Makala/Tahariri

YA ‘CCM-DOLA’ NA SIASA ZA ‘WATENDE WAO!’

Na: Mwandishi Maalum

Wahenga wa Waswahili walipata kusema; ‘Watende wao, wakitenda wenzao, huwa mwao!’ Kwa kuwa Waswahili wana utajiri wa methali na misemo, msemo huu wa ‘Watende wao’ ukapata kushereheshwa zaidi kwa msemo mwingine wenye mantiki na umaizi kama huu pale wahenga waliposema tena kuwa; ‘Kunya anye kuku tu, akinya bata huambiwa kaharisha!’
Misemo hii itakuwa kiini cha mjadala wangu katika makala hii inayonisukuma kuandika mada yenye kichwa cha habari kinachoonekana na kusomeka hapo juu. Kwa nini naandika hivi? Wacha kwanza niwarudishe kwenye historia fupi.

Inafahamika kwamba Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano iko chini ya utawala wa CCM. Ingawa kwa upande wa Zanzibar kuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoundwa na CCM na CUF, nguvu na mamlaka ya CCM bado ni makubwa. Ni makubwa kwa sababu CCM ndio dola. Na zaidi ya habari, CCM ndicho chama chenye kushika hatamu nchini. Ndio chama chenye kushika mpini.
Lakini pamoja na kuwa CCM ndiyo inayoshika mpini wa dola, katika nchi ya kidemokrasia, inayojivunia amani, utulivu na utawala bora, haijuzu wala haileti maana njema kusema kuwa CCM ina mamlaka au uwezo wa kufanya itakalo, eti tu, kwa kuwa imeshika mpini. Hivi sivyo, ingawa ndivyo ilivyozoeleka katika kipindi chote cha miaka 50 ya CCM ikiwa madarakani.
CCM kwa kuamini wameshika mpini, wamejipa mamlaka ya kufanya watakalo, watakavyo, kwa watakaye, mahala na saa watakazo. CCM kwa kujivisha mwavuli na magwanda ya dola, ina uwezo wa kuleta fujo, kupiga watu, kujeruhi, kufanya ufisadi, kumtukana yeyote mkubwa mdogo, kiongozi na raia wote hapana anayejaliwa na mtu. Haya yote ni kwa uchache tu. Ila kwa ufupi, CCM wana uwezo wa kufanya lolote wala lisiwe kosa kisheria wala kikatiba.

Cha ajabu, watende wao tu, wakitenda wenzao hata yasiyokuwa mabaya, ilimradi hayawafurahishi tu hata kama ni ya ukweli na ni ya haki na ya kisheria, basi kwa wao huwa mwao. Akitokezea mtu au kikundi cha watu wakafanya lolote tu dhidi ya utashi wa CCM jambo hilo huwa kosa na haliwi kosa dogo. Adhabu, mateso na vitimbi vyao dhidi ya wasiowaunga mkono wao, hupitiliza visa vya firauni au Adolf Hitler dhidi ya Wayahudi. Yote haya, ni kwa sababu ile ile: CCM ndiyo Dola. Iko juu ya sheria!
Nasema CCM iko juu ya Sheria kwa sababu matukio mengi yanayofanyika nchini yanathibitisha kauli hiyo. Tuanze kwa machache yaliyo wazi. Wako wapi wana Uamsho hivi leo? Chambilecho Balozi Seif Ali Idi, wako huko ‘wananyea ndooni!’ Kwanini Uamsho wanyee ndooni? Jibu liko wazi: kwanza ni Waislamu. Pili, waliapa kuuamsha uma na kupigania uhuru wa Zanzibar ndani ya Muungano. Hilo kweli kosa? Lakini kwa vile wametenda dhidi ya Dola, leo hii Uamsho yanawakuta ya kuwakuta huko bara. Hilo moja.
Hivi karibuni tulishuhudia vijana kadhaa wa CUF wakijeruhiwa vibaya kwa mapanga na vitu vyenye ncha kali wakati wakirudi mkutanoni Makunduchi. Wengi wa hawa, wamekuwa walemavu wa kudumu na wengine watakufa na makovu yasiyofutika kwa tukio hili.

Waliofanya vile yaaminika kuwa ni vijana wa ‘Janjaweed’ waliokuwa katika gari la wazi la mmoja ya Viongozi wa jimbo la Bububu. Tukasema sana juu ya tukio hili. Lakini kwa kuwa waliofanya vile ni ‘watu wao’ hili nalo halikuwa kosa wala hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya wahalifu wale wa Janjaweed. Watende wao hao!
Kati ya Tarehe 20 na 21 mwezi wa tano, mwaka huu, tumeshuhudia kiongozi wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF), Wilaya ya Mkoani Bwana Said Ali, akikamatwa na Polisi na kusafirishwa hadi Unguja kwa meli ili kwenda kujibu mashitaka ya kumkashifu Balozi Seif Ali Idi.

Nchi yetu inatajwa kuwa imekubali na kupitisha azimio la haki za Binadamu. Na moja kati ya haki hizo ni haki ya kujieleza na kutoa maoni huru. Alichokifanya Bwana Said Ali ni kutoa maoni yake na hisia zake tu na sio chengine. Sasa kwa vile aliyemsema ni Dola, na kama nilivyokwishatangulia kusema CCM- Dola Iko juu ya Sheria, Said Ali akatiwa hatiani.
Cha kushangaza, kosa lolote atakalokuwa nalo Said Ali, basi naamini mahakama zipo za kutosha Pemba za kumshitaki. Hapakuwa na haja ya kumsafirisha kwenda naye Unguja bure kama kweli nchi hii inafuata misingi ya utawala bora na utawala wa sheria. Lakini kwa kuwa waliofanyiwa ni wale wale ‘watende wao’ alichokisema Said Ali dhidi ya makununu ya Balozi Seif Idi, kimekuwa mwao! Naye siku si nyingi, tutamsikia Balozi Seif Idi akisema ‘ananyea ndooni!’.

Nilifuatilia sana kisa cha Said Ali na kwa hakika sijaona kama alikosea kiasi cha kusafirishwa kama haini kwenda Unguja kuhukumiwa. Kwa ufupi alichokisema Said kama Mwenyekiti wa JUVICUF ni kuwa Balozi Seif Idi asije Pemba kufanya MIKUTANO kwa kile anachodai kuwa Balozi alizuia wafuasi wa CUF kwenda mikutanoni mashamba. Hilo ndilo la Said kwa watawala wetu, CCM-DOLA.
Kinachoshangaza zaidi, kama unafuatilia hutuba za Borafya na Shaka Hamdu Shaka, utaona kuwa hotuba zao zote wanamtukana Maalim Seif, tena matusi ya nguoni. Borafya amefikia kumtukana Maalim matusi yasiyosemeka, tena hadharani. Tena kwa kumhusisha na ahali ‘Sunsumiya’ moja kwa moja. Hilo halikutosha, katika mkutano wa Kiembe samaki, Shaka Hamdu, mbele ya Balozi Seif Idi, alikuwa akimtaja Maalim Seif, ambaye ni makamo wa kwanza wa Rais, kwa jina la ‘MAUDODO!’ kuanzia mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake.

Nilijaribu kufuatilia maana ya neno ‘Maudodo’ nikaambiwa kwa lahaja ya Kingazija neno hili lina maana ya ‘mamdogo!’ Sina uhakika kama hiyo ndiyo maana yake halisi. Pia sina hakika kuwa ndiyo maana aliyokusudia Shaka lakini kwa kilugha na kimantiki, neno hilo lina maana ya kumdhalilisha Maalim Seif Sharif Hamad, moja kwa moja.

Kama kawaida ya watende wao, kwa vile aliyesema hayo ni Borafya na Shaka, hili halikuwa kosa. Kosa likawa la Said tu. Kwa maana nyepesi, hapa utaona kuwa; kumdhalilisha Makamo wa kwanza wa Rais hadharani sio kosa lakini kumsema Makamo wa Pili wa Rais ni kosa la uhaini au kosa la jinai. Haya ndiyo yale yalee; ‘Kunya anye kuku, akinya bata anaharisha!’
Mfano mwingine, hivi juzi juzi tu, yaani wiki moja iliyopita, wananchi wa kijiji cha Kwale, Micheweni , Pemba ambao ni wakereketwa halisi wa chama tawala, walijaribu kuiteremsha bendera ya CUF iliyokuwa imepachikwa pale na mwanachama mmoja wa chama hicho. Hoja yao kuu ya kutaka kuishusha bendera hii walidai kuwa hawataki ‘CUF’ katika kijiji chao. Hivi hii ni hoja sahihi kisheria?
Nini basi kilitokea? Mwenye bendera ya CUF alipoona wanakijiji wanataka kuishusha bendera, alitoka na panga akawaonya kuwa atakayesogea kuishusha bendera hiyo, atakiona kilichomfanya punda asiote nundu. Kifo si swahiba mwema. Wakereketwa wale walipoona hali imekuwa ngumu, waliita Polisi. Polisi walipofika walipiga risasi juu na kumtishia mwenye kupachika bendera. Akakimbia. Hapo kwa msaada wa Dola, bendera ya CUF ikashushwa juu ya mlingoti na wana CCM-DOLA wa Kwale.

Habari hii ilipowasilishwa bungeni siku iliyofuata, wahusika wote wakachukuliwa na Polisi na kuswekwa rumande huko Wete. Kati ya hao waliokuwamo ni Afisa Elimu Wilaya ya Micheweni Mbwana Shaame Hamad, Afisa wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Micheweni Bwana Khamis Massoud na Mwalim Mkuu skuli ya Shumba mjini Mwalim Bakari.
Kuwekwa ndani kwa wana dola hawa ambao wanashika nyadhifa nyeti za Serikali, hakukudumu masaa. Siku ya pili tu tangu watiwe mbaroni, kauli ya Balozi Seif Idi ilitumwa kwamba watolewe mara moja. Watuhumiwa hao, kwa amri ya Makamo wa Pili wa Rais, wakaachiwa huru huku ikisemwa kesi yao itasikilizwa wakiwa nje kwa dhamana.

Wananchi wenzangu, hebu tukae chini tutafakari: ingekuwa waliofanya jaribio hili ni waumini wa chama chengine au tuseme wapinzani, ingekuwaje? Jawabu utakalolipata, malizia na ujumbe wangu; ‘Watende wao, wakitenda wenzao huwa mwao!’ Na kwa hali kama hii – Je, tutafika?

Tagsslider
Share: