Makala/Tahariri

Uharibifu wa mazingira visiwani Zanzibar

By Sakim Said Salim

Kwa mara nyingine tena zimesikika habari za uharibifu wa mazingira ya bahari Zanzibar, kiasi cha kusababisha maji ya chumvi yanayotoka baharini kusogolea mashamba ya mazao katika vijiji viliopo jirani na pwani.

Taarifa za karibuni zimeleza kwamba baada ya mvua kubwa za hivi karibuni, mabonde ya mpunga katika baadhi ya vijiji vilivyopo kisiwani Pemba, yameingia maji ya chumvi na kusababisha uharibifu wa mazao hayo.

Hali hii inanikumbusha mwaka 1976 nilipokuwa nchini Ghana nikifanya kazi katika gazeti la Serikali la Daily Graphic kwa mwaka mmoja, ambako niliweza kutembelea karibu kila pembe ya nchi hii ya Afrika Magharibi.

Miongoni mwa eneo nililotembelea ni Mkoa wa Volta na miongoi mwa vijiji nilivyotembelea ni cha Keta, kwenye kijiji hicho nilivutiwa sana kwa vile mandhari yake ilifanana kwa kiasi fulani na vijiji viliopo pembezoni mwa bahari vya Zanzibar kutokana na kuwa na minazi na miembe.

Nilipofika pwani nikiwa na mwandishi mwenzangu Elizabeth Ohene, ambaye baadaye alikuja kuwa mwandishi maarufu wa BBC, nilikuta mitumbwi, ngalawa na vidau kama vinavyotumiwa na wavuvi wa Zanzibar, Bagamoyo, Mafia, Dar es Salaam, Mtwara, Lndi na na maeneo mengi ya ukanda wa pwani na sehemu za maziwa.

Hapo nikakutana na na mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kofi Agyeman ambaye alinielezea historia ya eneo hilo liliokuwa na watu wapatao 5,000.

Nilishtuka aliponionyesha ngalawa moja iliokuwa karibu mita 400 kutoka ufukweni kwamba pale ndipo ilikuwapo nyumba aliyozaliwa na nyingine nyingi, lakini takriban miaka 10 iliyopita walilazimika kuhama kutokana na bahari kusogea zaidi ufukweni.

Majengo mengine yaliyomezwa na maji ya bahari ni pamoja na maduka, shule na kiwanda kidogo cha kutengeneza mafuta ya nazi.

Watu wa hifadhi ya mazingira walinieleza baadaye kuwa bahari ilikula zaidi ya mita 400 za ardhi na ilikuwa inasogea kwa wastani wa kati ya futi tatu hadi tano kwa mwaka.

Mzee Agyeman aliniambia:” In Accra they chop the country small small and here the sea is chopping our land small small”, yaani kule Accra, mji mkuu wa Ghana wakubwa walikuwa wanaifisadi nchi kidogo kidogo na hapa bahari inakula ardhi yetu pole pole.

Nilipomwambia lakini na awao walikuwa wanawamaliza samaki baharini kidogo kidogo, yule mzee alicheka sana huku nikiona mapengo ya meno yake matatu ya mbele yaliyopotea.

Mzee huyu aliniambia:” You joke ooh…situation serious, but only God cares and not those driving big cars and enjoying fufu with big fish in Accra and Kumasi”, yaani wewe unafanya mzaha…hali ni mbaya, lakini Mungu ndiye anayejali na sio wale anaoendesha magari makubwa Accra na Kumasi huku wakila fufu ( chakula kama ugali mwepesi uliosongwa kwa mahindi,muhogo na kiai kikuu).

Siku hizi kila ninapofika katika vijiji vingi vilivyopo kwenye ufukwe wa bahari Unguja na Pemba au katika visiwa vidogo vidogo hukumbuka niliyoyaona Keta kwa nmna bahari inavyokula ardhi.

Karibu miaka 10 iliyopita tulielezwa kuwa kisiwa Panza kilichopo Pemba kinaliwa vibaya sana na bahari na hali katika vijiji vingi kama Nungwi na Jambiani, licha ya kujaribu kujenga uzio wa matofali makubwa hali ni mbaya na kila siku ngalawa za wavuvi zinasogea juu zaidi kutokana na maji ya bahari kupanda juu.

Hivi sasa mashamba katika katika vijiji vingi viliopo kando kando ya bahari kusini Unguja yanatarajiwa kutoweka kutokana na maji ya bahari kupenya na kuingia katika maeneo ya kilimo na kuharibu mazao.

Sasa tunasikia hatari kama hio katika mabonde ya mpunga ya vijiji vya kisiwani Pemba. Hii ni hatari kubwa.

Hapana ubishi kuwa hali hii imetokana na uharibifu wa matumbawe ya baharini unaofanywa na wavuvi wanotumia mabomu na ukataji wa miti ya aina ya mikoko ambayo tokea dahari na enzi imekuwa ndio kizuwizi kikubwa cha maji ya bahari kula ardhi.

Katika miaka ya karibuni maelfu ya mikoko imetoweka na katika baadhi ya sehemu kinachonekana ni visiki vya tu vya miti hii na minazi.

Hii hali ya kusikitisha na ya kutisha intoa ishara ya kutokea hatari kubwa zaidi huko mbele na kila siku tunasikia habari za maeneo ya ufukweni ya visiwa vya Uguja na Pemba kupotea kwa kumezwa na maji.

Ukataji holela wa mikoko ii kupata kuni, kuchoma mkaa au kupata miti kwa shughuli za ujenzi na michezo ya baharini ya watalii bila ya kuwepo utaratibu mzuri wa kuhifadhi mazinira ya bahari, utazusha balaa kubwa siku za baadaye kama haujadhibitiwa.

Kinachosikika siku hizi katika sehemu nyingi za visiwa vya Unguja na Pemba ni malalamiko ya bahari kula ardhi, lakini inasikitisha kwamba juhudi za kutafuta suluhisho hazitiliwi sana mkazo, ukiachilia mazungumzo katika semina na warsha.

Hili suala linahitaji mipango madhubuti ya kisayansi na elimu kwa jamii, pamoja na kuweka sheria zitazohakikisha hifadhi nzuri ya mazingira na hasa ukanda wa pwani.

Wakati umefika wa kusema sasa basi kwa huu mtindo wa ukataji miti holela na uharibifu wa mazingira ya bahari.

Upungufu wa baadhi ya mazao kama nazi, embe na mengine kuanza kupungua na miti mingine kupotea ni ishara ya hatari iliyopo usoni.

Uharibifu wa mazingira, hasa wa fukwe za bahari utaipotezea Zanzibari mandhari nzuri ambayo hivi sasa inawavutia watalii kutoka kila pembe ya dunia.

Watu wanaoharibu matumbawe baharini kwa uvuvi wa kutumia mabomu au wanaopiga mbizi bila ya kujali athari za mazingira ya bahari nao watungiwe sheria kali za kuwaadhibu na wasihurumiwe.

Ni wajibu wa kila Mzanzibari kutunza urithi mzuri wa bahari na ardhi tulioachiwa na wazazi wetu. Tusiwe majabari tu wa kukata miti ovyo, bali kwanza tuwe mahodari katika kupanda hiyo miti kwa wingi na kuitunza.

mwananchi

Share: