Makala/Tahariri

Wingu la wasiwasi lazidi kutanda Uingereza

Ahmed Rajab,

KUNA ushindi, na kuna ushindi. Sina hakika niuweke upande gani ushindi wa waziri mkuu Theresa May na chama chake cha Conservative katika uchaguzi mkuu wa Uingereza uliofanywa Alhamisi iliyopita, Juni 8.

Sijui niuweke kwenye fungu la ushindi wa aina ya kwanza au kwenye ushindi wa kundi la pili. Sina haja ya kufafanua wa aina ya kwanza ni upi na wa kundi la pili ni wa aina gani.

Ninababaika kwa sababu matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa ya kushangaza. Walioshinda ndio walioshindwa na walioshindwa ndio walioshinda. Kushinda kulikuwa sawa na kushindwa ; na kushindwa kulikuwa sawa na kushinda.

Theresa May alishinda lakini, kwa kweli, alishindwa. Ijapokuwa wapo wanaokubali kwamba May alishindwa lakini wapo pia wasemao kwamba hapakuwa na mshindi.

Sikubaliani nao kwa sababu ingawa Jeremy Corbyn, na chama chake cha Leba, walishindwa lakini, kwa kweli, wao ndio walioupata ushindi. Hasa Corbyn. Ushindi ulikuwa wake binafsi, ingawa chama chake hakikuweza kuwa na wingi mkuu wa viti bungeni na kuwa chama kikuu.

Ushindi wa Corbyn ulikuwa ushindi uliowasuta wote waliokuwa wakisema kuwa hakuwa na lake jambo na kwamba yeye atakuwa sababu ya chama chake kuwa na wabunge wachache sana. Corbyn aliwashangaza wote kwa idadi kubwa ya wabunge wa chama chake waliochaguliwa, baadhi yao wakiwashinda mawaziri na vigogo wa chama kinachotawala.

Hayo ndiyo yaliyokuwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Juni 8. Ulikuwa uchaguzi usiokuwa wa lazima. Bibi May hakuwa na haja kubwa hivyo ya kutaka pafanywe uchaguzi huo.

Juu ya hayo, May aliamka Aprili 18, akaamua ufanywe uchaguzi wa ghafla Juni 8 kwa sababu moja tu: alizugwa na matokeo ya kura za maoni yaliyomthibitishia kwamba ukifanywa uchaguzi wakati ulipofanywa chama chake kitapata ushindi wa kishindo.

Zaidi ya hayo, alihakikishiwa kwamba atakuwa waziri mkuu mwenye musuli zaidi za madaraka kwa vile atakuwa na wabunge wengi wa chama chake. Hakufanya uchaguzi kwa maslahi ya taifa bali kwa maslahi yake binafsi ya kuonekana kiongozi madhubuti kwa vile akitaraji chama chake kupata ushindi mkubwa.

May angeweza kuendelea kuongoza serikali hadi 2020 lakini kidudumtu kilimshawishi atangaze uchaguzi huo kwa kuwa na hakika kwamba angeshinda. Na si ushindi wa mchezo lakini ushindi wa maana.

Ilikuwa muhimu May aupate ushindi wa aina hiyo ili atapoanza mchakato wa Uingereza kujitoa kutoka Muungano wa Ulaya (European Union), ule mchakato weye umaarufu wa jina la “Brexit”, aonekane kwamba ana nguvu katika bunge la Uingereza kwa kuipitisha miswaada aitakayo.

Katika toleo la Raia Mwema la Aprili 28, 2017 niliandika, miongoni mwa mingine, kwamba mimi kuna mambo mawili, matatu ninayoweza kuyatabiri. La kwanza, niliandika, ni kwamba uchaguzi mkuu wa Juni 8 hautabiriki. “Chama cha Leba kinaweza kikaangushwa kama wachambuzi wengi wanavyotabiri au kinaweza kuushangaza ulimwengu kwa kushinda.”

Yaliyojiri ni kwamba, kinyume na walivyotabiri wachambuzi wengi, chama cha Leba hakikuangushwa. Badala yake kiliushangaza ulimwengu. Hakikuushangaza kwa kujipatia wingi mkuu wa viti bungeni lakini kwa kukinyima chama cha Conservative kisiupate wingi huo mkuu wa viti. Kilichoweza kufanya ni kumpunguzia nguvu Theresa May. Hana tena zile musuli alizofikiri atazipata baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa.

Nimeshuhudia chaguzi kuu nyingi hapa Uingereza tangu miaka ya 1960 hadi sasa. Ningetia mguu London kwa mara ya mwanzo Jumatano ya Oktoba 14, 1964 nikitokea Paris, kama nilivyokuwa nimepanga, ningeushuhudia uchaguzi wangu wa mwanzo wa Uingereza siku ya pili yake Alhamisi ya Oktoba 15.

Lakini Jiji la Paris liliuvuta mkono wangu likanizuia kwa siku mbili nisiondoke kwa vijambo na vivutio vyake. Kwa hivyo, niliingia London Oktoba 17. Hasara ilikuwa yangu kwa sababu niliukosa chupuchupu uchaguzi uliomuingiza madarakani waziri mkuu Harold Wilson wa chama cha Leba. Alimshinda Sir Alec Douglas Home wa chama cha Conservative.

Ushindi wa Leba haukuwa madhubuti. Leba kilipata wingi wa viti vinne tu kukishinda chama cha Conservative, Wilson akaamua (kama alivyoamua Theresa May Aprili mwaka huu) kwamba pafanywe uchaguzi wa ghafla Machi 31,1966. Katika uchaguzi huo wa 1966, Wilson alimshinda bila ya kutokwa na jasho Edward Heath, kiongozi mpya wa chama cha Conservative. Leba kiliibuka na wingi wa viti 96 bungeni.

Miaka nenda, miaka rudi kati ya chaguzi kuu 14 za Uingereza nilizozishuhudia zilikuwapo zilizosisimua. Lakini sijapatapo kuuona uchaguzi uliosisimua zaidi kama wa wiki iliyopita. Hayo si ya ajabu kwani siasa za Uingereza zinapita katika msimu wa msisimko mkubwa, msisimko wenye kuchangamsha na unaochemsha bongo. Hujui kutatokea nini kesho na inapofika hiyo kesho huzuka jipya la kushangaza au la kukufanya upigwe na bumbuwazi.

Theresa May alipotangaza kwamba patafanywa uchaguzi wa ghafla Juni 8, wachambuzi wengi, na hasa wale wa vyombo vya habari vyenye kukikunga mkono chama cha Conservative, walianza kumchambua Jeremy Corbyn, kiongozi wa Leba.

Lengo lao lilikuwa kumfanya Corbyn aonekane kuwa ni kichekesho. Walimkebehi, walimdharau na walijaribu kumfanya karagosi. Walisema kwamba hana sifa za kuliongoza taifa na wala hana haiba anayostahiki kiongozi awe nayo.

Walikuwako wengi walioshika majembe mikononi kumchimba Corbyn. Kwanza, hao wachambuzi wa vyombo vya habari, halafu mahasimu wake wa vyama Conservative na Liberal Democrats na hata baadhi ya wabunge wa chama chake mwenyewe cha Leba. Waliamini kwamba hachaguliki na walitumai kwamba wataweza kumchimba na kumzika mzimamzima. Walikosea.

Wapiga kura wa Uingereza walifikiri vingine. Walimuona Corbyn kuwa ni mtu wa kuaminika, mwenye msimamo kinyume na alivyo May. Vijana nao wakajitokeza kwa mkururo kumuunga mkono. Vijana walikuwa wakilipiza kisasi. Kwa maoni yao wazee waliwauza kwa kupiga kura katika kura ya maoni kupendelea Uingereza ijitoe kutoka Muungano wa Ulaya.

Wengi wa vijana wangependelea Uingereza ibakie ndani ya Muungano hayo. Wengi wa vijana pia wamevunjwa moyo na sera za kibepari, sera zilizoyafanya maisha yao yawe magumu hasa kwa upande wa umiliki wa nyumba. Corbyn anawavutia vijana kwa sababu ya msimamo wake na sera zake za kisoshalisti.

Kwa upande mwingine, vijana wamempa mgongo Theresa May. Wanamuona kuwa ni mtu wa ajabu. Ni aina ya mwanasiasa mwenye kuwatukanisha wanasiasa wenzake, na mwenye kuzitukanisha siasa. Hufanya hivyo kwa unafiki wake. Ameonesha wazi kwamba hutetea mambo asiyoyaamini ilimradi aweze kuendelea kuwa waziri mkuu. Anavutiwa zaidi na madaraka badala ya misimamo ya kisiasa.

Wakati wa kura ya maoni iliyoamua iwapo Uingereza ibakie ndani ya Muungano wa Ulaya (EU) au itoke, May alikuwa miongoni mwa mawaziri wazito waliomuunga mkono kwa nguvu waziri mkuu wa siku hizo David Cameroon kwamba Uingereza ibakie ndani ya Muungano huo.

Baada ya Uingereza kupiga kura kuwa ijitoe kutoka EU, May akajifanya yeye kuwa ndiye mshika bendera wa wenye kuweka masharti magumu ya kujitoa. Tatizo lake ni kwamba kila ukimsikiliza akizungumzia mchakato wa kujitoa kutoka EU unajikuta unamsikiliza mtu asiyeamini kwa dhati kuwa ni busara kujitoa. Ndiyo maana akionekana kuwa ni mtu asiyejua anasema nini. Akiulizwa aeleze mchakato wa “Brexit” ni nini, hujibu tu kwamba “Brexit maana yake Brexit”. Akiambiwa afafanue, hawezi. Wala hawezi kusema anakusudia nini.

Jengine lililomponza May ni kwamba akionekana kuwa ni mtu mwenye kiburi. Akijiona kuwa yeye ni yeye na hakuwa mnyenyekevu.

Tangu awe waziri mkuu May amekuwa akipigania jambo ambalo yeye anahisi linawaunganisha wananchi wote wa Uingereza lakini ambalo kwa kweli halina gundi madhubuti ya kuwaunganisha. Jambo lenyewe ni uamuzi wa kujitoa EU. Matokeo ya kura ya maoni ya mwaka jana kuhusu Uingereza kujitoa yana mushkili wake. Ingawa asilimia 52 ya wapiga kura walitaka Uingereza ijitoe, walifikia uamuzi huo kwa kutishwa, kudanganywa na kupewa ahadi za uongo.

Nyingi za ahadi hizo zilikuwa za kitoto kama ile ya kwamba Uingereza inaweza ikatoka lakini wakati huo huo ikaendelea kufaidika kama ingekuwa bado mwanachama wa EU. Wanataka mambo yabadilike na wakati huohuo yaendelee kuwa kama zamani. Kwa ufupi, wanasiasa wa sampuli ya May walipokuwa wakiulizwa na wenzao wa EU nini wanachotaka, hawakuweza kujibu kwa ufasaha.

Yote hayo yamemfanya May aonekane kuwa ni kichekesho na hasa na wakuu wa EU jijini Brussels. Alikuwa na wingi wa wabunge kuweza kupitisha miswaada yake lakini akitaka awe na wingi mkubwa zaidi ili aonekane kuwa ni kiongozi madhubuti.

Ninavyohitimisha makala haya naona kuna hali ya wasiwasi iliyotanda Uingereza. Kuna mengi tusiyoyajua. Hatujui serikali ya sasa ya May itadumu kwa muda gani kabla haijaporomoka. Hatujui akianguka May, atachomoza nani ndani ya chama chake kushika usukani wa kukiendesha.

Hatujui serikali ya sasa ya May itashirikiana vipi na chama cha Democratic Unionist Party (DUP) cha Ireland ya Kaskazini kwa vile ushirikiano huo unaweza ukayaathiri Mapatano ya Amani ya Ireland ya Kaskazini.

Hatujui wabunge kutoka Uskochi wa chama chake Theresa May watampa masharti gani au watatoa madai gani kwani May asingeliweza kujaribu kuunda serikali mpya lau asingekuwa na wabunge hao kutoka Uskochi.

Hatujui nchi hii itataka nini hasa itapokuwa inaanza mashauriano ya mchakato wa kujitoa kutoka Muungano wa Ulaya. May ameitia mtegoni Uingereza.

raiamwema

Share: