Makala/Tahariri

Zimbabwe: Kufikia Urais kwa kupanda mabega ya „Mzee“ ?

Na Othman Miraji

Grace Mugabe at her first political rally in Chinhoyi. She is expected to become head of the Zanu-PFMwenyezi Mungu amemjaalia sura nzuri Grace Mugabe (umri miaka 51), mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe (umri miaka 93). Bibi huyo amejipatia bahati hiyo. Lakini yeye pia ni mwanamke anayeogopwa nchini mwake. Anaogopwa si tu kwa vile yeye ni mke wa mkuu wa sasa wa nchi, lakini sababu nyingine ni kwamba, kwa mujibu wa mambo yanavyokwenda, kuna uwezekano mkubwa wa yeye siku moja kuwa rais wa nchi, akimrithi mumewe.

Karibuni Grace alitoa tamko ambalo lilitafsiriwa na watu kadhaa kama mzaha, wakalichekea na kujaribu kulisahau kwa haraka. Lakini baadae watu haohao wakaanza kulitafakari tamko hilo na wakajiuliza: Mama huyo anakusudia nini hasa kutokana na tamko hilo? Alitamka kwamba mumewe anapendwa sana na wananchi wengi wa Zimbabwe kwa kiwango ambacho hata akigombea uchaguzi wa rais, huku akiwa (yeye Robert) ameshakufa, bado mume wake huyo atakuwa na nafasi kubwa sana ya kushinda katika uchaguzi huo. Grace aliyasema maneno hayo siku chache kabla ya rais huyo kuadhimisha sherehe ya kutimiza miaka 93 tangu azaliwe. Sherehe hiyo ilifanywa kwa mbwembwe na kugharimu fedha nyingi.

Grace alitamka kwamba hata ikiwa Mwenyezi Mungu atamuita Robert Mugabe mbele ya Haki kabla ya uchaguzi ujao wa urais, ambao utaitishwa miaka miwili kutoka sasa, bado chama cha ZANU/PF kitapendekeza jina la maiti ya Robert Mugabe igombee uchaguzi huo. Ni maajabu! Mimi kwanza sijayaamini macho yangu nilipoisoma habari hiyo kutoka gazetini.

Mwezi Desemba mwaka jana Mkutano Muuu wa chama tawala cha ZANU/PF huko Zimbabwe ulilipendekeza jina la Robert Mugabe awe mgombea wa urais katika uchaguzi ujao. Kiongozi huyo amekuwa akiitawala nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kwa miaka 37 sasa tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Muingereza. Atakapomaliza kipindi hicho kijacho basi Mugabe atakuwa ana umri wa miaka 99. Atavunja rekodi iliowekwa duniani na mtu mwingine yeyote kabla yake.

Ikiwa nimefahamu vizuri ni kwamba Grace, bila ya kujali kama Robert Mugabe atakuwa hai au ameshakufa ( maiti ) wakati uchaguzi ujao unafanyika, bado mkongwe huyo aliyeongoza vita vya ukombozi atakuwa mgombea wa ZNU/PF. Kwa ufupi, wapiga kura wa Zimbabwe huenda (Mwenyezi Mungu akipitisha kudura Yake) wataenda kumpigia kura mtu aliyekwishakufa ( maiti). Na akishinda? Hilo ndilo suali gumu. Jee itaapishwa mait yake ikamate madaraka ? Hapa bado mimi ninachanganyikiwa. Huenda Grace anayaamini miujiza, kwamba punde maiti ya Mugabe itakaposhinda, yeye mwenyewe Mugabe atafufuka na ataiongoza upya Zimbabwe na yeye Grace ataendelea kubakia kuwa FIRST LADY( Mke wa Baba wa Taifa)!

Ukweli ni kwamba siku hizi „Mjomba“ au kwa wengine watamuita „Babu“ Bob anazeeka, tena kwa kasi kubwa, zaidi kuliko ile kasi tunayoishuhudia ya kuporomoka uchumi wa Zimbabwe. Usiangalie mvi zinazozidi kichwani mwake, licha ya kuzitia rangi, lakini kitizame kipara chake kinachopanuka kichwani kwa haraka mno. Uso wake unazidi kuchakaa. Babu Mugabe mara kadhaa, kutokana na umri wake mkubwa, tumemuona akijikwaa mwenyewe, miguu ikikataa kuchanganya kwa upesi pale anapotembea. Anatembea tata tata kama vile ni mtoto mdogo wa miaka minne. Anapopanda ngazi kuingia ndani ya ndege utafikiri atadondoka wakati wowote ule, wapambe wakiwa tayari kumuokota mbiombio. Anaposoma hotuba kutoka karatasini si ajabu akautanguliza ukurasa nambari tatu kabla ya wa nambari mbili. Uzee, Bwana! Tusijidanganye. Mifupa husema yenyewe, huwa mashahidi wa ukongwe wa binadamu. Mifupa inalia na kutoka machozi ndani kwa ndani na kusema „ Tumechoka, tunataka kupumzika na pia pensheni!“

Mara kadhaa humuona pichani mzee wetu huyo kutoka Harare akisinzia wakati anahudhuria vikao muhimu vya mikutano ya kimataifa inayotoa maamuzi muhimu juu uhai na kifo kwa wananachi. Karibuni raia wa Zimbabwe aliitaka mahakama ya nchi yake itoe tamko na isema kwamba Mugabe ni mzee na amefikia hawezi tena kutekeleza majukumu yake ya urais. Promise Mkwananzi alitaka Robert Mugabe atangazwe hafai. Hakimu alilikataa ombi hilo.

Robert Mugabe amepitia mambo na mitihani mingi katika maisha yake marefu. Katika shule ya misheni ya kanisa katholiki alikuwa mwanafunzi hodari, wa kupigiwa mfano. Akamaliza mafunzo yake ya chuo kikuu akisifiwa sana na waalimu wake. Pia aliuonja uchungu wa maisha magumu ya msituni akiongoza vita vya ukombozi dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Wazungu wachache katika iliokuwa Rhodesia. Ulipokuja uhuru alianza kukubalika kwa Wazungu wa nchi hiyo ambapo hapo kabla waliendesha vita vikali dhidi yake. Lakini baada ya muda si mrefu mambo yakabadilika. Wazungu wa ndani na wa nje ya nchi mpya iliopewa jina la Zimbabwe walizipinga siasa zake za kuwapa mamlaka wazawa wa nchi hiyo kumiliki ardhi. Wazungu kadhaa waliihama nchi na uchumi ukaanza kusambaratika.

Baadae, Mugabe, ambaye kwa kiasi chake ni msomi ( amejipatia digrii za vyuo vikuu akijisomea mwenyyewe gerezani), akageuka na kuwa mbishi mkubwa wa siasa za nchi za Magharibi katika Afrika. Wapinzani katika nchi yake wamekuwa wana wakati mgumu chini ya utawala wake. Lakini kwa baadhi ya Waafrika, Mugabe anabakia kuwa shujaa, jasiri, mtetezi wa Waafrika dhidi ya unyonyaji na dhuluma zinazofanywa na nchi za Wazungu dhidi ya Waafrika. Hajali kubadikwa jina la „Dikteta“. Anachojali ni anataka kuirejeshea Afrika hadhi yake iliyoporwa na wakoloni wa Kizungu.

Pindi Robert Mugabe angejipumzikia na kuondoka madarakani baada ya miaka 20 tangu alipokamata uongozi wa nchi yake, basi leo angekuwa anaheshimika kama mzee wa busara na kuyafaidi maisha yake ya uzeeni. Lakini umaarufu wake umekwenda chini sambamba na kuvurugika Zimbabwe ambayo pale alipoingia madarakani ilikuwa „Kapu la Mkate“ kwa Afrika. Ilinawiri kwa kila namna.

Zimbabwe, kiuchumi, hivi sasa imesambaratika na inatetemeka zaidi kuliko hata unavyotetemeka mwili wa mwenyewe Mugabe. Hayo yote hayatoshi. Sasa hata mke wake anamfanya kuwa kichekesho au „karagosi“ mbele ya dunia. Grace anaiambia pia dunia kwamba si muda mrefu kutoka sasa, kutokana na umri wake, Robert Mugabe siku yake ya kwenda mbele ya HAKI inakaribia. Kwa hivyo, inafaa kiongozi huyo atambue kwamba pia wakati umewadia wa yeye Mugabe kuamua nani awe mrithi wake na awache kuhepa kulijibu suali hilo.

Chama tawala cha ZANU/PF hakijitambui, wakuu wake wanatafautiana na hata wako tayari kuraruana kuhusu suala la nani atamrithi Mugabe katika uongozi. Upande mmoja kuna „Mamba“ Emmerson Mnangagwa, aliye makamo wa rais, mtiifu kwa Mzee, akiumezea mate urais. Anaungwa mkono na Wakongwe wa Vita vya Ukombozi. Upande mwingin kuna Grace, mke wa rais ( Bibi „Hiki Changu“) aliye na uchu linapokuja suala la fedha na madaraka. Anaungwa mkono na wanajeshi vijana. Si hasha wala si ajabu kwamba Grace akaihitaji hata maiti ya mumewe ishinde uchaguzi ujao. Kuna ukweli uliojificha katika tamko lake hilo la kutisha. Grace hatishiki na tamko hilo alilolitoa, kwani anaamaanisha kuwaambia watu, tena mchana kweupe, kwamba yeye anataka kuwa rais wa Zimbabwe hata ikiwa kwa siku moja, na hata ikiwa kwa kupanda juu ya mabega ya Mzee Mugabe aliye hai au aliyekufa.

Yule mwandani wa zamani wa Mugabe katika siasa, aliyewahi kuwa makamo wa rais wa nchi, Joyce Mujuru, ambaye hapo kabla alitarajiwa atavivaa viatu vikubwa vitakavyoachwa na Mugabe, sasa amegeuka kuwa mpinzani mkubwa wa Mzee. Joyce anapendwa na watu wengi. Mwenyewe ameshatangaza atamenyana na Mzee katika uchaguzi ujao wa urais miaka miwili kutoka sasa. Mungu atuweke hai sisi na pia Mzee ili tushuhudie tukeo hilo.

Katika siasa kuna watu walio na bahati ya hukabidhiwa madaraka katika kisahani cha dhahabu, kuna wale inaowabidi watumie vishindo na vikumbo kufika kileleni, na kuna wale waliokuwa tayari hata kulipia thamani ya roho zao ili waitwe „Mheshimiwa Rais.“ Si muda mrefu kutoka sasa tutajuwa njia atakayopitia Grace Mugabe.

Share: