Makala/Tahariri

Zanzibar inahitaji mchango wa CUF

Kwa hali ilivyo mpaka sasa, ni dhahiri shahiri chama kikuu cha upinzani CUF visiwani Zanzibar, katika msimu huu hakitokuwamo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) itakayoundwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu ujao wa marudio.

Kwani, mpaka sasa chama hicho kimeendelea kushikilia msimamo wake wa kutoshiriki katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika hapo Machi 20, mwaka huu, huku kikienda mbali zaidi kwa kuchukua hatua ya kuiiandikia barua Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) visiwani humo ya kutaka kuondolewa kwa majina ya wagombea wake katika fomu za kupigia kura.

Ombi ambalo ZEC imesema halikufuata taratibu za kisheria na hivyo kusisitiza kuwa majina ya wagombea wa CUF na vyama vilivyotangaza kujitoa yataendelea kuwamo katika karatasi za kupigia kura kama ilivyo kuwa hapo awali katika uchaguzi uliofutwa mwezi Octoba mwaka jana.

Hata kama ZEC itaendelea kuyaacha majina ya wagombea waliojitoa, haitarajiwi kwa wafuasi wa chama cha CUF kwenda vituoni kupiga kura siku hiyo ya uchaguzi, kwani walishatangaziwa na viongozi wa CUF wasifanye hivyo.

Hali hiyo ya kujitoa kwa vyama vingine na hususan CUF, kunatoa mwanya kwa CCM kuingia ulingoni na wagombea dhaifu wa vyama ambavyo vimeendelea kuonyesha nia ya kushiriki uchaguzi huo.

Huku pia CCM kikipata mwanya wa kumtafuta mshirika, mara hii tofauti na CUF ili kuungana naye na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ipo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika mabadiliko yake ya mwaka 2010.

Hali ya mambo jinsi ilivyo, chama cha upinzani kitakachoshirikiana na CCM msimu huu katika Serikali hiyo ya SUK, bila shaka kitatazamwa kama chama kilichokosa sifa stahiki ya kuwa mwakilisha wa wengi wa Wazanzibar wasiopikika chungu kimoja na CCM pamoja na sera zake.

Hali hiyo inaakisiwa na utofauti wa sera, itikadi na mienendo ya vyama hivyo vya upinzani, vitu ambavyo hutoa taswira halisi ya kipi ni chama halisi cha upinzani, huku chama cha CUF huonekana kuvipiku vyama vingine vyote vya upinzani.

Kwani sera, itikadi na mwenendo wa CUF ndio huwavutia Wazanzibari walio wengi na wao kuamini kuwa ili visiwa hivyo visonge mbele katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, basi CUF ndiyo tiba mbadala tofauti na vyama vingine kikiwamo cha CCM.

Hivyo basi, linapokuja suala la ushirika maridhawa ndani ya SUK, vyama vya CUF na CCM ndivyo vinaonekana kuwa sahihi zaidi na hata bila kujali chama kipi ndiyo kimemtoa Rais wa visiwa hivyo.

Mtazamo huo unatokana na wingi wa wafuasi vyama hivyo vilivyo nao, kama inavyokuwa ikishuhudiwa katika matokeo mbalimbali ya chaguzi visiwani humo, ambako kwa takribani vipindi vyote vya uchaguzi, kumekuwepo na tofauti ndogo ya kura baina ya vyama hivyo.

Suala siyo wingi wa wafuasi wa vyama hivyo, bali ni tofauti zinazopelekea kila chama kikawa na wingi huo wa wafuasi, tofauti kama na Tanzania bara, utofauti uliopo baina ya wafuasi wa CUF na CCM visiwani Zanzibar ni wa kipekee na usio katika hali rahisi ya kutanzuliwa.

Kwani utofauti huo umejikita zaidi katika masuala tata na nyeti yanayotokana na historia ya visiwa hivyo, kama matukio ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na lile la Muungano baina yake na Tanganyika mwaka huo huo.

Pamoja na mambo mengine, matukio hayo kwa kiasi kikubwa yamewagawa watu wa ndani na hata nje ya visiwa hivyo na kupelekea hali ya kushindwa hata kuvumiliana kisiasa na kufikia hata hatua ya kujeruhiana na kubaguana katika sekta mbalimbali.

Mfano tukio kama la Mapinduzi ya Zanzibar linatazamwa na baadhi ya Wazanzibar kuwa lilikuwa ni la ubaguzi wa rangi hususan dhidi ya waarabu kutoka kwa watu weusi, huku la Muungano likionekana kuwa lililenga kupeleka ‘ukoloni’ katika visiwa hivyo kutoka Tanzania bara (zamani Tanganyika).

Hali hiyo ya siasa za uhasama mkali kwa kiasi kikubwa ilikuja kupata ahueni mara baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, huku Chama cha CUF kikiwa ni mshirika mkubwa wa uundwaji wa Serikali hiyo kupitia kwa Maalim Seif aliyefanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume hapo mwaka 2009.

Ila kwa bahati mbaya, sasa hivi chama cha CUF kilichoshirikiana na CCM katika kuijenga Zanzibar yenye utulivu na uvumilivu wa kisiasa kupitia SUK, katika awamu hii ni kama kimetupwa nje ya duara hilo la Zanzibar isio kuwa na uhasama wala chuki.

CUF ni kama kimetupwa nje ya duara hilo, kwani jitihada zake zote za huku na kule ili kuhakikisha mkwamo wa kisiasa unamalizwa kwanza kabla ya hatua zingine, zilizimwa ghafla.

Jitihada hizo zilizimwa na kufanya chama cha CUF ‘kuwekwa kando’ mara baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kutangaza tena uchaguzi wa marudio, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ‘akibariki’ zoezi liendelee kinyume na matarajio ya wengi.

Kwa msingi huo wa ‘kuenguliwa’ kwa Chama cha CUF kinachoamini uchaguzi ujao ni batili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni kama inaelekea kuwa ya uwakililishi wa chama kimoja kwenye Serikali na Bunge kwani hakuna chama kingine chenye wafuasi wengi kama CUF.

Hali hiyo pia, inaelekea kuiua ile dhana ya ujumuishi (inclusion) iliyopatikana katika Serikali ya SUK, kwa minajili ya kuwafanya watu wote wa Zanzibar wajihisi kila mmoja anawakilishwa ndani ya Serikali na kuondokana na hisia za kubaguliwa.

Dalili tosha ya visiwa hivyo kurejea kule kule vilivyotoka katika siasa za uhasama na chuki na hivyo kuzidi kuzorota katika kupiga hatua mbele za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali.

Hivyo basi kwa hali ya kisiasa ilivyo Zanzibar, Chama cha CUF bado ni sehemu muhimu ya amani na utulivu wa visiwa hivyo, hakikupaswa kutengwa hata kidogo, kwani nyuma yake kuna wafuasi karibia sawa na wale wa CCM wenye mitazamo mikali inayokinzana.

Zanzibar haipaswi kuchukua mkondo wa watu wenye mtazamo mmoja katika ujenzi wake, kwani raha ya ujenzi wa taifa ufanywe na wananchi wake wote walioko katika makundi na mitazamo tofauti, huku wakiwa hawana uhasama wala chuki.

mwananchi

Share: