MaadiliMakala/Tahariri

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA UTAJIRI.

Baada ya kumshukuru ALLAH (SW) kama anavyostahiki kushukuriwa, sala na salamu zimfikie Mjumbe wake Sayyidina Muhammad (saw) pamoja na Masahaba wake na kila anaefuata njia yake kwa wema mpaka siku ya malipo.

Amma baad :
Enyi Waja wa ALLAH.
Tambueni kuwa utajiri ni neema kubwa ambayo ALLAH huwaneemesha baadhi ya waja wake. Hivyo, alieruzukiwa mali na akatekeleza haki ya mali kama ipasavyo huwa amewafikishwa katika kheri na furaha ya milele. Lakini kutokana na vitendo vya baadhi ya matajiri, wametokea watu katika umma huu wanaotizama mali kuwa ni kitu cha shari na chenye mwisho mbaya, na hii sio fikra sahihi. Kwani katika Qur-ani Tukufu kuna amri ya kutoa zaka na sadaka, kuwasaidia masikini na mafakiri, na kujenga misikiti na madarasa. Basi nani atafanya haya ikiwa kila Muislamu atakua masikini au vipi mtu atafanya haya ikiwa hana mali ?

Enyi Waislamu.
Pamoja na aya zenye kuamrisha kutoa zaka, katika Kitabu ya ALLAH (SW) kuna aya nyengine nyingi zinazowahimiza waislamu kutafuta mali na rizki zao katika ardhi.
Anasema ALLAH (SW) :
{ هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولاً فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِنْ رِّزْقِهِ } الملك 15
“ Yeye ndie alieidhalilisha ardhi kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake ”.

Na pia anasema :
{ فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّهِ } الجمعة 10
“ Na itakapokwisha sala, tawanyikeni katika ardhi na mtafute fadhila za ALLAH ”.

Na haya yametiliwa mkazo na Mtume (saw), kwani alikuwa anapotoka msikitini anasema :
(( اَللَّهُمَّ اغْفِرْ لِيْ ذُنُوْبِيْ ، وَافْتَحْ لِيْ أَبْوَابَ فَضْلِكَ ))
“ Ewe Mola, nisamehe dhambi zangu na nifungulie milango ya fadhila zako ”.

Na imepokewa kutoka kwa Ibnu Umar (ra) kuwa Mtume (saw) amesema :
(( لاَ حَسَدَ إِلاَّ فِيْ اثْنَتَيْنِ : رَجُلٌ آتَهُ اللهُ مَالاً فَسَلَّطَهُ عَلَى هَلَكَتِهِ فِيْ الْحَقِّ ، وَرَجُلٌ آتَهُ
اللهُ الْحِكْمَةَ فَهُوَ يَقْضِيْ بِهَا وَيُعَلِّمُهَا ))
“ Hakuna kuoneana choyo isipokuwa katika mambo mawili : mtu aliepewa mali na ALLAH kisha akaitumia yote katika njia ya haki, na mtu aliepewa hikma na ALLAH kisha akaitumia na akaifundisha ”.

Enyi Waja wa ALLAH.
Inafaa tujiulize, vipi Sayyidina Abuubakar Al-Siddiq (ra) aliweza kuliandaa na kulihudumia jeshi la waislamu kwa hali na mali kama hakuwa tajiri ? Au jee pale Sayyidina Othman bin Affan (ra) alipolilisha jeshi la waislamu alikuwa fakiri ? Jawabu ni kuwa, hawa wote walikuwa ni matajiri na walitumia mali zao katika njia za kupigania haki na kunyayua bendera ya tawhidi.
Ni wajibu wetu kujua kuwa, ALLAH (SW) ndie muendeshaji wa mambo yote ya ulimwengu huu na rizki zetu zote ziko mikononi mwake, na pia kumpa mtu utajiri ni katika maamuzi yake.
Anasema ALLAH (SW) :
{ وَأَنَّهُ هُوَ أَغْنَى وَأَقْنَى } النجم 48
“ Na kwamba yeye ndie atowae cha kutosheleza na cha kuweka ”.

Basi tujitahidi kutafuta mali kwa njia za halali ili tujiepushe na umasikini, na katika uislamu kuna njia na sababu nyingi za kupata rizki na utajiri.
Njia ya mwanzo ni uchamungu kwa maana ya kumuogopa ALLAH, jambo ambalo hufunguwa kila mlango wa kheri.
Anasema ALLAH (SW) :
{ وَمَنْ يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجاً * وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَحْـتَسِبُ } الطلاق 2-3
“ Na anaemuogopa ALLAH humtengezea njia ya kuokoka (na kila balaa). Na humruzuku kwa njia asioitarajia ”.

Na anasema :
{ وَمَنْ يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَلْ لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْراً } الطلاق 4
“ Na anaemuogopa ALLAH humfanyia mambo yake kuwa mepesi ”.

Na pia anasema :
{ وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَى آمَنُواْ وَاتَّقَواْ لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالأَرْضِ وَلَـكِنْ
كَذَّبُواْ فَأَخَذْنَاهُمْ بِمَا كَانُواْ يَكْسِبُونَ } الأعراف 96
“ Na lau kama watu wa miji wangeliamini na kuogopa, kwa yakini tungeliwafungulia baraka za mbingu na ardhi. Lakini walikadhibisha nasi tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliokuwa wakiyachuma ”.

Njia ya pili ya kuwepesisha kupatikana kwa rizki ni kuomba msamaha kwa ALLAH kutokana na makosa yetu ya kila siku, kama alivyofundisha hayo Nabii Nouh (as) pale aliposema :
{ فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّاراً * يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَاراً * وَيُمْدِدْكُمْ بِأَمْوَالٍ
وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَاراً } نوح 10 -12
“ Nikawaambia : Ombeni msamaha kwa Mola wenu, hakika yeye ni mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi. Na atakupeni mali na watoto na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito ”.

Amma njia ya tatu ya kuzidishiwa rizki ni kumshukuru ALLAH (SW) kwa kila neema aliotuneemesha.

Anasema ALLAH (SW) :
{ وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِنْ شَكَرْتُمْ لأَزِيدَنَّكُمْ وَلَئِنْ كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ } ابراهيم 7
“ Na kumbukeni alipotangaza Mola wenu kuwa : Kama mkinishukuru nitakuzidishieni na kama mkikufuru basi jueni kuwa adhabu yangu ni kali sana”.

Umma wa Kiislamu.
Kumbukeni kuwa pamoja na hayo, kutoa zaka na sadaka na kutumia mali katika mambo ya kheri nayo pia ni katika mambo yanayoengeza baraka katika mali na kuwepesisha upatikanaji wa rizki.
Anasema ALLAH (SW) :
{ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ } سبأ 39
“ Na chochote mtakachokitoa yeye atakilipa, na yeye ni mbora wa wanaoruzuku ”.

Anasema ALLAH (SW) :
{ فَأَمَّا مَن أَعْطَى وَاتَّقَى * وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَى * فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَى } الليل 5-7
“ Amma mwenye kutoa na akamchamungu. Na kusadiki jambo jema. Tutamuwepesishia njia ya kwenda peponi ”.

Amesema Mtume (saw) :
(( مَا مِنْ يَوْمٍ يُصْبِحُ فِيْهِ الْعِبَادُ إِلاَّ مَلَكَانِ يَنْزِلاَنِ فَيَقُولُ أَحَدُهُمَا : اَللَّهُمَّ أَعْطِ مُنْفِقًا خَلَفًا ،
وَيَقُولُ الآخَرُ : اَللَّهُمَّ أَعْطِ مُمْسِكًا تَلَفًا ))
“ Hakuna siku wanayopambazukiwa nayo waja isipokuwa huteremka malaika wawili. Na husema mmoja wao : Ewe Mola mpe mtoaji ziada katika mali yake.
Na husema wa pili : Ewe Mola mpe mwenye kuzuia upungufu katika mali yake ”.

Na katika sababu za kuzidishiwa rizki na baraka katika mali ni kuwaunga jamaa na kuwasaidia watu wenye shida za kidunia, kwani Mtume (saw) amesema :
(( مَنْ سَرَّهُ أَنْ يُبْسَطَ لَهُ فِيْ رِزْقِهِ وَأَنْ يُنْسَأَ لَهُ فِيْ أَثَرِهِ فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ ))
“ Anaependa kuzidishiwa katika rizki yake na kuengezewa baraka katika umri wake, basi na awaunge jamaa zake ”.

Na pia amesema :
(( وَمَنْ يَسَّرَ عَلَى مُعْسِرٍ يَسَّرَ اللهُ عَلَيْهِ فِيْ الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ ))
“ Atakaemuwepesishia (atakaemsaidia) mwenye shida, basi nae ALLAH atamuwepesishia katika dunia na akhera ”.

Enyi Waja wa ALLAH.
Inasimuliwa kuwa masikini miongoni mwa Muhajirina walikwenda kwa Mtume (saw) wakasema : “ Wamekwenda zao matajiri hali ya kuwa wana daraja za juu na mambo mazuri”. Mtume (saw) akawauliza : “Ni mambo gani hayo ?” Wakasema : “ Wanasali kama tunavyosali, wanafunga kama tunavyofunga, lakini wao wanatoa sadaka na sisi hatutoi na wanawaachia huru watumwa na sisi hatuna uwezo huo”.
Mtume (saw) akawaambia : “ Jee nisikufundisheni kitu ambacho mkikifanya mtawafikia waliokupiteni na mtawashinda waliokuwa nyuma yenu, isipokuwa atakefanya kama munavyofanya nyinyi ?”
Wakasema : “Tuambie Ewe Mjumbe wa ALLAH”.
Mtume (saw) akawaambia : Semeni baada ya kila sala ‘Subhanallah’ na ‘Allahu-akbar’ na ‘Alhamdu-lilah’ mara thalathini na tatu.
Baada ya muda wale Muhajirina wakarudi tena kwa Mtume (saw) wakasema : “ Ndugu zetu matajiri wamesikia haya tunayoyasema na wao sasa wanayasema ”. Mtume (saw) akasema :
(( ذَلِكَ فَضْلُ اللهِ يُؤْتِيْهِ مَنْ يَشَاءُ ))
“ Hizo ni fadhila za ALLAH anampa amtakae ”.

Enyi Waja wa ALLAH.
Kumbukeni kuwa, miongoni mwa masuala atakayoulizwa kila mja siku ya hesabu ni : “ Vipi aliichuma mali yake na vipi aliitumia ? ”
Basi mcheni ALLAH Mola wenu mtukufu katika mambo yenu yote, na chumeni mali kwa njia za halali na zitumieni katika mambo ya haki, ili mpate kufaulu katika dunia na akhera yenu.

والسلام عليكم ورحمة الله تعالى وبركاته .

Share: