Makala/Tahariri

Wagombea wenye dhamira tofauti

Jabir Idrissa

JENGA picha kwa haya: Wakati mgombea urais mshindani mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maalim Seif Shariff Hamad anahutubia mkutano wa kampeni yake, Jimbo la Mpendae, ghafla gari iliyofunga maspika inapita.

Inapita uwanjani Kwa Binti Amrani, ikitangaza mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.
Gari hii ya matangazo ipo katikati ya eskoti ya Jeshi la Polisi – mbele gari ya polisi na nyuma gari ya polisi. Gari mbili. Waliomo katika msafara huu, wamejaa mbwembwe.

Ninakuongezea tu maneno upate kujenga vizuri picha ambayo sidhani kama hujaielewa. Kama hujaipata picha ninayokufikirisha, itakuwa unalo tatizo; samahani.

Mkutano unaotangaziwa wananchi wafike ni wa uzinduzi wa kampeni ya mgombea urais wa CCM, Rais anayetaka miaka mingine mitano ya kuongoza Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ule mkutano wa Kwa Binti Amrani “unaoingiliwa kihujuma” (ndivyo ninavyotafsiri), ukavunjwa. Maalim Seif anayerudia mara kwa mara kusema anahujumiwa kisiasa, aliliacha jukwaa, akateremka, na kuita wasaidizi wajitahidi kuepusha shari.
Hapo walinzi wa CUF wasimamie pasitokee mapambano.

Safari hii Maalim Seif, inajulikana wazi na kila Mzanzibari, Mtanzania na hata mgeni anayefuatilia uchaguzi mkuu wa Tanzania wa 2015, anawakilisha muungano wa vyama vinne uitwao Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Umeipata picha enh?

Rais mtaka tena uongozi, ni kiongozi mkuu CCM. Wafuasi wake kwa kulindwa na Polisi, taasisi mojawapo ya dola ambayo kikatiba ndio msimamizi wa sheria na amani nchini, wanahujumu mkutano wa mshindani wake.

Mpaka ninapoandika uyasomayo, Polisi – hii taasisi unayowaona wakuu wake wakisema kila wakati na sasa wakihimiza utiifu wa sheria kipindi cha uchaguzi mkuu – haijakamata mtu kuhusiana na tukio hilo.

Jamani, gari tatu katika sinema: iliyobeba watangazaji wanaopeperusha bendera ya CCM; na nyingine mbili za hii Polisi, waliovaa kivita.
Hili somo muhimu. Tarehe 30 Machi mwaka huu, Maalim Seif alilazimika kukagua majeruhi majumbani na hospitalini (angalia picha hapo juu). Ni majeruhi wa tukio la kijinga na kikatili, la kupigwa mapande ya nondo na mapanga wakati wakiwa kwenye gari za msafara mrefu wa watu wakitoka Makunduchi, kijiji cha Wilaya ya Kusini Unguja, kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CUF.

Akiwa mkutanoni Makunduchi, eneo ngome ya CCM, Maalim Seif alikabidhi kadi 600 kwa wanachama wapya waliohama CCM.
Kule, alipata kusema mpango wa wahuni kuhujumu msafara wakati utakapokuwa unarejea mkutanoni.

Mpaka unavyosoma haya, hajakamatwa yeyote kuhusiana na tukio hilo ingawa namba za usajili za gari zilitajwa na gari limetambuliwa mwenyewe, kiongozi wa CCM.

Mkutano ulilindwa na Polisi hasa kwa kuwa ulimhusisha mkubwa huyu, Makamu wa Kwanza wa Rais, msaidizi mmojawapo wa Rais Dk. Shein.
Siku kadhaa kabla ya Makunduchi, wahuni waliteketeza kwa moto ofisi za kisasa za CUF, Jimbo la Dimani, zilizokuwa hatua chache kutoka uzio wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume, Kisauni.Hajakamatwa yeyote. Sina shaka hakuna kesi mahkamani kuhusu tukio hilo.

Sambamba na matukio hayo, wananchi kadhaa wameumizwa kwa mashambulizi ya kijasusi yanayofanywa na watu wanaolindwa na askari wa vikosi vya SMZ ambao hujifunika soksi usoni. Mengi ya matukio haya huwa mchana kweupe.

Kijijini Chwaka mwanamke alibakwa mchana kweupe; yalitokea Tumbatu kisiwani alikojenga ufalme wa kisiasa Waziri anayehusika na vikosi hivi vya SMZ, Haji Omar Kheri, mgombea uwakilishi kwa mara nyingine.

Wakati wa uandikishaji wapigakura wapya, matukio yalitokea Kizimkazi, kijiji jirani na Makunduchi ambako mwananchi alipigwa risasi ya mguu. Mjini Zanzibar haya ni matukio ya kawaida.

Hajashitakiwa mtu yeyote mote humo, hakuna kesi hata baada ya “majambazi” hawa kuvamia kituo cha Coconut FM, Migombani walikotaka kumteka ripota ambaye baada ya vitisho, mwajiri amemtoa kazini.

Yote haya yanatokea, huku kauli za wakuu wa Polisi, zikifanana na dhihaka. Polisi haijali ushenzi wanaotendewa wananchi. Wanapuuza kwa sababu hawawezi kudhibiti uhalifu huu mkubwa. Wanaouweza ni vibaka wa kuku, mazao na ‘unga’ pamoja na michongo ya kudai kuna magaidi. Kumbe mwananchi asemeje?

Nikaandika makala iliyobeba maneno “Dk. Shein zuia siasa za kijambazi.” Nikaanza, kuna dhambi kubwa inatendeka Zanzibar. Ni siasa chafu ambayo fumbo zuri la maneno linalostahili kuiita, ni “siasa za kijambazi.”

Nikasema, “na kwa kadri nionavyo, ni muhimu Rais Dk. Shein, kama anadhibiti dola hii (leo nataja Zanzibar), akatoa uongozi wa hekima kuzuia mchuruziko mkubwa wa damu.”

Ni miezi mitano leo, wahuni waliobeba bendera ya CCM, nao wakiwa wamebebwa na Polisi, wanavuruga mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa mgombea urais. Tume ya Uchaguzi Zanzibar ipo kazini. Kimya.

Ama kweli, hawa CCM ni sikio la kufa lisilosikia dawa. Wanatosha.

Nami sina zaidi, niseme tu kwa hakika kabisa, nikiamshwa usiku wa manane, na lepelepe la usingizi, nitasema kati ya wagombea hawa wawili, mmoja anajali umma na mustakbali wa Zanzibar, mwingine anajijali binafsi na chama chao.

Wewe mwananchi amua – unataka kiongozi anayekujali na nchi yako; au anayekudhihaki na nchi yako. Nimejitoa mhanga kuipigania kauli yangu popote na vyovyote iwavyo. Ewe Mwenyeezi Mungu nisaidie!

Tagsslider
Share: