Makala/Tahariri

Wanaompopoa Shein ni CCM maslahi

Jabir Idrissa,

ASILI ya kutokea wanachama wa CCM wakalalamikia wanachokiona kama kitu kibaya kutendeka ndani ya siasa za chama hicho, ni kumsimanga Dk. Ali Mohamed Shein.

Ndani ya andishi la wanaojiita “Wana-CCM kindakindaki” au wanachama wa Taliban, lililotupwa mtandaoni wiki iliyopita, yapo malalamiko kwamba Dk. Shein ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, amekikabidhi chama kusikopaswa.

Kwanza, wana-CCM Taliban wanasema hawakushangaa kuona Dk. Shein hakushtushwa wala kupatwa na hofu na fadhaa kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.

Ni kwanini hawakushangazwa na Dk. Shein kutoshtushwa? Wanasema katika andishi lao kuwa yu kiongozi mwenye tabia ya kutaka “kumfurahisha kila mwenye jina kubwa ndani ya CCM.”

Wanadai kuwa walipoona taarifa ya ufisadi wa Balozi Amina Salum Ali, katika mitandao ya kijamii, walijua arubaini ya (wanataja jina baya la kumtuhumu Balozi Amina) imetimia. Dk. Shein anaambiwa amempa uteuzi wa bure Balozi Amina. Eti hana sifa ya kuteuliwa.

Ni hapo wana-CCM wa Taliban wanasema mwenendo huo wa Dk. Shein kumteua Balozi Amina umekuja kutokana na wasiwasi wake na fadhaa katika kile kiti alichokalia akiuogopa “mzimu wa CUF wa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, alioutengeneza mwenyewe.”

Hapa wanazungumzia Chama cha Wananchi (CUF) ambacho yumkini wanathibitisha kuwa siasa za CCM zilishindwa kumwezesha Dk. Shein kushinda uchaguzi. Kwamba kila akikaa leo, anaona kivuli cha CUF, chama kinachoshikilia kuwa kilishinda uchaguzi na kufisidiwa.

Umekuwa ndio msimamo wa CUF kwamba CCM kilishindwa uchaguzi na kilipobaini kushindwa, viongozi wake walishikamana na kwa msaada wa vyombo vya dola wakafanikiwa kumlazimisha Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi na matokeo yake yote. Ilikuwa ni hatua ya kuvunja Sheria na Katiba ya Zanzibar.

Mpaka sasa, CUF wakishikilia msimamo huo wa kuhujumiwa kwa maamuzi ya wananchi waliopigakura halali, uongozi wa CCM umekataa kuirudisha haki kwa walioshinda halali.

Hata ile ahadi ya Rais John Magufuli siku alipohutubia Bunge la 11 mjini Dodoma, kuwa atashughulikia mgogoro wa Zanzibar uliohusu uchaguzi, akisaidiana na makamu wake wa rais, Samia Suluhu Hassan, imepigwa kumbo.

Ni rais Magufuli mwenyewe aliyetangaza hadharani mwaka mmoja baadaye kuwa hakuna mabadiliko na kwamba Dk. Shein ndiye rais wa Zanzibar, hata watu wakitaka kuchoma samaki, hataondoka.

Fuatana nami. Wakati Rais ambaye pia ndiye sasa Mwenyekiti wa CCM Taifa, akishikilia msimamo huo, kama kuonesha CCM ilishinda kihalali uchaguzi, wana-CCM wa Taliban wanasema vingine.

“Ukitazama kwa undani hali ya chama chetu hivi sasa ambacho kilisimama kwa uzalendo mkubwa katika miaka ya 1990 pamoja na upinzani mkali wa CUF, utaona kimeshapoteza na kinaendelea kupoteza mvuto kwa wanachama wake.

“Matokeo ya haya hayawezi kujificha wala kufichwa, kila kitu kipo hadharani. Hebu tuangalie uchaguzi wetu wa ndani ya chama ulioanza (hivi karibuni). Uchaguzi huu unathibitisha namna CCM yetu ilivyokosa ghera, raghba na hamasa.”

CCM kimepoteza mvuto kwa wanachama wake. Dalili ziko wazi, hazifichiki. Mwenendo wa uchaguzi wa CCM unaofanyika sasa, unathibitisha. CCM imekosa ghera, raghba na hamasa. Maneno yao wenyewe.

Maana yake ni kwamba chama hicho hakivutii tena machoni pa umma, hasa kama tayari wenyewe wanakiri kimepoteza mvuto kwa wanachama wao. Viongozi wake hawaaminiki tena. Ni kwanini wasiaminike tena viongozi wanaotajwa kuwa imara wakati wa utawala wa Dk. Salmin Amour Juma – Komandoo aliyesifika kwa uongozi wa mkono wa chuma dhidi ya viongozi wa CUF?

Kumetokea mabadiliko makubwa ya kifikra Zanzibar. Achilia mbali watu wazima walioshuhudia Mapinduzi ya 12 Januari 1964 na baadaye Muungano wa 26 Aprili 1964, nguvu kubwa ya vijana wanaotaka mabadiliko ya kivitendo, imeshtadi isivyo kawaida.

Vijana wanataka matunda ya uongozi mwema leo. Wanataka maisha mazuri ya maziwa na asali. Hawa wameikubali manifesto ya CUF, ambayo pamoja na mambo mengine, imeahidi kuibadilisha Zanzibar kuwa Singapore ndani ya bara la Afrika.

Ahadi hii wameithibitisha kuwa si ndoto ya alinacha. Asilani. Ni mpango unaotekelezeka kwa namna ulivyowasilishwa na timu ya kampeni ya Maalim Seif Shariff Hamad, kiongozi anayevutia makundi yote ya Wazanzibari, hususan hao vijana.

Makundi ya vijana walikuwa wakimfuata Maalim Seif kila alikofika kufanya kampeni. Hawakujali vituko vya serikali ya CCM iliyotumia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kudhibiti mfumo mzima wa uchaguzi kama ilivyotokea mwishoni.

Lakini kinachoshtua zaidi viongozi wa CCM kwa sasa, ni namna wananchi wa vijiji maarufu kwa kuwa ngome yao kisiasa, walivyokigeuka chama hicho na kujiunga CUF. Kilichowavutia ni imani kwa viongozi na pia kuipenda Zanzibar na kuitakia haki zake ndani ya mfumo wa Muungano.

Viongozi wa CCM wamethibitisha mara kadhaa shida yao ni kuwepo tu madarakani; wala sio kulinda maslahi ya kweli ya Zanzibar na watu wake. Kilichotokea kwenye Bunge Maalum la Katiba, kuivuruga Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano yenye maoni ya wananchi, ushahidi mzuri.

Ndani ya Baraza la Wawakilishi, wajumbe wakiwemo wa CCM walijadiliana masuala ya kutambuliwa kuwa ndio muhimu zaidi kwa maslahi ya Zanzibar na watu wake, na kukatoka azimio la baraza kuhusu msimamo huo.

Lakini, mbele ya kuta za Bunge, na wakiwepo wakubwa zao, wale wanaosimamia maslahi yao ya kutwaa madaraka ya dola, wakawageuka wenzao wa upinzani na kujitenga na azimio.

Hili azimio kwa sehemu kubwa lilitokana na maoni ya wajumbe wa CCM ndani ya Baraza la Wawakilishi, ambao walisikika hadharani wakitoa sauti nzito kulalamikia namna Zanzibar inavyokandamizwa chini ya mfumo wa Muungano.

Wajumbe wenyewe wa CCM ndani ya Baraza, ni pamoja na waliokuwa mawaziri katika serikali ya umoja wa kitaifa aliyoiongoza Dk. Shein, baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 ambako kulikuwa na maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na CUF kumaliza siasa za chuki na fitna.

Kitendo cha CCM kudhibiti mawazo ya wajumbe wa Bunge Maalum kiliwalazimisha wajumbe wa upinzani na wale wajumbe waliokuwa si wanasiasa lakini wenye mawazo yao, kutoka bungeni.

CCM waliendeleza mkakati wao na hatimaye wakatoka na walichoita “Katiba inayopendekezwa” ambayo mpaka sasa wananchi hawajapewa fursa ya kuiamua.

Utaratibu huu wa CCM kupenda zaidi matakwa yake kuliko hatima ya kweli ya nchi, umekitia adabu chama hicho. Ni chimbuko kuu la kupoteza mvuto kwa umma. Na si ajabu leo, kama wanachama wenyewe wanavyosema, kisipate wagombea nafasi katika uchaguzi wa ndani.

Kila mwenye akili anajua Dk. Shein atakuwa anatupiwa lawama lakini wa kulaumiwa ni uongozi wote ulioshindwa kusoma alama za nyakati, wakisahau asili zao za kupigania haki za wanyonge. Siku hizi wanapigania haki za kibinafsi zaidi.

Tagsslider
Share: