Makala/Tahariri

Tahadharini na utumwa mpya wa aina hii ndugu zanguni!

Na: Omar Mussa Msaga

Ndugu Waislamu na wapenda amani wote wa Afrika Mashariki.

Naamini mtakubaliana nami kuwa kwa kiasi kikubwa maisha yamekuwa magumu sana huku kwetu: Tanzania, Zanzibar na Kenya.

Ugumu wa hali za maisha ni mkubwa kiasi kwamba kila mtu ameupokea vile anavyohisi yeye au kwa mujibu wa nafsi yake inavyomwamrisha afanye.

Katika kupambana na ugumu wa maisha, wako walioamua kuomba. Wapo walioamua kukimbia makwao na kwenda nje kutafuta. Wamo walioamua kufanya kazi za majumbani au sehemu nyengine. Pia wako katika wazazi walioamua kuwatoa watoto wao ili wasaidiwe kulea. Na mwisho, wapo wanakwenda bara Arabu kufanya kazi za ndani.

Katika wasaa huu nataka nitoe tahadhari katika mambo au nukta mbili muhimu: Kutoa watoto kwa ajili ya kulelewa na watu wasio kuwa wana familia na la pili, kuchuuza watu hasa hasa wasichana, kwenda nchi za Kiarabu kufanyishwa kazi majumbani.

Nikianza na nukta ya kwanza. Kumekuwa na utamaduni wa watu wanaojiweza, hasa hasa kutoka mijini kwenda maeneo ya mashamba kuchukua watoto kwa kisingizio cha kuja kuwalea mijini na kuwapunguzia mzigo wazazi wao.

Maeneo ambayo watu wengi huyatumia kuwapata watoto hao kwa Unguja ni Tumbatu, Makunduchi, Nungwi na maeneo mengine ya shamba ambayo hali a maisha ni ngumu kwa baadhi ya watu.

Ama kwa Pemba sehemu kubwa inayotumiwa sana kwa kuwapata watoto hawa ambao mwisho huishia kuteswa na kufanywa watumwa majumbani mwa watu ilhali wakiwa na umri mdogo ni Micheweni, Sumba mjini, Kiuyu Mbuyuni, Maziwa Ngombe, Mjini Wingwi, Makangale, Tondooni, Fundo, Gando na Ukunjwi.

Natoa tahadhari kwa wazazi na wahusika wote, msikubali kutoa watoto wenu kwa kisingizio wataenda huko kulelewa. Sio kweli. Watoto wenu hawa wanaishia kuteswa na kufanywa watumishi wa ndani wakiwa na umri mdogo sana. Ni bora kupata shida na mtoto wako kuliko kumpa mtu akusaidie malezi. Chonde chonde, kama unampenda mwanao kaa naye ule naye unachokipata usimpe mtu akamfanya mtumwa na kumnyima haki zake za msingi.

Jambo la pili, muhimu zaidi nalo, natahadharisha kuwa kuna watu wanaotangaza kutafuta watu wa kufanya kazi nzhi za falme za Kiarabu kama vile Saudia, Misri na nyenginezo. Watu hao angalabu ni wasichana kati ya miaka 18-40 ambao hufanyiwa safari kwenda kutumika huko kwa mkataba wa miaka miwili.

Watu hawa wakifika huko, hufanyishwa kazi za ndani. Sio mbaya. Lakini kwa hakika, nasema kwa kuwa shuhuda, kazi hizi ni zaidi ya utumwa na udhalilifu uliopitiliza. Ukiachilia kufanyishwa kazi muda wote. Kulala saa sita usiku kuamka saa kumi na moja alfajiri. Kuna kifungo cha ndani kwa takribani miaka yote miwili. Pia mateso na masuupio yanayoambatana na unyanyasaji wa kijinsia, ukabila na ubaguzi wa daraja la kwanza ni sehemu ya mateso wayapatayo watumishi huko.

Hivi karibuni, tumeona kijana wa kikenya aliyepigwa mpaka kufa na watumishi wake wa ndani na hakuna lililofanyika. Mkataba wa waajiri hawa unakuwa halali kabla hujaingia mikononi mwao tu, ukifika huko hakuna ubalozi unaoweza kukutetea wala mtu yeyote anayeweza kukuombea. Unakuwa mtumwa wa kileo (huwi na minyororo mkononi lakini huwi na uhuru wala haki yoyote ya msingi).

Nawaomba, ndugu zangu, tuweze roho na shida zetu. Tusiwapeleke ndugu zetu kwenye nakama zaidi kwa kuwarubuni kuwa kwenda arabuni kufanyishwa kazi watafanikiwa kimaisha. Kwa kweli hali ni ngumu kuliko maelezo. Pigeni vita aina hii ya utumwa kwa kuwanusuru ndugu zenu kwenda huko kufanya kazi. Hakuna maisha bora kitu, ni utumwa tu.

Shukran

Share: