Makala/Tahariri

Watu wema wakikaa kimya, maovu hushamiri!..

Mjumbe wa Kamati Kuu na aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA chini ya mwevuli wa UKAWA 2015, Edward Lowassa wakibadilishana mawazo na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama hicho, Dk Salim Ahmed Salim katika moja ya matukio muhimu ya kijamii.

Imeandikwa na Gululi Kashinde – Raia Mwema
Marchi 21, 2018

EDMUND BURKE (1729-1797) ni jina mashuhuri sana katika duru za kisiasa na utetezi wa haki za binadamu. Burke, alizaliwa huko Dublin, Republic of Ireland zaidi ya miongo ishirini iliyopita.

Katika hali ya kushangaza aliwahi kusema “The only Necessary for the Triumph of Evil is for Good Men to do nothing” kwa tafsiri isiyo rasmi sana alimaanisha kuwa, watu wema wakikaa kimya maovu hushamiri.

Kila jamii huzalisha watu wake wema. Na watu hawa wanapatikana katika makundi yote tuliyonayo ndani ya jamii zetu. Hawa wakipaza sauti zao husikika, husikilizwa na kuheshimiwa.

Katika nchi nyingine zinazoheshimu misingi ya kidemokrasia makundi haya ya watu wema, hujigeuza kuwa washauri muhimu wa serikali kwa namna mbalimbali kadri fursa inapojitokeza.

Sababu za kupenda kushauriwa na watu ambao hawapo ndani ya mifumo rasmi ya ushauri ni kutoa fursa ya kuambiwa hata yale usiyopenda kuyasikia.

Kundi hili la washauri lilijipatia nguvu kubwa sana ya ushawishi ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Jakaya Mrisho Kikwete.

Nguvu ya kundi hili la “watu wema” ilisababisha serikali ya Kikwete kuchelewa kuchukua au kufanya uamuzi kwa haraka kwa kile kilichofahamika wakati huo “serikali kusoma upepo kwanza”.

Suala la kusoma upepo katika kufanya uamuzi wa kiserikali ilikuwa na faida moja kubwa kwa serikali ya Kikwete. Faida kubwa ni kwamba, serikali iliweza kusikiliza maoni ya wadau na makundi mbalimbali yenye fikra na mitizamo tofauti ndani ya nchi.

Kuna wakati fulani Serikali ya Awamu ya Nne iliweza kuheshimu maoni hayo na kuyafanyia kazi walau kwa shingo upande. Orodha ya mambo yaliyofanyiwa kazi japo kwa shingo upande ni mchakato wa kuandika Katiba Mpya.

Hii haikuwa hoja ya serikali hata kidogo, wala haikuwemo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni “kelele” pekee za wananchi ndizo zilizosababisha serikali ya Kikwete kuanzisha mchakato huo.

Japokuwa mchakato wenyewe ulivurugwa na wale ambao hawakuupenda tangu awali, lakini tuliowengi bado tunaamini kwamba angalau kuna pahala pakuweza kuanzia.

Jini la Katiba Mpya limekwisha kutoka kwenye chupa. Kamwe haliwezi kurudi tena ndani ya chupa. Katiba Mpya bado ni hoja pendwa hususan kwa wazalendo wa nchi hii.

Katika safu hii ya leo, nitachambua baadhi ya makundi ya watu wema ambayo bado wamekaa kimya, huku maovu yakizidi kushamiri. Ni vema nikaeleweka mapema kwamba, makundi haya si washauri rasmi wa mifumo ya nchi na utawala.

Bali hawa ni wale wanaojitokeza na kujipa kazi hiyo ngumu ili kuokoa jahazi baada ya kupigwa na upepo mkali, radi, mvua na kimbunga cha hapa na pale. Nahodha mzuri lazima awasikilize kwa makini ili chombo kisiende mrama na safari ndefu kifike salama.

Kundi la kwanza ni wazee. Mara nyingi kundi hili huundwa na watu mchanganyiko; wamo wastaafu waliofanya kazi kubwa na utumishi uliotukuka ndani ya nchi yetu, wamo wafanyabiashara maarufu waliofanikiwa sana kibiashara na wenye ushawishi na heshima kubwa ndani na hata nje ya mipaka ya nchi yetu.

Mtaji wa kundi hili ni uzoefu katika medani mbalimbali, hekima na busara. Tafasiri halisi ya uzee katika tamaduni nyingi barani Afrika ni wingi wa hekima na busara. Wazee ni nuru ya kutuonesha njia, kupoza na kutuliza mizuka na kuimarisha umoja palipo na dalili za mitafaruku.

Kundi hili la wazee lilijitokeza hadharani katika awamu ya nne kwa kukemea na kuonya bila woga. Lakini katika awamu hii ya tano inayoongozwa na John Magufuli siwaoni, hawasikiki, wako kimya.

Hata baadhi yao ambao taifa lilianza kuamini kuwa wanaweza kuwa warithi wazuri wa Mwalimu Julius Nyerere hasa kwenye misimamo na tafakuri ya mambo ya nchi, pia hatuwaoni, hatuwasikii na wako kimya. Hii si dalili nzuri huko tuendako.

Ni ukweli mtupu kwamba, baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kutangulia mbele ya haki, taifa letu limekosa vyote.

Kwanza, tumekosa Baba wa Taifa. Pili, tumekosa kiongozi anayechukia makosa na kupenda wakosoaji. Tatu, tumekosa kiongozi anayekubali makosa yake na kukiri udhaifu wake hadharani. Nne, tumekosa kiongozi anayetambua kuwa hata wanuka vinywa wana hoja!. Tusihangaike na vinywa vyao vinavyonuka, tuhangaike na hoja zao.

Kundi la pili, ni la viongozi wa dini. Hawa ni wazazi wetu wa kiroho. Kundi hili ni muhimu sana katika kulinda hadhi ya taifa na kujenga maelewano ndani ya jamii.

Kuna baadhi ya nchi ambazo dini hutumika kama utambulisho wa taifa na utaifa kwa watu wake. Alama za dini hazifutiki kirahisi, kwa sababu msingi wa imani unachorwa kwenye nafsi na mioyo ya watu.

Hivyo, ni sahihi kabisa kusema, viongozi wa dini huongoza nafsi na mioyo ya watu. Kwa sababu hiyo, viongozi wa kidini wanasifa kuu nne.

Mosi, wanawafuasi wengi. Pili, husikilizwa na wafuasi wao kwa dhati kwa sababu wamebeba dhamana ya mioyo ya watu. Tatu, huaminika sana na kuheshimika kwa sababu ya kufanya kazi za kitume. Nne, ni watenda haki.

Hii ni sifa ya kipekee na kiupendeleo waliopewa na Mwenyezi Mungu. Katika nchi ambayo kuna dini mbili kubwa, ni rahisi sana kuleta utengamano wa kijamii. Msingi muhimu wa dini ni haki.

Haki ambayo kwenye misahafu yote inatajwa ndio huinua taifa na kinyume chake ni sahihi. Si haki hata kidogo kupuuza ushauri au makatazo kutoka kwa viongozi wetu wa dini.

Tatizo pekee linaloanza kuchomaza kwa kasi kwa baadhi ya viongozi wetu hawa wa kiroho tunaowapenda sana, ni kutosema au kushindwa kukemea kwa wakati huku maovu yakishamiri.

Ni vema tukatambua kwamba, ushauri mzuri uliochelewa ni mbaya zaidi, kuliko ushauri mbaya uliokuja kwa wakati.

Kundi la tatu ni wasomi; kundi hili ni muhimu sana katika maendeleo na mabadiliko ya nchi yoyote duniani. Hawa ni watu wenye nguvu ya maarifa na utajiri wa maono.

Kuna baadhi ya viongozi na wafalme huogopa kutembelea maeneo ya wasomi na vyuo vikuu kwa hofu ya kupingwa na kuogapa mijadala ya kisomi.

Sehemu kama vyuo vikuu ni tanuru la kupika na kuzalisha mawazo mapya. Hawa ni watu wanaoheshimika sana duniani kote, kwa sababu nguvu zao za ushawishi zinatokana na utafiti na hoja.

Hawa wanafursa kubwa ya kukemea, kuonya na hata kutoa muelekeo mpya wa taifa. Changamoto kubwa inayowakabili wasomi wetu hususan kwa siku za hivi karibuni ni kutokuwa thabiti juu ya kauli zao. Alichokikubali jana ndicho atakachokikataa kesho. Hawaaminiki tena. Wameanza kupoteza turufu yao ya uwashawishi ndani ya jamii.

Mifano hai ya kuyumba na kuyumbishwa kwa wanazuoni wetu ipo mingi. Rais John Magufuli pamoja na mambo mengine, amejipambanua kuwa ni muumini wa wasomi. Amekuwa akiteua wasomi mbalimbali katika kada mbalimbali za utumishi wa umma.

Baadhi yao wameenda mbali zaidi na kuiita awamu hii ya tano ni “awamu rafiki kwa wasomi”. Kwa kweli Rais Magufuli amewapiku watangulizi wake wote katika hilo.

Sina hakika kama uteuzi huo unafanywa kimkakati au anajaribu kujibu kilio cha siku nyingi cha wasomi kuwa “wanatengwa na kubaguliwa”.

Wapo baadhi ya wasomi na wengine ni walimu wangu, waliokuwa wameweka msimamo wa kumtaka rais Magufuli kutoteua wahadhiri.

Hoja yao ilikuwa, kuteua wahadhiri ni kuviua na kuvinyima uhai na uwezo vyuo vyetu. Walienda mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa waachwe wafanye tafiti na majukumu mengine ya kihadhiri.

Baada ya muda mfupi, Rais Magufuli aliwateua!. Walikubali kwa mikono miwili uteuzi huo. Hawakuikumbuka tena hoja ya uhaba kwa wahadhiri vyuoni. Walikaa kimya!. ni sawa na kusema, malalamiko yao yalizaa vyeo. Na vyeo vilizaa ukimya.

Pengine huu ni mjadala mpya, unaohitaji uchambuzi kwa siku zijazo!. Itoshe tu kusema, wasomi ni jukwaa huru la kukemea na kuonya ili maovu yasishamiri ndani ya jamii yetu ya Tanzania.

Imeandikwa na Gululi Kashinde; gululig@yahoo.com simu: 0753 270 441

Share: