansi, ambaye alikuwa mwalimu Mkuu wa Fidel Castro, alinusurika chupuchupu kufukuzwa kazi baada ya kuusubiri mwenge kwa masaa, na kwa vile bwana huyu ni mcha mungu mno, wakati wa sala ya laasiri ulipofika, yeye ni imamu pale, akaingia msikitini mwenge haujafika tangu saa sita mchana walipousubiri. Mambo ya Mungu, kupiga takbiratul-ihraam tu, mwenge huo! Hapana mtu wa kuupokea nje! Siku chache baadae akapata tetesi kuwa atafukuzwa kazi, akaachia ngazi bila kutoa taarifa. Akawapiga bao la kisigino. Yuko bara ambako sasa ni mkemia sijui vile, wa dawa za mifugo kule! Mwenge huo!

Dokta Ayub Khamis, ana Masters ya Utalii ya UK, alikuwa Afisa mdahamini wa Kamisheni ya Utalii Pemba. Licha ya kutiliwa fitina na jirani yake pale Wete aliekuwa na nafasi kama yake Wizara ya Fedha wakati huo, kwa tuhuma za kuwa ni CUF, pamoja na fitina za msaidizi wake ambae ndie alieshika wadhifa wake sasa, Dokta Ayubu alifukuzwa kwa kutokwenda kumpokea mmoja kati ya viongozi pale Uwanja wa ndege, kwani alikuwa na shuhuli muhimu pale ofisini siku hio. Kafukuzwa!

Sasa pima wewe hapo, kuna maendeleo hapo katika nchi kama hio? Ikiwa Serikali inaweza kufukuzwa nguvu kazi muhimu kama hizo kwa jambo la kupita wala lisilo na mchango wowte katika pato la taifa wala maendeleo ya nchi, akili kweli hizo? Hivi niambie kumopkea kiongozi uwanja wa ndege kungeliingizia nini taifa? Na kutompokea kungelipunguzia nini taifa? Mwenge je? Ndivyo tulivyo!

La pili, suali la kuwatoa wanafunzi madarasani wakati wa masomo kwenda kuimba, kuigiza kwa ajili ya Elimu bila malipo halina faida zaidi ya kumuharibia maisha mtoto wa mnyonge. Watoto wetu tangu mwanzo wa mwaka huimbishwa, na kupelekwa huku na kule eti Elimu bila malipo. Sherehe hizi na zile za Mapinduzi hata kama zina umhuhimu kwa viongozi ni vyema zisishirikishe wanafunzi wetu wa kinyonge. Kama ni suali la michezo Jumamosi ni siku nzuri kwa michezo naifanywe rasmi kuwa hivyo na sio siku za masomo.

Zaidi ya hayo watoto wetu katika skuli za Serikali wamekuwa watumwa. Mara huteka maji, hubeba mawe, matofali, huchimba udongo, huwapikia walimu, huwasuka na hata kuwapaka hina katika baadhi ya maskuli. Haya si mambo ya maana hata kidogo. Sisi kama wazazi hatuwapeleki watoto wetu shule kusuka walimu wao au kuteka maji na kupikia wageni. Mnatuonea na kuwadhulumu watoto wetu kwa sababu hatuna uwezo wa kuwasomesha nje ya nchi wala shule za kulipia. Naomba, na hili kwa niaba ya wazazi lifutwe na likomeshwe.

La mwisho litawahusu viongozi. Kuna tabia viongozi wetu kukimbilia mambo ambayo hata ukiyachunguza hayana uzito wa kitaifa wala hayafanani kuwa yana umuhimu wa kufanywa na viongozi wakuu wa nchi. Kwa mfano, akija msanii mkubwa hapa Rais huvunja kazi kwenda kumpokea. Kuna umuhimu gani? Hili moja.

Viongozi wetu ni wepesi kukimbilia kuweka mawe ya msingi yawe ya vyuo, mtaro, tuta la mboga ya viazi, banda la ushirika wa kufuga kuku na mengineyo chini ya hayo. Mimi najua kwanini viongozi wetu hukimbilia kujiwekea mawe ya msingi. Ni kwa sababu hutaka wabakishe kumbukumbu yao kwa watu wakiondoka madarakani kwani bila hivyo huwa hawana kilezea chengine cha kuonesha jambo la kudumu litalowafanya wakumbukwe zaidi ya hayo mawe ya msingi. Lakini suali linabaki je, lina faida gani kwa kiongozi kuacha kazi kubwa muhimu kwa jambo kama hili ambalo hata katibu kata angeweza kulifanya?

Naiomba Serikali ibadilike. Nchi za wenzetu zimepiga hatua kwa kasi kwa sababu ya kuacha itikadi zilizopitiwa ni wakati na zisizoleta maendeleo kwa taifa. Zanzibar kuna mengi ya kufanywa zaidi ya haya ya kutaka kutukuzwa na kuabudiwa na wanachi kwa kila kiongozi wa chama na Serikali ajapo madarakani. Tuachane na mila na tamaduni hizi na tuunge nguvu kujenga taifa letu.
Natoa hoja!

Tagsslider
Share: