Makala/Tahariri

Zanzibar ya Sheikh Karume haikuwa na ubaguzi huu

Muhariri wetu Ahmed Rajab

KUNA mengi ambayo Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalikusudia kufanya na hayakufanyika. Miaka 50 baadaye Mapinduzi hayo yamechakaa, yamezeeka na yameshindwa kutimiza ahadi zake.

Wapo wenye kushikilia, tena kwa inadi, kauli mbiu ya ‘Mapinduzi Daima’ lakini kwa hakika, ukiitathmini kwa undani kabisa utaona kwamba kauli mbiu hiyo ni kama mlio wa debe tupu. Una ghasia na vishindo vingi lakini debe halina kitu.

Yote ambayo Mapinduzi hayakuyatimiza yalikuwa mambo adhimu kwani Mapinduzi hayo yalikuwa na malengo adhimu. Hilo halina shaka.

La msingi katika hayo ni azma ya kuondosha ubaguzi wa kila aina na kuleta usawa katika jamii. Wazanzibari wa kawaida walifanikiwa kuacha kubaguana wao wenyewe kwa wenyewe. Ajabu ya mambo na kwa bahati mbaya ubaguzi bado umewavaa baadhi ya wakubwa hasa wahafidhina walio ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Huu ndio ukweli wa hali ya mambo ilivyo.

La kusikitisha ni kuwaona wabaguzi hao wenye kutumia lugha chafu wanapowabagua kikabila wananchi wenzao katika majukwaa ya CCM wanavumiliwa uanachama na chama chao ilhali wanayoyahubiri yanakwenda kinyume kabisa na sera rasmi za chama hicho.

Miaka 50 baada ya Mapinduzi, ambayo moja ya malengo yake yalikuwa ni kuleta usawa, bado watu wa makabila fulani wanabaguliwa wasishike nyadhifa fulani au kazi fulani, kwa mfano katika majeshi au polisi. Wanafanyiwa ngumu hata katika kupatiwa misaada ya kwenda nje kusoma. Hivi sivyo mambo yalivyokuwa katika miaka ya mwanzo ya Mapinduzi. Hali ilianza kubadilika kuanzia Aprili 1972, baada ya kuuawa Rais wa kwanza Sheikh Abeid Amani Karume. Hapo ndipo palipozuka ule usemi wa“mtoto wa nyoka, nyoka” usemi ambao ulizidi kushadidia ubaguzi.

Na kuushadidia zaidi pakatungwa nyimbo na kwaya ya Jeshi, chombo ambacho kiliundwa kulilinda taifa na raia zake, iliyosema “mtoto wa nyoka ni nyoka; kamata, chinja.”

Hali haikuwa hivi wakati wa utawala wa Karume. Kweli haki za binadamu zilikiukwa na kulikuwa viroja vingi lakini hapakuwa na ubaguzi wa aina hii. Si hivyo tu lakini kuna mashahidi wasemao kwamba katika siku za mwisho za uhai wake Karume alikuwa akifikiria kutoa mwito kwa Wazanzibari waliokimbia nchi warudi kusaidia kuijenga nchi yao na kwamba alikuwa na hamu kubwa papatikane umoja miongoni mwa Wazanzibari.

Madhara yanayoweza kusababishwa na serikali yenye kuwabagua raia zake ni makubwa mno. Tumeona, kwa mfano, jinsi ubaguzi ulivyowafanya watu wenye ujuzi waihajiri nchi yao kwa mkururo baada ya 1972. Si kwamba walipenda kufanya hivyo isipokuwa hawakuwa na hila kwa vile walinyimwa fursa ya kuweza kuendeleza maisha yao kwao.

Baadhi yao wakahamia Bara. Ujuzi na maarifa yao yalichangia kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo huko Bara hasa sekta ya elimu kwani walimu wengi walilazimika kuhamia Bara walikopokelewa kwa mikono miwili. Hasara ilikuwa ya Zanzibar.

Wengine walivuka mipaka mingi zaidi na kuishia nchi za ng’ambo ya bara la Afrika.

Baada ya kumalizika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi sasa ni wakati wa kuangalia kwa dhati mustakbali wa Zanzibar. Ni wakati wa kuanza kuachana na mabaya ya nusu karne iliyopita na kuchukua hatua zitakazoiwezesha Zanzibar iwe na mustakbali mwema hasa kwa vile karibu inatazamiwa kuwa na mfumo mpya wa uhusiano wake na Tanganyika.

Moja ya hatua za mwanzo zinazopaswa kuchukuliwa ni kuirekebisha Katiba ya Zanzibar ili izifanye taasisi muhimu za dola kama vile mahakama na polisi ziweze kutekeleza kazi zao bila ya kuingiliwa na wanasiasa wakiwa wakuu wa serikali.

Njia moja, kwa mfano, ya kuepusha hayo ni kuyazima kwa kuyapunguza madaraka ya Rais na kuyahamishia baadhi ya madaraka yake kwenye Baraza la Wawakilishi, chombo kikuu cha utungaji sheria. Hatua hiyo itasaidia kuushirikisha umma katika shughuli za uamuzi wa utawala.

Lakini umma hautoweza kushirikishwa kikamilifu isipokuwa kwanza serikali na utawala wake umfanye kila Mzanzibari athaminiwe kwa Uzanzibari wake na kwa mchango wake wa kusaidia kuistawisha jamii. Ili hilo litimizwe lazima ubaguzi wa aina zote — wa kikabila, kidini, kisiasa na wa kijinsia — upigwe vita na taasisi zote za serikali ziwe na sura halisi ya mchanganyiko wa Zanzibar.

Kwa ilivyo hivi sasa hata hii Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopo haina ubia unaostahiki. Hali yake ni kinyume na ilivyokuwa katika miezi ya mwanzo ya Mapinduzi ambapo makada wa vyama vyote viwili vilivyoshiriki kufanikisha Mapinduzi yaani Afro-Shirazi Party (ASP) na Umma Party walipewa dhamana za kusimamia majukumu mbalimbali.

Ingawa Umma Party sicho kilichoyaasisi Mapinduzi lakini kwa kuyaunga mkono na kwa kujitolea mhanga kuyasaidia makada wake waliingizwa katika Baraza la Mapinduzi na katika Baraza la Mawaziri.

Wengine waliteuliwa wakuu wa wilaya na mikoa, walikuwa katika ngazi za chini hata za juu katika majeshi na katika Idara ya Uhamiaji na kuna walioteuliwa mabalozi au kushika nyadhifa nyingine za kidiplomasia.

Baada ya Muungano kuundwa baadhi ya makada hao wa Umma Party walihamishiwa Bara kuitumikia Serikali ya Muungano na Jumuiya ya Afrika Mashariki ya wakati huo. Huo ulikuwa ushirikiano wa dhati na uliojenga umoja wa kitaifa.

Serikali hii ya sasa ina kasoro kubwa. Ubia wake unaishia kwa mshirika mdogo kupewa umakamu wa Rais na wizara. Katika ngazi za chini bado uteuzi unaendelea kuzingatia ukereketwa wa chama cha Rais ambaye ndiye mwenye kufanya uteuzi huo.

Awali, kulikuwa na tetesi kwamba angefanya uungwana wa kuwateua angalau wakuu wa mikoa michache kutoka upande wa pili. Lakini, kwa sababu azijuazo mwenyewe, hakufanya uteuzi huo.

Taksiri hii imechangia katika kuwachagua watu wasio na sifa zinazostahiki kushika baadhi ya nafasi zilizo nyeti na hivyo kusababisha utendaji wa idara zao uzorote. Na vilevile uteuzi wa aina hiyo umezidisha chuki na kupunguza imani miongoni mwa jamii kwamba kweli kuna mshikamano wa dhati wa kuendeleza maridhiano.

Haya maridhiano yameweza kufika hapa yalipo kwa sababu msingi wake mkuu umejengwa kutokana na uamuzi wa kijasiri wa wengi wa Wazanzibari katika kura ya maoni ya 2010 walipoamua kuzizika tafauti zao za kisiasa na kuiweka Zanzibar kwanza.

La kusisitiza hapa ni kwamba ni kauli hiyo ya Wazanzibari iliyowanyamazisha wahafidhina na vichwa mchungu ambao hadi leo nia yao ni kuyatia munda maridhiano haya.

Sherehe za mwaka huu za kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi zimethibitisha kwamba hatimaye wengi wa kizazi cha sasa cha Wazanzibari wameyakubali. Ni mjinga tu atayethubutu kusema kwamba kuna wenye kutamani kurejesha utawala wa Kisultani visiwani Zanzibar.

Shtuma hiyo ni kisingizio kikubwa kinachotumiwa na wahafidhina na wanasiasa wasiojiamini wenye kuupotosha ukweli. Na kimekuwa kikitumiwa kama fimbo ya kuwachapa wale ambao wahafidhina wanataka kuwabagua.

Si kwamba hawakuwako waliopinga au waliolalamika kwa kufanywa sherehe hizo. Walikuwako na walikuwa na sababu zao.

Kuna walionung’unika kwamba gharama za sherehe zilikuwa kubwa mno na kwamba fedha zilizotumika zingelitumika kwa mambo ya maana zaidi. Kuna waliolalamika kuwa ni dhambi kusherehekea mauaji kwa vile Mapinduzi yalisababisha vifo vingi vya watu wasiokuwa na hatia.

Kuna waliosema hawaoni sababu ya sherehe hizo kwani hakuna cha kusherehekea kwa vile miaka 50 baada ya Mapinduzi hakuna maendeleo ya maana yaliyopatikana. Kuna waliosema kwamba hakuna cha kusherehekea kwani Mapinduzi yalipoteza lengo lake na badala yake yalizalisha tabaka jipya la wachache waliofaidika na hayo Mapinduzi.

Lakini kwa namna wananchi walivyoshiriki katika sherehe hizo kumetoa changamoto kwa utawala uyatimize yale yaliyokuwa matarajio ya Mapinduzi yenyewe. Njia ya kufanya hivyo ni kurekebisha Mapinduzi yalipokwenda kombo.

raiamwema

Share: