Makala/Tahariri

VIONGOZI KAMA HAWA HAWATUFAI

Katika maisha yangu niliyoishi kama mwananchi wa Zanzibar, na chini ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sijapata kuona Rais hodari na mwenye imani na nchi hii, na aliefanikiwa zaidi kisiasa kama Amani Karume. Mimi ni muumini mkubwa wa Amani Karume na ni mtu ambaye namchukulia Karume kama ni Rais bora katika maisha yangu yote ukilinganisha na viongozi wengine waliotangulia kwa sababu chungu nzima.
Ya kwamba,tukiacha Amani Karume alitoka chama gani, ukweli unabaki kuwa ni Rais pekee aliefanikiwa kuzungumka kiuno kipana cha mbuyu wa siasa nyaufunyaufu za Zanzibar. Siasa za kujipatia uluwa na umaarufu si kwa kuleta sera za kimaendeleo wala hoja za kimsingi na kimaendeleo, bali kwa siasa za kuuza pumba na ujinga wa kuwagawa Wazanzibari. Pia kuwa na ubavu wa kudiriki kuzilima fitina na uhasama, ukaweza kuzipalilia na watu wakavuna.

Siasa za Viongozi wetu wa vyama hapa Zanzibar tangu asili hazina jipya la kushika kama si pumba na upuuzi wa kuhamasisha uhasama na chuki. Na haya ndio matunda yanayobakia katika madaftari ya kihistoria ya siasa za Zanzibar kwa muda mrefu. Ya kwamba ili uchagulike na ili upate uluwa chamani, ujue kutukana, kufitinisha watu, kushushuwa na kuchenjebuwa, na zaidi kutukana matusi ya nguoni hadharani. Hapo utakuwa kiongozi na mtu unayependwa. Ili hutuba yako ipendwe, sharti ijae matusi na mipasho ya bila kwa wala. Hivi ndivyo tulivyojengwa na watawala wetu.

Upeo wangu wa kuelewa siasa za kikwetu wanibashiria kuwa yote hayo niliyoyataja hapo juu ni matokeo ya akili za watu walioishiwa, muflis, walio nyuma sana kimakuzi ya kiakili na maarifa ambao katika nchi zilizojengeka kiuzalendo hawawezi kupata wadhifa wala kazi yoyote zaidi ya mieleka, misumbwi, riadha, kuvuta mbungo na kazi nyengine za kibachore (menial jobs). Hivi ndivyo mataifa yenye macho na uzalendo yanavyowahukumu watu wanaoabudu kiuno cha mbuyu wa ujinga kinachozaa mbuyu za uhasama na chuki ili kujipatia uluwa wa nchi kama hivi tunavyofanya hapa Zanzibar.

Rais Karume wa Kwanza aliendekeza fitina alizoakipata kutoka kwa Sefu Bakari. Mema aliyotenda yakafunikwa na ubaya wake ikiwamo ya kututia kwenye Muungano unaotula sasa, na yeye akapata lake fungu kwa kusokolewa roho yake mbichi. Mungu amrahamu. Aboud Jumbe, akiongozwa ni akili zake za kilevi. Akawa analoliona zuri asubuhi mchana ni baya. Lililokuwa tamu jioni ya jana asubuhi ya kesho hushinda shubiri kwa uchungu. Akaboronga kwa kuabudu siasa za kilevi na tamaa ya madaraka. Akapata mrabaha wake kutoka kwa Bwana wake aliemuamini, Mwalimu!

Hassan Mwinyi hapa simgusi kwani si mahala pake. Akaja Sheikh Idrisa, welii mzuri na Sheikh mtambuka wa dini ya Kiisalmu. Akatiwa kizoro cha panga ya mashetani, akachagawa pepo wa kichwa na wa kiluwa waingiao kiunoni. Akaendekeza ya kuambiwa hadi akaponyokwa na kauli kwa kusema ‘Mpemba ni kutu la Ng’ombe’, na bila kujali maana na athari ya kauli hii kuwa amepandikiza chuki na fitina baina yetu. Alipobaini kafanya makosa, akaachia ikiwa ni pamoja na kushindwa kuendesha nchi.

Salmin Amour (a father of the modern day hatred, and divisive politics in Zanzibar) yeye anatambulika kama muasisi na mkulima mkubwa wa chuki na fitina baina ya Wazanzibari. Kama wangine waliotangulia, hakuwa na cha kuifanyia nchi hii wala cha kusema kwa wanachi zaidi ya pumba na fitina kama wengine. Salmini aliamini siasa hii ya kiuno cha mbuyu wa uhasama na chuki na aliifanyia kazi kubwa na ni vigumu kuiondosha athari zake leo. Matusi ya kisonge, utamaduni wa kisaadati wa maskani, Uunguja na upemba, kuiuwa Zanzibar kimuungano ni athari ambazo zimeacha vidonda ndugu visivyopoa hapa Zanzibar. Kilichompata anakijua mwenyewe. Asfala safiliina!

Amani Karume, wengi wetu tulimuona tobwe na zezeta na tukaamini ni mlevi asiejuwa hata kutia udhu wala kufunga Swala. Tukamdharau. Karume si mtu wa porojo, ni mtu wa vitendo. Na moja kati ya dalili ya mtu mkosefu na asieweza kitu huwa na mdomo mkuubwa na mkali. Karume hakutaka siasa za kijinga na pumba kwani alijuwa haziwezi kuisaidia Zanzibar. Akauwa Maskani, akaondosha chuki licha ya mashindikizo mengi kutoka bara yaliyotaka kumchafulia jina likiwemo la mauwaji ya Januari 26/27, mwaka 2001. Karume alifanikiwa kuleta Amani na maendeleo ya ukweli ndani ya nchi hii kuliko yeyote aliyetangulia.

Wakati wa Karume ulikuwa humuoni Borafya kusimama akatukana matusi ya vua nguo nikuvishe hadharani. Fitina za kipuuzi za kutekana nyara, kupiga watu majumbani kwa ushahidi wa ‘kisayansi’ wa Mussa, na hata ulumbi usiokuwa na maana kama ilivyo sasa haukuwepo. Wakati wa KARUME watu kama Omar Awesu Dadi, Baraka Shamte, Borafya ambao uhodari wao ni kuuza siasa za kijinga na pumba hawakuwa na nafasi. Karume hakuwa mtu wa Fitina wala majungu. Na nchi yetu ilipiga hatua japo moja kimaendeleo tafauti na sasa na hapo awali.

Leo Dokta Sheni karudisha itikadi ya kikale. Itikadi ya kuwapa usoni wapofu, wasio hoja wala haja na nchi hii kuwa na mdomo na kufanya wapendalo. Amri kuu na maamuzi makuu yamerudi kwenye maskani badala ya Baraza la Sheria au mawaziri. Kila mtu ana uwezo wa kufanya na kusema atakalo ilimradi halikigusi chama fulani tu. Ndani ya Serikali ya Dokta Sheni wamerudishwa tena kina Borafya, na watu kama Balozi Sefu Idd ambao siasa zao ni zile tu za kuhamasiha chuki na fitina baina ya Wazanzibari.

Mfano mzuri wa haya ni pale balozi Sefu Iddi alipotoa mlinganyo (equation) ya hesabu safi kule Bububu alipokuwa akifunga kampeni kwa kusema, maadui zetu ni wawili kwa watatu (CCM buluu+ CUF+ Uamsho = Maadui wa CCM jani na Muungano). Balozi ni mjuzi wa hisabu za Algebra. Akajaribu kupunguza hisabu hio ikawa hivi ( CCM bluu+ CUFUAMSHO =Maadui zetu). Kiongozi ni sukani au kioo cha jamii. Wananchi wameimeza hisabu hii na huku Borafya akiishadidia. Dokta Sheni kanyamaza kimya! Mti wa Chuki na uhasama unazidi kumea huko. Mara yule kafanywa hivi yule vile hamna anaejali. Hizi ndio siasa zetu tulizozizoea. Mburumatari na vichwa maji wamepewa sukani, wacha waendeshe tu!

Na kama watu wenye mitazamo mgando kama hawa wasiojuwa cha faida chochote ndani ya nchi wanaotumia siasa za pumba na majungu ili kujipatia umaarufu kwa kufitinisha watu na kutoa sera zenye kasumba na pumba hawakuondoshwa basi hatuwezi kufuzu. Ipo haja ya kuwasahau watu wanaokimbilia katika siasa kwa kupitia mlango huu. Nchi hii inahitaji watu wenye upeo mpana na uelewa.

Watu wanaotanguliza hoja badala ya haja zao. Watu wenye kuamini kuwa ukweli kwa wananchi ndio utaowajenga na kuleta maendeleo nchini. Nchi hii inahitaji kuwasamehe watu wanaopenda kuingia katika siasa kwa kukosa la kufanya kutokana na upeo wa maarifa yao kuwa finyu. Huu sio wakati wa kujipatia sifa kwa mtu au chama bali nchi kwa kuleta maendeleo ambayo hayapatikani kwa kuendekeza kuchaguana kwa vigenzo bubu vya ujinga, kasumba na kujuana kama tulivyo sasa. Tunajirudisha nyuma wenyewe! Tubadilike!

Tagsslider
Share: