Makala/Tahariri

Z’bar yaanza kumponza Magufuli

Ahmed Rajab Toleo la 434 2 Dec 2015

WIKI iliyopita Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) liliionya Tanzania kuwa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar usipotanzuliwa na Tanzania isipotoa ufafanuzi wa sheria yake ya uhalifu wa mtandaoni basi shirika hilo litainyima Tanzania msaada wa dola za Marekani milioni 472. Hizi ni fedha ambazo Tanzania inazihitaji sana kuendeleza mradi wake wa nguvu za umeme.

Onyo hilo la MCC lilikuwa katika barua ya Novemba 19, aliyopelekewa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Tanzania, Dk. Servacius Likwelile, na Jonathan Bloom, Naibu Makamu wa Rais wa MCC anayeshughulikia miradi ya Afrika. Ingawa barua hiyo iliandikwa kwa upole na kwa lugha ya kidiplomasia, ujumbe wake ni wazi: Tanzania lazima ifuate misingi ya demokrasia na iheshimu uhuru wa kutoa mawazo.

Kwa ufupi, Tanzania inawajibika kuonyesha dhamira ya kuwa na utawala bora.
MCC huzisaidia nchi zilizo masikini duniani ziondoe umasikini wao lakini kwa masharti. Sharti la kwanza ni kwamba nchi hizo ziwe na utawala bora, la pili ziwe zina uhuru wa kiuchumi na la tatu ni kwamba nchi hizo ziwe zinawekeza kuwaendeleza raia zao.

Nchini Tanzania, shirika la MCC linajishughulisha zaidi na miradi ya kuwapatia maelfu ya wananchi umeme wa kisasa pamoja na kujenga na kuzitengeneza barabara zitazosaidia usafirishaji wa mazao kutoka mikoani na hivyo kusaidia kuunyanyua uchumi wa nchi.

Barabara zilizokwishajengwa kwa msaada wa MCC ni zile za Tunduma hadi Sumbawanga, Tanga hadi Horohoro na ile ya Namtumbo kuelekea Songea hadi Mbinda.

Zilipoanza fununu kwamba serikali ya awamu ya nne ilikuwa na mpango wa kutunga sheria kali dhidi ya uhalifu wa mtandaoni palikuwa na hofu kwamba sheria hiyo huenda ikatumiwa vibaya. Hofu iliyokuwako ni kwamba ama itatumiwa kuwaziba mdomo wapinzani na wakosoaji wa serikali au itatumiwa kuyaziba madudu ya serikali yasitangazwe katika vyombo vya habari na majukwaa ya mawasiliano ya kijamii.

Hatua zote hizo zilionekana kuwa na athari ya kuuzima uhuru wa watu kutoa maoni yao.

Shirika la MCC nalo pia lilikuwa na wasiwasi kwamba sheria hiyo ya uhalifu wa mtandaoni huenda ikatumiwa vibaya, kama kisingizio cha kuyakaba mawazo huru. Shirika hilo lilipeleka ujumbe Tanzania kulifuatiliza suala hilo.

Wahusika serikali waliuhakikishia ujumbe huo kwamba hapatotungwa sheria mbovu ya uhalifu wa mtandaoni na kwamba itapotungwa, sheria hiyo haitotumiwa vibaya kwa kuuminya uhuru wa mawazo.

Kukamatwa kwa watu kadhaa, raia na wasio raia wa Tanzania, chini ya sheria hiyo mpya ya uhalifu wa mtandaoni kumelitia wasiwasi shirika la MCC. Kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar katikati ya zoezi la kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo ni hatua iliyozidi kulitia wahaka shirika la MCC.

Hamna shaka yoyote kwamba barua hiyo ya MCC imemtia dosari Rais John Magufuli, aliyeanza utawala wake wa awamu ya tano kwa kasi inayopigiwa mfano ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Hatua alizozichukua hadi sasa ni hatua zinazomfanya aungwe mkono hata na baadhi ya wapinzani wake.

Wengi wako tayari kuendelea kumuunga mkono ilimradi asiwe anazipinda sheria au kwenda kinyume na Katiba. Hatua zake tayari zimemfanya awe kama aliyempiku Rais aliyemtangulia, Jakaya Kikwete.

Magufuli amekuwa akitenda mambo kana kwamba anauonyesha ulimwengu ya kuwa amekamia kuusafisha uoza wa serikali ya awamu ya nne.

Hata hivyo, onyo la Marekani kupitia shirika lake la MCC ni ushahidi wa kutosha kwamba mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar umekwishaanza kumponza. Na Magufuli atazidi kujipalilia moto ikiwa ataendelea kukaa kimya akiwanyamazia wachache wa huko Zanzibar walioivunja sheria na kuikiuka Katiba ya Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mpaka sasa ni Marekani pekee iliyotangaza hadharani nia ya kuichukulia hatua Tanzania endapo mgogoro wa kikatiba wa Zanzibar hautomalizwa kwa kukamilisha zoezi la kutangaza matokeo yaliyoyabaki ya uchaguzi mkuu wa huko na kutangazwa kwa aliyeshinda urais wa Zanzibar. Hilo pia ndilo takwa la nchi kadhaa wafadhili wa Tanzania, ikiwemo Uingereza.

Raia Mwema limearifiwa jijini London kwamba serikali ya Uingereza inalishughulikia kwa dhati suala hilo. Hivi majuzi Wazanzibari wanaoishi Uingereza waliruhusiwa waandamane nje ya ofisi na makazi ya Waziri Mkuu David Cameroon, 10 Downing Street.

Kadhalika, mwakilishi wa waandamanaji hao aliruhusiwa mlangoni mwa ofisi hiyo ili akabidhi risala maalum. Risala hiyo iliisihi serikali ya Uingereza, kwa kushirikiana na jumuiya nyingine za kimataifa, “ichukue hatua kali dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania endapo watawala wa Zanzibar wataendelea kuyapuuza maombi ya jumuia ya kimataifa yanayowataka watangaze matokeo yaliyosalia ya uchaguzi uliofanywa Zanzibar Oktoba 25, 2015.”

Siku chache baadaye maandamano mingine yalifanywa na Wazanzibari waishio Marekani mbele ya Ikulu ya White House, jijini Washington.

Sakata la Zanzibar lilizungumzwa pia katika House of Lords, Baraza la Juu la Bunge la Uingereza, baada ya Lord David Steel, aliyewahi kuwa kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, kumuuliza waziri wa nchi katika wizara ya mambo ya nje Baroness Anelay nini tathmini ya serikali ya Uingereza kuhusu uchaguzi wa Tanzania na hususan kuhusu yaliyojiri Zanzibar.

Akijibu Baroness Anelay alisema kwamba serikali ya Uingereza ilisikitishwa na uamuzi wa kuubatilisha uchaguzi wa urais wa Zanzibar na wa Baraza la Wawakilishi na kwamba mara kadhaa walieleza masikitiko yao kwa serikali ya Tanzania, ikiwa pamoja na kuitwa Balozi wa Tanzania jijini London aliyeelezewa masikitiko hayo.

Canada pamoja na Muungano wa Ulaya nazo pia zimekuwa na msimamo kama wa Uingereza na Marekani kuhusu kubatilishwa kwa uchaguzi wa Zanzibar. Kwa hakika, Jumuiya ya kimataifa, kwa jumla, inatambua kwamba msimamo wake ndio ufunguo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa sasa uliopo Zanzibar.

Na ndio maana jumuiya hiyo inashikilia kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar irejee kuyatangaza matokeo yaliyosalia ya uchaguzi wa Zanzibar na imtangaze aliyeshinda uchaguzi wa urais wa huko.

Pamoja na onyo la Marekani la kutishia kuinyima misaada serikali ya Tanzania, kuna tetesi katika duru za kimataifa kwamba baadhi ya nchi wafadhili wa Tanzania zimekwishaanza kushauriana ni vikwazo vya aina gani viekewe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania endapo watawala wa Zanzibar wataendelea na ukaidi wao wa kuyapuuza matakwa ya wapiga kura kwa kutomtangaza rais waliyemchagua. Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo watawala hao wanaiteka nyara demokrasia.

Ndani ya CCM, Bara na Visiwani, kuna wenye kusema kwamba wachache wao wa Zanzibar wanaong’ang’ania madaraka wadhibitiwe ili kuepusha madhara yanayoweza kuiangukia Tanzania nzima kutokana na hatua zitazoweza kuchukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Zanzibar kwenyewe kuna viroja na vichekesho. Dk. Ali Mohamed Shein anaendelea kuwa Rais akijuwa wazi kwamba si yeye aliyechaguliwa Rais. Hata hivyo, aliye mbelembele na anayeonekana kuwa anaidhibiti Zanzibar si yeye bali Balozi Seif Ali Idi, anayeendelea kuitwa Makamu wa Pili wa Rais ijapokuwa uhalali wa wadhifa wake una mushkili.

Ukweli ni kwamba serikali ya Zanzibar kama ipo basi ipo kwa mabavu. Itakuwa walioishika dola wamejipa wenyewe mamlaka ya kutawala. Na wamejipa mamlaka hayo kwa namna wanavyoifasiri wao, na kivyao, Katiba ya Zanzibar.

Vuai Ali Vuai, naibu Katibu Mkuu wa CCM, amesema kwamba uchaguzi wa Zanzibar utarejewa; Nasor Mazrui, naibu Katibu Mkuu wa CUF, anaseme hautorejewa. Mradi kila mmoja anavutia upande wake.

Baraza la Wawakilishi halipo kwa vile halina wajumbe kutokana na kubatilishwa kwa uchaguzi lakini Pandu Ameir Kificho anaendelea kuwa Spika. Mawaziri wa CCM wanaendelea kufanya kazi lakini wale wa CUF wamerejesha magari ya serikali na hawendi kazini kwa sababu wakifanya hivyo watakuwa wanaikiuka Katiba kwa vile hawakuthibitishwa kuwa ni wawakilishi.

Alipokuwa akilifungua Bunge Magufuli alisihi kuwa suala la Zanzibar litatuliwe kwa mazungumzo, lakini huku nyuma katibu wa idara ya itikadi wa kamati maalum ya CCM/Zanzibar, Waride Bakari Jabu, amesema kwamba wao hawayatambui mazungumzo yanayofanywa Ikulu, Unguja, na yanayohudhuriwa na Shein pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Viongozi wa CCM/Zanzibar faraghani wanakiri kwamba walishindwa katika uchaguzi uliopita kwa sababu vijana wengi wa CCM hawakwenda kupiga kura. Linalowashangaza ni kwamba hawajui kwa nini vijana hao waliwaacha mkono.

Katika mchafukoge wa kisiasa uliopo sasa Zanzibar, si Watanzania peke yao bali jumuiya ya kimataifa nzima inamuangalia Magufuli atacheza karata gani kuleta haki Visiwani. Ulio muhimu ni msimamo wake na si wa chama chake.

Yeye ndiye aliye jukwaani na hapo jukwaani anang’ara. Bila ya shaka wahafidhina wa Zanzibar wenye uchu wa madaraka watamlilia kwamba bila ya wao Muungano utavunjika. Swali ni kuwa jee, atakubali ahadaiwe ovyo ovyo kama hivyo au ataweza kuona mbali?

Magufuli ana nafasi ya pekee ya kuleta makubaliano. Akiitumia vizuri fursa hiyo basi chama chake hakitokuwa na ubavu wa kumzuia. Akiwadekeza wahafidhina au akisubirisubiri bila ya kuchukua hatua madhubuti basi mambo lazima yatakwenda kombo na hatokuwa na kimoja atachoweza kukifanya kuhusu suala hilo ila kuwaridhia wahafidhina. Akifanya hivyo atazidi kujiharibia mbele ya macho ya ulimwengu kwa sababu ya ukaidi wa wachache huko Zanzibar.

Share: