Makala/Tahariri

Tanganyika inahofu ya nini kuvunjika kwa Muungano ?

Na,B.OLE,
Nianze kwa kuuliza suali ili na mimi nipate kuelimika, kwani Wahenga walinena kwamba ”kuuliza sio ujinga” pia uliza ili upate uweledi. Hivi Tanganyika wanahofia nini iwapo Muungano wao kati ya Zanzibar na Tanganyika utavunjika ? Shaka na huzuni zimetawala hasa kwa Viongozi wa Serikali na baadhi ya vikundi fulani kuhusu kuvunjika kwa Muungano huu,tatizo lao ni kitu gani? Mbona inaonesha dhahiri kama vile kuna siri ambayo  imeshaanza kujitokeza kwa wale waumini wa Muungano huu,huku wakiwa hawapendi siri hio kujulikana na wote.

Imekuwa ni gumzo kubwa hivi sasa kwa upande wa Tanganyika kwa kila mtu kujadili kuhusu kuvunjika kwa Muungano na huku baadhi ya viongozi wa Serikali pamoja na Wananchi husasani kutoka upande wa Tanganyika,magazeti na vyombo vya habari wakilalamika na kulia lia kuvunjika kwa Muungano huu kama vile inataka kuvunjwa nguzo ya dini.Naamini ipo haja ya kutueleza hofu yao, ili na sisi ambao sio waumini wa Muungano tuweze kusikiliza hoja zao kama ni za msingi au la.

Hapa napata wasi wasi mkubwa sana ,kwa nini Tanganyika wang’ang’anie Muungano huu na Zanzibar kwa nguvu zote,na wasipiganie sana kwenye Muungano wa Afrika Mashariki na Kati kama kweli wao ni waumini na wanaupenda Muungano na udugu ? Hapo ni dhahiri kwamba Watanganyika kwa kushirikiana na baadhi ya Wahafidhina akina Seif Idd na Seif Khatib wana ajenda ya siri ya kuifanya Zanzibar kuwa ni mkoa wao.Watanganyika wanaumia sana wakisikia Wazanzibar wanazungumzia ajenda ya kuwa na uhuru kamili wa Nchi yao.Hii nikuona kwamba maslahi yao yanaanza kutoweka nahisi hii ndio sababu kubwa mojawapo ya vilio vyao vya kinafiki.

Mimi nathubutu kusema kwamba kwa yeyote yule ambae ana mawazo kama hayo basi ni muflisi wa nafsi yake na pia ni vyema akapata ushauri wa madokta kwa sababu inawezekana kwamba wahusika wana matatizo ya kisaikolojia.Napenda kuwafahamisha kwamba Zanzibar itabakia kuwa Zanzibar na wala wenye mawazo na uchu wa kufikiria kwamba iko siku Zanzibar itakuwa ni sehemu ya Tanganyika  au sio Nchi hilo walisahau na waondowe kwenye akili zao,hilo ni jambo ambalo haliwezikani na wala halitowezekana katika karne hii.

Kama leo kuna Wasomi,Maprofesa na wachambuzi wa mambo wanaojipumbaza na kushindwa kuelewa ukweli halisi basi nawaomba wasituletee pumba zao,ikiwa wanashindwa kuelewa kwamba Zanzibar ni nchi na ndio maana pakapatikana Muungano, kwani hata mimi ambae sikupata elimu hata ya darasa la pili, basi naelewa na nafahamu kwamba siku zote unapozungumza Muungano wa kitu maanake ni kitu zaidi ya kimoja,sasa nashangaa kuona hawa wasomi wakubwa wanashindwa kulielewa hilo,hivi kweli bongo zao zinafanya kazi.

Tokea enzi na dahari, Zanzibar ilikuwa inajitegemea wenyewe sasa viereje hii leo Watanganyika waripuke na waone kwamba Muungano huu wa udanganyifu wao ndio waungu watu na ukivunjika watu wote watakufa na njaa na baadae watakwenda motoni ? wacheni pumba zenu,tumechoka kutawaliwa na weusi wenzetu,Tanganyika ni koloni kuliko hao Wazungu waliopita kwa jinsi wanavyotunyanyasa Wazanzibar,hili lazima lifikie mwisho wake, Maprofesa na Madokta hili lazima mulifahamu tumechoka na propaganda zenu.

Fikra za Julius Nyerere na ukachero wake wa kutumikia Mabwana zake haziwezi kututawala daima Wazanzibar.Yeye alikuja akaikuta Zanzibar na baada ya madhila yote ameondoka na ameiwacha Zanzibar ingawa iko taabani lakini bado ipo na itaendelea kuwepo hilo Watanganyika mulifahamu.Sisi Wazanzibar tunajivunia Uzanzibar wetu na nilazima uzanzibar uje mwanzo kwani ndio fahari yetu.Na nyinyi sio vibaya mukajivunia Utanganyika wenu hakuna sababu za kuukataa,hiyo ndio asili yenu.

Hivi imekuwa chokochoko haishi,oh’ mara Muungano ukivunjika tutawahamisha Bara, mara Wazanzibar watapigana wenyewe kwa wenyewe ,watashindwa kujiendesha,sisi tunawabeba watakosa mbatata na upuuzi kibao hivi Zanzibar imeundwa jana huko nyuma haikuwepo ? Zote hizo ni kelele za mfa maji,Wazanzibar tuko imara hatuko tayari kusikiliza kasumba za Watanganyika ”any more”.Ukombozi wa Zanzibar ni suala ambalo halina mjadala miongoni mwa Wazanzibar.Tutaendelea kupigania Nchi yetu kwa bei yeyote ile mpaka mwisho wa tone la damu yetu.

Share: