Makala/Tahariri

Uamsho ni rehema ilioteremshiwa ASP na CCM–Zanzibar Kwanini waipiga mabomu ?

Na Laila Abdullah,

Ni ukweli usiokanushika wa Historia ya miaka 48 ya Mapinduzi na Muungano, kwamba Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) na baadae CCM –Tawi la Zanzibar, pamoja na viongozi wake wote walioshika hatamu tangu 1964, ndio wenye JUKUMU la Msiba ulioiangukia Zanzibar. ASP kamwe haiwezi wala haipaswi kuvitupia lawama vyama vyengine vya kisiasa kuhusu kusababisha msiba huo.

ASP na baadae CCM (Zanzibar) na Viongozi wake wote walishika hatamu na mpini kuamua hatima ya Zanzibar, ndio walioshika mpini chini ya biramu la “MAPINDUZI DAIMA”. Hatamu na Mpini huo hawakutaka kuziachia au kuwaponyoka tena kwa kila hali hadi hii leo.

Msiba gani huo?
Ni Msiba wa Zanzibar kupoteza Uhuru wake na Mamlaka yake (Soveregnity) kwa Tanganyika iliojibatiza jina la Tanzania . Matokeo yake kuanzia April 26,1964 , ni kuona historia ya miaka 2000 ya dola la Zenj kuanzia (City State)ikianza kuzikwa kabisa hatua kwa hatua.Mjadala wa sasa wa Katiba mpya ambao awali ulikataza maoni juu ya Muungano “mtakatifu”, unalenga kuizika kabisa dola ya Zanzibar hapo 2014.

Ni chini ya usimamizi wa Afro-Shirazi Party ndipo:
a) Zanzibar ilipoteza KITI chake Katika Umoja wa Mataifa 1964-
b) Zanzibar imepoteza Umashuhuri wake katika ramani ya dunia-
c)Zumari leo likipulizwa Zanzibar,hakuna tena achezae mrima-
d)Zanzibar,haiwezi kufunga Mikataba ya Mikopo na wafadhili wa Kimataifa bila ya ruhusa ya Dodoma-
e)Zanzibar ilibidi kujitoa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) licha ya kuwa ndio iliokuwa Mecca ya Afrika ya Mashariki katika kueneza uislamu-
f)Hata hodi-hodi za Zanzibar kujiunga na Shirikisho la mpira Ulimwenguni (FIFA), hazikufua dafu.
g) Marais wa Zanzibar wanachaguliwa na kuidhinishwa DODOMA kama tulivyoona kisa cha Dr.Amani Karume na Dr.Gharib Bilal.

Kwa ufupi, ni dhahiri-shahiri kuwa,chini ya UONGOZI wa ASP na baadae CCM-Zanzibar, visiwa vyetu vimepoteza SAUTI yake ndani na nje ya Zanzibar .Hali hii ya kufadhahisha, yafaa kuungama hatahivyo, haikuridhiwa na viongozi wote wa afro-shirazi party na baadae wa CCM-Zanzibar .Walipotanabahi na kun’gamua madhambi walioifanyia nchi yao, walijaribu kurekebisha au kugeuza mkondo,lakini bila ya mafanikio.

Mzee Karume alijaribu wakati wa utawala wake wa miaka 8 ulioanzia Januari 12,1964 hadi kuuwawa kwake April 7, 1972 kuikwamua Zanzibar kutoka makucha ya “MUUNGANO-KOTI”bila kudiriki kulivua.Rais Jumbe,mfuasi wake madarakani, nae alijaribu 1984 na kuangushwa Dodoma-lilikochimbwa KABURI la kuizika dola ya Zanzibar na hata viongozi wake.

Commandoo Dr.Salmin Amour,alitumbua macho huku nae KIBIRITI chake KIKITIKISWA alipolazimishwa kujitoa OIC (Jumuiya ya Nchi za Kiislamu). Mwalimu Nyerere aliukomea mlango wa nyuma na wa mbele wa OIC mpaka hii leo wakati nchi ambayo inapinga UDINI,ni rukhsa kuwa na usuhuba wa kibalozi na VATICAN na hata kulitambua dola la Wakristo wa Nigeria ya Mashariki (BIAFRA) walilojaribu kuunda miaka ya 1970.

Seif Shariff na wenzake wakiwa ndani ya CCM walipotaka kufuata NYAYO za Rais Jumbe, na kutetea masilahi ya Zanzbar,walikiona kilichomtoa kanga manyoya walipotimuliwa nje ya CCM Dodoma.

Matokeo yake : Yeyote Yule anaebisha sera za CCM-DODOMA, mfano walivyofanya hivi punde akina Mzee Hassan Nasoro Moyo na Mansouri Himidi kuiweka nchi yao ya Zanzibar kwanza na sera za chama nyuma, SAUTI ZA “MASULTANI WA DODOMA NA MABALOZI WAO waliopo VISIWANI ZANZIBAR NA PEMBA”, zinamkemea. Eti wanakiuka sera ya chama ya serikali 2 kwendea moja ? Ni dhahiri uwepo wa serikali 3 unazuwia sera ya serikali mbili kwendea moja. USIA ULIOACHIWA CCM NA BABA WA TAIFA. Ndipo Mwalimu alipowakemea akina Kikwete na wenzake G-55 walipodai serikali ya Tanganyika.

Hatua walizochukua viongozi hao wote wa Afro-Shirazi party au CCM –Zanzibar, kumvika paka kengele, hazijaiokoa Zanzibar .Na wapi viongozi wa sasa wa CCM walioshika mpini na hatamu katika serikali ya umoja wa kitaifa- akina Sheni na Balozi Seif Idi, wanakoikokota Zanzibar huku wakitetea sera ya chama ya serikali 2 , ni siri yao wenyewe. Mzalendo yeyote wa Zanzibar anaekula kiapo huku ameshika msahafu kuitetea na kuilinda Zanzibar,hawezi kamwe kuchangia mazishi yake makaburini dodoma.

Ni jambo la wazi kabisa viongozi hawa wa CCM , bila ya ridhaa ya Dodoma, wasingeshika hatamu tangu chamani hata serikalini.Vilio vya hivi punde za kuwaajibisha akina Mzee Moyo na kijana Mansouri, ni ushahidi wa hayo.Idhini ya wazanzibari, yadhihirika hawaihitaji na ndio maana wahafidhina ndani ya CCM –Zanzibar na bara ,wanatetea sera za chama na sio nchi yao (Zanzibar).Kuibuka kwa jumuiya ya kiislamu ya muamsho na kudai haki na mamlaka ya Zanzibar,kwa hivyo, ni neema ilioteremshiwa viongozi wa sasa na wa zamani wa ASP-CCM (Zanzibar) na mwenye enzi Mungu.

Ni jahazi la safina walioletewa kulipanda kuwavusha salama na dharuba za kisiwa cha chumbe na mwishoe kujikosha na laana za kuja kulitosa kabisa dola la Zanzibar.kwamba kwani historia itakuja kuandika kuwa (ASP) ndicho chama kilichoiongoza Zanzibar chini ya biramu la “mapinduzi daima” kutoweka katika ramani ya dunia.

Viongozi wa jumuiya ya UAMSHO- akina Amir Msellem;Darid na zan ,wamenadi hadharani,tena dhahiri-shahiri kuwa , hawataki madaraka! .
Watakacho ni kuwarejeshea VIONGOZI wa Zanzibar hadhi yao,kuirejeshea Zanzibar na WaZanzibari UHURU wao na MAMLAKA yao na kuwafanya waZanzibari wote wa Zanzibar na Pemba wapumuwe.

Kwanini basi wanapigwa mabomu hata misikitini?
Kile viongozi wa CCM-ZANZIBAR isipokuwa wachache kama Mzee Moyo na Mansour , wasichothubutu kudai kwa nchi yao ya Zanzibar,UAMSHO wanakidai,tena bila ya hofu,woga na kutetereka. wamejitoa mhanga kusafisha madhambi ya miaka 48 ya viongozi wa ASP na CCM-Zanzibar, waliofanya ama kwa kupenda au kwa kulazimishwa .
Kwanini basi neema hii ilioteremshiwa ASP na CCM-Zanzibar na mwenye enzi mungu,hawaipokei mikono miwili na badala yake waipiga mabomu ? je, chama bora kuliko Zanzibar ?

Tagsslider
Share: